ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 10, 2019

WAZIRI MKUU KUWA MGENI RASMI UZINDUZI WA MAFUNZO KWA VIJANA YA KILIMO CHA KISASA KWAKUTUMIA KITALU NYUMBA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akitoa maelekezo kwa kamati ya maandalizi alipotembelea viwanja vya Mpilipili kwa ajili ya kukagua eneo hilo utakapofanyika Uzinduzi wa Mafunzo kwa vijana ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia Kitalu Nyumba (Greenhouse) pamoja na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa Mkoani Lindi. (Kulia) ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi 
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi (wa tatu kutoka kushoto) akieleza jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama walipotembelea eneo la Ngongo mahali kilipo Kitalu Nyumba. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Andrew Massawe (wa pili kutoka kulia).

Na; Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Uzinduzi wa Mafunzo kwa vijana ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia Kitalu Nyumba (Greenhouse) pamoja na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyikia Mkoani Lindi siku ya Alhamisi tarehe 10 Oktoba, 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 9, 2019 kuhusu Uzinduzi wa Mafunzo kwa vijana ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia Kitalu Nyumba (Greenhouse) pamoja na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Mhagama alisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu Programu ya ukuzaji ujuzi kwa lengo la kuwawezesha vijana kuondokana na tatizo la ajira, kukuza ujuzi wao na kuwasaidia waweze kushiriki kwa wingi kwenye ujenzi wa taifa kwa uzalendo.

“Tumeamua kutoa mafunzo haya kwa vijana wasiopungua 18,000 katika kila halmashauri ili vijana waweze kunufaika na mradi huu kwa kujihusisha na kilimo cha Kisasa chenye tija kwao,” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa matokeo haya chanya yameletwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwawezesha vijana nchini.

“Tunaamini teknolojia hii itakapoenea kwenye maeneo mbalimbali nchini vijana watakuwa na uwezo wa kushiriki kwa wingi kwenye kilimo cha aina hii chenye tija kwao, kwani wataweza kupata mazao mengi kwenye eneo dogo,” alifafanua Mhagama.

Aidha amewasihi wananchi kufuatilia matangazo ya uzinduzi huo yatakayorushwa moja kwa moja kwenye televisheni ya Taifa (TBC) ili waweze kuona juhudi za Serikali katika kuwawezesha vijana kupitia Mafunzo ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia Kitalu Nyumba (Greenhouse).

Wakati huo huo aliwahimiza wakazi wa Mkoa wa Lindi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Nanenane, Ngongo ambapo uzinduzi wa mafunzo hayo yatafanyika na pia kutembelea viwanja vya Mpilipili ambapo Maadhimisho ya 17 ya wiki ya Vijana yatafanyika.

No comments: