Dar es Salaam. Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimewataka wanachama wa chama hicho wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 waandike barua za kuonyesha nia.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Januari 29, 2020 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati wa mahojiano maalum yaliyorusha Kituo cha Televisheni cha ITV.
Mnyika amesema hayo baada ya kuulizwa na mtandazaji kwenye mahojiano hayo kama Chadema wanatarajia kumsimamisha aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kugombea nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.
“Waswahili wanasema linalosemwa lipo, ni kweli kwamba mnataka kumsimamisha Lissu kugombea nafasi ya urais mwaka 22020?” alihoji mtangazaji wa kipindi hicho, Farhia Middle
Akijibu swali hilo, Mnyika amesema, “mimi ni msimamizi wa uchaguzi na uteuzi wa mgombea ni sehemu ya uchaguzi, naomba kwa sasa niseme chama kinalenga kumsimamisha nani kugombea urais na katiba ya chama chetu inasema kamati kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutafiti jina la mgombea urais.”
“Ila watanzania wawe na uhakika, Chadema itasimamisha mgombea wa urais ambaye ana uwezo wa kushinda na kuleta mabadiliko ya kweli.”
Amesema kwa sasa chama kinawaalika wanachama na wasio wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao waandike barua kuonyesha nia zao.
“Katika hatua ya sasa nitoe wito sio tu kwa wenye dhamira ya kugombea urais, wanaotaka kugombea udiwani, ubunge, popote pale kwenye maeneo ya nchi yetu wajitokeze kwa kuandika barua za kuonyesha nia,” amesema Mnyika
“Kila mwana Chadema na hata ambaye sio mwana Chadema lakini anataka kugombea kupitia Chadema aandike barua sasa ya kuonyesha nia kuwa anataka kugombea kata gani, jimbo gani au nafasi gani, hatutasubiri badaye, sisi tutaingiza kwenye michakato yetu ya kichama na baadaye michakato mingine itaendelea.”
Mnyika alisema, “tunataka kufanya mkakati thabiti wa kuwaandaa watu wetu kwa mabadiliko, na kati ya watu tunaowaandaa ni wagombea, lazima tuwafundishe misingi ya chama, falsafa, itikadi ya chama ili ukiingia kwenye uongozi uwe kiongozi wa tofauti.”
“Lakini kwa mazingira tuliyonayo kwa sasa hivi, unapaswa vilevile kufundishwa mikakati, unajiandaaje kushinda? Ili yote haya yafanyike ni lazima wagombea wajulikane mapema na muda pekee wa wagombea kujulikana natoa rai kwa Watanzania wote wenye dhamira ya kugombea kupitia chadema waandike barua za kuonyesha nia” amesema
Pia, alipotakiwa kuelezea suala la Makamu Mwenyekiti Bara wa Chadena, Tundu Lissu kuchaguliwa kwenye wadhifa huo wakati yuko nje ya nchi, Mnyika amesema , “kila Mtanzania ana haki ya kuchaguliwa na Chadema ya sasa mtu anaweza kuwa nje ya nchi lakini akashiriki kwenye vikao vya kikatiba vya chama kwa kuwa katiba inaruhusu na Lissu alihudhuria mkutano na akaomba kura na wanachama waakamchagua,” amesema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba
No comments:
Post a Comment