Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa 13 wa shirikisho la wadau wa korosho Afrika (ACA) unaofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam tarehe 7 Novemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa 13 wa shirikisho la wadau wa korosho Afrika (ACA) unaofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam tarehe 7 Novemba 2019.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika Tasnia ya Korosho nchini Tanzania ili kutumia vyema fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo kuwekeana katika viwanda vya korosho.
Katika kipindi kirefu serikali imekuwa ikiuza korosho ghafi jambo ambalo nitapunguza kipato cha wananchi na pato la serikali hivyo kuagiza wafanyabiashara kuwekeza kwenye viwanda vya korosho.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 7 Novemba 2019 wakati akifungua mkutano wa 13 wa shirikisho la wadau wa korosho Afrika (ACA) unaofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam.
Waziri Hasunga amesema kuwa kwa sasa uwezo wa ubanguaji wa korosho ghafi nchini ni tani 50,000 ambayo ni sawa na takribani asilimia 20 ya uzalishaji wa korosho ghafi msimu wa 2018/2019.
Amesema uwezo huo ni mdogo ikilinganishwa na uzalishaji uliopo sasa na hivyo nchi inapoteza fursa ya ajira viwandani hususani kwa wanawake na vijana, kukosa mapato yanayotokana na bidhaa zilizoongezwa thamani kama vile mafuta ya ganda la korosho (Cashewnut Shell Liquid), vyakula vya mifugo na kupanua wigo wa soko la korosho.
Amesema kwa sasa kuna jumla ya viwanda 25 vya ubanguaji korosho nchini vyenye uwezo wa kubangua tani 78,000 kwa mwaka. Kati ya hivyo, ni viwanda 12 vyenye uwezo wa kubangua tani 24,660 ndivyo vinavyofanya kazi hivyo kuna fursa kubwa ya uwekezaji kwenye viwanda vya ubanguaji korosho.
Aidha, Waziri Hasunga amesema kuwa kwa upande wa wabanguaji wadogo wa korosho nchini kupitia umoja wao (UWWKT) wameendelea kuimarisha Umoja wao kwa lengo la kuongeza kiasi cha korosho kinachobanguliwa nchini.
Mpaka sasa kuna jumla ya vikundi 209 vidogo vya kubangua korosho nchini kutoka Wilaya 14. Katika msimu wa 2018/2019 vikundi hivi vimefanikiwa kubangua korosho tani 78 tu. Ukosefu wa mitaji, mashine za kubangua korosho, na masoko ya uhakika ni baadhi ya changamoto zinazokabiliwa na wabanguaji katika kundi hili.
Kwa ujumla Serikali kupitia Taasisi zake inaendelea kusimamia mikakati iliyopo ya kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi kufikia wastani wa tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2023/2024.
Mikakati hiyo ni pamoja na kupanda mikorosho mipya 15,000,000 kila mwaka kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2023/2024, kuanzisha mashamba mapya ya kuzalisha mbegu bora za korosho hususani katika maeneo mapya ya kilimo cha korosho, Kutoa elimu ya ugani kwa wakulima juu ya kilimo bora cha korosho ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu vya zao la korosho na kuhakikisha upatikanaji wa uhakiki na wa bei nafuu wa viuatilifu vya zao la korosho kwa wakulima.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyataja maeneo ambayo yapo wazi kwa ajili ya uwekezaji katika Tasnia ya Korosho hapa nchini ni pamoja na; Ubanguaji wa korosho ikiwa ni pamoja na usindikaji wa bidhaa zitokanazo na korosho; Ufunguaji wa mashamba makubwa ya korosho (Cashewnut plantations/Block farming); Usambazaji na uuzaji wa mashine za kubangua korosho; Uwepo wa ardhi ya kutosha iliyotengwa katika mikoa inayozalisha korosho kwa wingi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho; Uwepo wa sera ya viwanda katika ngazi ya Taifa.
Mhe Hasunga amesema kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazozalisha korosho ghafi yenye ubora wa hali ya juu. Korosho ya Tanzania inapendwa katika masoko mbalimbali ya Kimataifa kutokana na kuwa na ladha nzuri na ya kuvutia, rangi nyeupe ya asilia ya korosho karanga na ukubwa unaofanana (Uniform size); sifa inayopunguza gharama ya kudarajisha kabla ya kubanguliwa. Pia, faida ya kijiografia (Geographical Advantage) ya kuwahi kwa msimu wa korosho nchini miezi 6 kabla ya nchi nyingine duniani zinazozalisha korosho kwa wingi hazijaingia sokoni.
Sifa hizo pamoja na usimamizi mzuri wa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ndio kimsingi imepelekea kuimarika kwa bei ya korosho ghafi za wakulima kutoka mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2017/2018, ambapo bei ya korosho ghafi imekuwa ikiongezeka na kufikia ya juu kuwahi kupatikana ya Shilingi 4,128/= kwa kilo katika msimu wa 2017/2018.
Zao hili huzalishwa kwa wingi hapa nchini kutoka mikoa mitano ambayo ni mikoa ya Kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na mikoa ya Mashariki ambayo ni Pwani na Tanga. Kutokana na faida za kiuchumi zitokanazo na zao la hili, uwepo wa eneo la kutosha kwa kilimo na hali ya hewa maridhawa kwa kilimo cha korosho hapa nchini zao hili kwa sasa linalimwa na zaidi ya mikoa 17 ikiwemo Singida, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Songwe, Njombe, Iringa, Katavi, Tabora, Kigoma, Shinyanga na Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment