Advertisements

Sunday, January 26, 2020

TANZANIA YAFIKIA VIWANGO VYA UTOKOMEZAJI WA UKOMA

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza wakati akitoa tamko la siku ya Ukoma duniani alilolitoa kwenye makazi ya waathirika wa ugonjwa huo yaliyopo kijiji cha msamalia kilichopo Hombolo mkoani Dodoma.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akimvalisha mmoja wa waathirika wa ugonjwa wa Ukoma alipotembelea makazi ya kituo hicho yaliyopo kijiji cha msamalia,Hombolo mkoani Dodoma

Na Catherine Sungura, Dodoma
Tanzania tayari imefikia viwango vya kidunia vya utokomezaji wa Ukoma vya kuwa na chini ya wagonjwa 10 kati ya 100,000 mnamo mwaka 2006.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akitoa tamko la siku ya Ukoma duniani alilolitoa kwenye makazi ya waathirika wa ugonjwa huo yaliyopo kijiji cha msamalia kilichopo Hombolo mkoani dodoma
“Kutokana na juhudi za serikali, viwango hivyo vya utokomezaji vimeendelea kuboreshwa na kushusha idadi ya waathirika wa Ukoma kutoka wagonjwa 4.3 kati ya watu 100,000 mnamo mwaka 2014 na kufikia wagonjwa 3 kati ya watu100,000 mwaka 2019".
Aidha,amesema jitihada kubwa za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli zimeweza kupunguza viwango vya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukoma kutoka wagonjwa 43 kati ya watu milioni moja mwaka 2014 hadi kufikia wagonjwa 26 kwa watu milioni moja mwaka 2019.
"Vile vile, tumepunguza idadi ya watoto wanaougua Ukoma kwa asilimia 41, kutoka watoto 90 mwaka 2014, hadi 53 mwaka 2019.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2019, mikoa yote isipokuwa Lindi ilikuwa tayari imefikia kiwango cha utokomezaji.
Waziri huyo aliongeza kuwa zipo Halmashauri 16 ambazo bado hazijafikia viwango hivyo na kuzitaja Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya Lindi, Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Masasi, Nanyumbu, Morogoro, Mvomero, Mpanda, Nkasi, Manispaa ya Shinyanga, Manispaa ya Kigoma, Kibaha, Mkinga na Tunduru.
“Nipende kuzikumbusha Halmashauri hizi na mikoa kuongeza kasi ya kutokomeza Ukoma na kuhakikisha kaya zote hatarishi na zenye wagonjwa wa Ukoma zinafikiwa, wanakaya wanachunguzwa dhidi ya ugonjwa wa Ukoma na wale ambao tayari wanaugua wanatibiwa kikamilifu".Alisisitiza Waziri Ummy
Waziri Ummy aliitaka Mikoa na Halmashauri zihakikishe zinatenga bajeti katika mipango yao ili kuendesha kampeni za uhamasishaji, uelimishaji, na uibuaji wa wagonjwa wapya,kauli mbiu ya siku ya Ukoma duniani mwaka huu ni"Tuthamini haki na utu wa waathirika wa ukoma kwa kutokomeza ubaguzi,unyanyapaa na chuki".

No comments: