Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na watumishi wa umma wilayani Tunduru wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kilichofanyika wilayani humo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na watumishi wa umma wilayani Tunduru wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kilichofanyika wilayani humo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro.
Baadhi ya watumishi wa umma wilayani Tunduru wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kilichofanyika wilayani humo
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro akimshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) kwa kuitembelea wilaya yake na kufanya kikao kazi na watumishi wa wilaya hiyo jana kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
NA JAMES K. MWANAMYOTO, TUNDURU
SERIKALI haitosita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi wa umma watakaobainika kujihusisha na rushwa ya ngono katika maeneo yao ya kazi, kwani kitendo hicho kinadhalilisha na kushusha hadhi ya utumishi wa umma nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kilichofanyika wilayani humo jana kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Mhe. Mkuchika ametoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya Walimu wa shule za msingi wilayani Tunduru kushikiliwa na vyombo vya dola kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ya ngono jambo ambalo halileti taswira nzuri kwa umma, ikizingatiwa kuwa Walimu wana jukumu la kuwalea wanafunzi katika maadili mema.
“Inakuwaje Mwalimu unaepaswa kuwa mfano bora wa kuigwa kimaadili unataka rushwa ya ngono kwa mwanafunzi, kitendo hicho kinamuathiri mwanafunzi husika kitaaluma na kisaikolojia”, Mhe. Mkuchika amefafanua.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, hivi karibuni ofisi yake imesitisha ajira ya Mhadhiri mmoja wa chuo kikuu nchini, ambaye alituhumiwa na kubainika kuwaomba rushwa ya ngono wanafunzi wa kike ili waweze kufaulu mitihani yao kwa upendeleo.
“Wanafunzi wa kike wa chuo hicho waliandika barua ya malalamiko kwenye ofisi yangu na baada ya kuwahoji na kufanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo vya dola ikabainika kuwa ni kweli hivyo akafukuzwa kazi,” Mhe. Mkuchika ameeleza.
Mhe. Mkuchika amewatahadharisha watumishi wa umma nchini kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iko kazini na ina utayari wa kumshughulikia mtumishi yeyote atakayetumia cheo chake vibaya ili kujinufaisha na rushwa ya ngono.
Aidha, Mhe. Mkuchika amesema nchi yetu imebahatika kuwa na viongozi wenye utashi wa kupambana na rushwa kuanzia Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere hadi Awamu hii ya Tano, inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amejipambanua kwa vitendo kwa kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na Wahujumu Uchumi.
No comments:
Post a Comment