ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 13, 2019

TANZANIA KURATIBU MAADHIMISHO YA SIKU YA UTUMISHI WA UMMA BARANI AFRIKA KWA MWAKA 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb), akizungumza na vyombo vya habari jijini Dododma kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2019. Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb), alipokuwa akizungumza nao kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2019.

Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inaratibu maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika kwa mwaka 2019 ambayo hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika amesema maadhimisho hayo kwa mwaka huu, yanatarajiwa kufanyika Nairobi, Kenya kuanzia tarehe 21 hadi 23 Juni, 2019.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, malengo ya kuadhimisha siku hii kila baada ya miaka miwili, ni kuziwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali ya Usimamizi wa Utumishi na Utawala hususan mafanikio na changamoto ili kuzitumia kama chachu ya kuboresha utoaji huduma kwa umma.

Mhe Mkuchika amesema, taasisi zitakazoshiriki katika maadhimisho hayo, ni zile ambazo huduma zake zinalenga moja kwa moja kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Uhusiano kati ya uwezeshaji wa vijana na usimamizi wa masuala ya uhamiaji: Kujenga utamaduni wa Utawala Bora, matumizi ya TEHAMA na ubunifu katika utoaji wa Huduma Jumuishi,” hivyo kuzitaka taasisi hizo kuwa mabalozi wazuri katika kuiwakilisha nchi yetu.

No comments: