



MASHABIKI wa Yanga wanalijadili na kutambia bao la Mapinduzi Balama wakiamini ndio lililowarejesha mchezoni, ila unaambiwa kama kuna mchezaji aliyewanyima raha Wanasimba basi ni kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo anatetajwa alikuwa kikwazo kwa timu yao.
Kipa huyo Mkenya alifanya kazi kubwa kuokoa michomo hatari mitatu iliyokuwa inawapa Simba mabao ya mapema na pengine yangemeliza pambano hilo la Watani lililopigwa Uwanja wa Taifa.
Kiungo Mtemi Ramadhan na beki, Fikiri Magosso kwa nyakati tofauti wamemtaja kipa huyo kuwa ndiye nyota aliyefanya matokeo kuwa sare ya mabao 2-2, licha ya Simba kutangulia kufunga kabla ya Yanga kusawazisha.
"Shikhalo amefanya kile ambacho alielekezwa na kocha, alipata misukosuko mingi kipindi cha kwanza, lakini hakutetereka," amesema Fikiri Magosso.
"Simba langoni kwao ukiachana na mabao mawili waliyofungwa ambayo binafsi naona ni uzembe wa mabeki, lakini kipa wake hawakusukwa sukwa kama ilivyokuwa kwa Shikhalo," alisema Magosso.
Naye Mtemi pia amemtaja Shikhalo kuwa nyota wa mchezo huo akibainisha kwamba kama si yeye, Yanga wangefungwa hata mabao manne kipindi cha kwanza katika mchezo wa jana.
No comments:
Post a Comment