Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye hawafai kuendelea na nyadhifa zao kutokana na mambo waliyoyafanya.
“Nitaendelea kuwapenda lakini kwenye nafasi zenu hapana. Watanzania mmenichagua kusimamia haki na utendaji kazi ndani ya Serikali ili kila fedha ya Watanzania iktumike kwa mujibu wa sheria,” amesema Rais Magufuli.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 23, 2020 katika hafla ya uzinduzi wa nyumba za Jeshi la Magereza Ukonga, jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa tume nyingi zimeundwa kuchunguza miradi ya hovyo inayosimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Magufuli amesema kutokana na sakata hilo katibu mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu ameandika barua ya kujiuzulu na amemkubalia.
“Watu wamekosa uadilifu, hivi karibuni kulikuwa na mkataba mmoja wa ajabu unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya zaidi ya Sh1 trilioni. Mradi huo umesainiwa na kamishna jenerali wa Zimamoto.”
“Haujapangwa kwenye bajeti na haujapitishwa na Bunge. Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wote wa Tanzania waliokuwa wanakwenda katika majadiliano na kulipwa Dola 800 za posho ya vikao,” amesema Magufuli, na kubainisha kuwa hata tiketi za ndege walilipiwa.
Amesema mkataba huo ni wa hovyo kwa sababu ili kuuvunja yaliyoanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa.
No comments:
Post a Comment