Advertisements

Tuesday, September 17, 2019

Watendaji Wizara Ya Kilimo Watakiwa Wajipange Kufikia Malengo

Watendaji wa wizara ya kilimo na taasisi zake wameagizwa kufanya kazi kwa weledi na maarifa ili kuweza kufikia malengo ya uzalishaji mazao nchini.
 
Agizo hili limetolewa leo (17.09.2019) jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakati wa kikao kazi cha watendaji wa wizara ,taasisi na bodi za mazao kujadili taarifa za utekelezaji wa malengo ya mwaka 2018/2019
 
Waziri Hasunga amewajulisha watendaji hao kuwa bado wizara na taasisi zake hazijafanikiwa kufikia lengo ya uzalishaji wenye kuzingatia tija na kuwezesha kilimo kiwe cha kibiashara
 
“Takwimu zinaonyesha hatujafanya vizuri kwenye kusaidia upatikanaji wa masoko ya mazao ya wakulima nchini kwa kipindi cha mwaka 2018/2019” Waziri Hasunga alieleza
 
Aliongeza  jukumu la wizara ni kuhamasisha uzalishaji na kuhakikisha mazao ya wakulima yanaongezwa thamani  ili kuwa na soko la uhakika
 
Waziri Hasunga alisema changamoto ya masoko kwa mazao ya wakulima inahitaji kuwekewa mfumo mahsusi wa utatuzi ,hivyo ni jukumu la wataalam kuja na mipango mizuri ya utekelezaji.
 
‘Wizara yetu inasimamia aina 85 za mazao nchini  “ hii inafanya wizara kuhitaji weledi na utaalamu kupata ufumbuzi wa haraka wa  changamoto za mazao haya, alisisitiza Waziri Hasunga
 
Waziri wa kilimo ametaja  malengo sita (6)  ambayo serikali ya awamu ya tano inatumia kupima utendaji kazi wa wizara hiyo kwa mwaka 2019/2020, kwanza ni kuhakikisha nchi inazalisha chakula cha kutosha na kuwa na usalama wa chakula.
 
Pili,kilimo kinachangia upatikanaji wa fedha za kigeni, na tatu kilimo kinatoa mchango mkubwa katika pato la taifa zaidi ya asilimia 30 ya sasa.
 
Kigezo cha nne ni malighafi kiasi gani inapatikana kwa matumizi ya viwandani,tano kiasi gani cha ajira zimezalishwa katika sekta ya kilimo na sita namna gani wizara inasimamia ushirika nchini kuwa na tija na kuondoa kero.
 
Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amewapongeza watendaji wote waliopo chini ya wizara hiyo kwa utendaji mzuri uliofanikisha Tanzania kuongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kati ya nchi za Afrika Mashariki mwaka 2019
 
“Nawapongeza wote waliosaidia nchi yetu kuzalisha mahindi kwa asilimia 103 na kuongoza Afrika Mashariki hali iliyofanya nchi kuwa una utoshelevu wa chakula wa asilimia 119” alipongeza Waziri Hasunga.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini Marco Mtunga ameelezea mafanikio ya zao  hilo kuwa  hadi kufikia mwezi huu Septemba tani 301,132 za pamba zimekusanywa toka kwa wakulima ikilinganishwa na tani 222,039 mwaka 2018
 
Ameongeza kusema kuwa bodi  imefanikiwa kusambaza chupa milioni sita za viuatilifu kwa wakulima katika msimu huu 2019/2020 ili kudhibiti magonjwa kwenye zao hili.
 
Hata hivyo,Mtunga ameeleza kuwa zao la pamba linakabiliwa na changamoto kubwa ya soko kutokana na ukosefu wa wanunuzi wa uhakika. 
 
“Tunaiomba serikali iingilie kati suala la upatikanaji wa soko la uhakika la pamba hususani katika mkoa wa Katavi ambako mvua sasa imeanza kunyesha na wakulima bado hawajauza pamba yao” alisema Mtunga
 
Katika hatua nyingine,Mwenyekiti wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Monica Mbega amesema bodi imefanikiwa mwaka huu kuanza kuzalisha unga wa mahindi tani 180 kwa siku  katika viwanda vya Arusha (60),Iringa (60) na Dodoma(60) zinazokidhi viwango vya soko la kimataifa.

Imeandaliwa na ‘
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo

No comments: