Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga (katikati) akifafanua jambo wakati yeye pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipofanya ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa Mahakama Kuu Kigoma na nyumba za makazi ya Wahe. Majaji.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta akiongoza msafara wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi mara walipofika Katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma. Nyuma ya Mhe. Jaji ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga akiteta jambo na Mhe. Jaji Mfawidhi pamoja na Wakandarasi katika UKumbi wa Wazi wa Jengo la Mahakama Kuu.
Picha ya pamoja ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kigoma, Viongozi wa Mahakama na Wakandarasi wa 'Masasi Construction Ltd.'
Na Festo Sanga, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kigoma
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kigoma ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga imetembelea Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na Nyumba za Makazi za Majaji na kupongeza upatikanaji wa huduma ya Mahakama Kuu katika mkoa huo.
Ugeni huo ulitembelea miradi hiyo ya ujenzi mapema Oktoba 08, 2019 na ulipokelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta.
Katika ziara hiyo, Brigedia Jenerali Mstaafu Maganga amepongeza jitihada za Mahakama ya Tanzania katika kusogeza huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwani awali walikuwa wakisafiri umbali wa takribani kilomita 858(kwenda na kurudi) kufuata huduma za Mahakama Kuu Mkoani Tabora.
Pia amepongeza utendaji kazi wa Mkandarasi wa ‘Masasi Construction Co Ltd’ anayejenga jengo la Mahakama Kuu pamoja na nyumba za Makazi za Majaji.
“Wajumbe wenzangu tuone uwezekano wa kuwatumia wakandarasi hawa katika miradi ya ujenzi kutokana na kazi waliyoifanya katika jengo hili,” alisema Mkuu wa Mkoa
Ziara hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango ulioandaliwa na Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma kuhakikisha wadau wa Mahakama Mkoa wa Kigoma wanapata fursa ya kutembelea jengo hilo jipya na kujionea miundo mbinu iliyopo ikiwa ni pamoja na kupata elimu.
Baadhi ya wadau wakiwemo wajumbe wa Haki Jinai Mkoa, wajumbe wa vituo vya msaada wa kisheria( paralegal) Mkoa wa Kigoma, watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma, wazabuni mbalimbali waliweza kutembelea jengo hilo ambalo linatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment