Advertisements

Sunday, January 26, 2020

Hasheem Thabeet Safari ya kurudi NBA - 1

Hasheem Thabeet Safari ya kurudi NBA -Hasheem Thabeet-Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani-NBA-
INDIANA, MAREKANI . YUKO wapi Hasheem Thabeet? Ndiyo amefulia kabisa? Bado anacheza mpira wa kikapu? Nini malengo yake? Haya ni maswali yanayosumbua vichwa vya Watanzania wengi wapenda michezo.

Ikumbukwe kuwa Thabeet ndiye Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA), wengi waliamini mafanikio yake yangefungua milango kwa Watanzania zaidi kutua NBA.

Lakini, tofauti na matarajio ya wengi, mambo hayakwenda kama yalivyotarajiwa licha ya kutabiriwa makubwa Thabeet ambaye alikuwa mtu wa pili kuchaguliwa kujiunga na NBA kwa vijana wa chuo mwaka 2009, alidumu kwenye ligi hiyo kwa miaka mitano tu na kupotea.

Wakati wengi wakiamini amemaliza na amefulia moja kwa moja, lakini Thabeet anaamini kitu tofauti kabisa akili yake inaamini bado ana nafasi ya kupambana na kurudi NBA ndiyo maana kila kukicha anahaha kwenye ligi za chini kupata timu ya kumfungulia njia. Ndiyo maana alijaribu kupitia G League (ligi ya chini ya mpira wa kikapu ya Marekani), anaweza kurudi NBA na kuuthibitishia Ulimwengu kuwa nafasi ile hakuipata kwa bahati mbaya.

Thabeet aliamini akiwa sehemu ambayo hana presha kama awali, anaweza kupambana na kuhakikisha anarudi NBA na kumalizia kile alichokianza na kiukweli amepania kurudi juu.

Aliamini kupitia timu ya Fort Wayne Mad Ants aliyokuwa anachezea katika G League anaweza kutoka, maana timu ile walimuamini na kumthamini na chini unaweza kuona mfano tu maisha yake yalivyokuwa katika timu hiyo kiasi cha kuamini ni njia ya kurudi NBA.

Ilikuwa siku ya mechi ya G League, Thabeet alitembea kutoka benchi hadi katikati ya Uwanja kwa hatua tatu tu. Na kuangalia mashabiki huku akisikiliza namna walimshangilia. Mashabiki 3,000 walikuwa wamegawanyika katika Uwanja huo wenye kuingiza watu 13,000 waliokaa.

Mashabiki hao walikuwa uwanjani hapo kuangalia mechi ya G League kati ya Fort Wayne Mad Ants dhidi ya Erie BayHawks michuano ambayo Thabeet anaitumia katika kuhakikisha anarudi NBA.

Baada ya kuingia uwanjani Thabeet ambaye bado mashabiki wanamkumbuka kama mtu aliyechaguliwa katika nafasi ya pili kuingia NBA mwaka 2009, alikabidhiwa kipaza sauti na kuwashukuru mashabiki wake.

“Habari za jioni,” alisema Thabeet huku akiwa ameshika kipaza sauti kwenye kiganja chake kikubwa. “Kwa niaba ya wachezaji wenzangu, familia na waandaaji tunapenda kusema asante na tunawatakia msimu mzuri wa sikukuu, tunashukuri kwa sapoti yenu.”

Kisha Thabeet alirudisha kipaza sauti kwa muongoza shughuli na kurudi kukaa na wenzake benchi, lakini yeye alikalia stuli ambayo ilimruhusu kunyoosha miguu yake mirefu na timu yake maana hakuhitajika tena uwanjani.

Baada ya mechi dhidi ya Erie, Thabeet alikaa mbele ya kabati lake kwenye vyumba vya kubadilishia nguo akipitia kitabu cha Sapiens: A Brief History of Humankind. Ili kuchangamsha akili yake.

Kisha akabadilisha nguo na kuvaa traki suti la kijivu na raba aina ya Air Force 1s zilizoendana na nguo zake. Mchezaji mwenzake Ike Nwamu, alimtania kwa kumwambia, “Lazima utakuwa mtu mwenye hadhi kubwa sana kuvaa viatu hivyo.”

Thabeet alicheka na kurudi uwanjani, kisha akampa boksi la pipi aina ya Reese’s Pieces shabiki wa kwanza mdogo aliyekutana naye. Kisha akakaa sehemu ili kuwapa nafasi mashabiki waliotaka kupiga naye picha au saini waweze kumfuata.

Mashabiki wawili waliomfuata walikuwa ni mtu na mtoto wake wa kike mwenye miaka minne. Kwanza mtoto yule aliona aibu kumwambia Thabeet jina lake, Lakini baadaye kakakubali kugonga na staa huyo.

Baada ya kugonga Thabeet alirusha mkono wake juu kama mtu aliyeumia. Mtoto yule wa kike akaanza kucheka na kumpiga tena mkononi na kumfanya azidi kujifanya kaumia zaidi na kumfanya azidi kucheka.

“Inabidi unionee huruma aisee!” Thabeet akamwambia binti yule. “Nahitaji huu mkono maana bado sijamaliza kucheza mpira wa kikapu.”

Hayo ndiyo maisha ambayo Thabeet alikuwa anaishi katika timu ya Fort Wayne Mad Ants, mashabiki walimkubali huku yeye mwenyewe akiamini kuwa timu hiyo ndiyo ina tiketi yake ya kurudi NBA. Lakini unajua nini kilimtokea?

ITAENDELEA

Mwananspoti

No comments: