ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 6, 2020

Yanga yaijibu Simba yamleta winga wa TP Mazembe

Mwanaspoti-Yanga-yaijibu Simba-Tanzania-yamleta winga-TP Mazembe-Mapinduzi Cup
By KHATIMU NAHEKA

Dar es Salaam.Yanga imewajibu Simba kwa kumleta winga wa TP Mazembe, Owe Bonyanga ametua nchini leo anatarajia kuungana na kikosi hicho Zanzibar kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Ujio wa Bonyanga kutoka TP Mazembe umeijibu Simba ambayo ilimsajili winga Deo Kanda kutoka kwa mabingwa hao wa DR Congo mwanzoni mwa msimu huu.

Winga Bonyanga alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa ameambatana na meneja wake na kupokelewa Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM, Hersi Said.

Ujio wa Bonyanga ni kama kutaka kuwafunga midomo watani wao, waliwapiga bao kwa Luis Jose Miquissone aliyekuwa UD Songo ya Msumbiji waliyekaribia kumvuta Jangwani na inaelezwa jamaa alikuwa kwenye hesabu za Yanga ila alikuwa akitakiwa na DC Motema Pemba ya kwao kwa ajili ya kukiongeza nguvu kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo inaelezwa mpango huo ulifeli kutokana na utata uliojitokeza, kwani inalezwa jamaa ana mkataba ndani ya timu yake ya TP Mazembe ambao kuna kipengele kinachoitaka timu hiyo kushirikishwa katika klabu anayotaka kwenda winga huyo.
Mazembe hawakuwa na hiyana kumruhusu Bonyanga kwenda Angola alipoenda kuzichezea Sagrada Esperança na hata Sporting de Cabinda kwa mkopo, lakini lilipokuja suala la kwenda Motema Pembe likawa gumu kuruhusiwa na hapo Yanga wakanasa mchongo.
Urahisi wa Yanga umekuja baada ya Bonyanga kutotaka kurejea TP Mazembe kwani kocha wake, Pamphile Mihayo Kazembe hakuonyesha kumhitaji sana kwa vile chaguo lake ni winga Muavory Coast, Rufin Gnanzou ambaye Yanga ilitangulia kumtaka ila ikabanwa na mkataba wa kumchomoa klabuni hapo.
Mazembe hawakutaka kumruhusu winga huyo kirahisi kwenda kuiimarisha DC Motema Pembe ambapo utata huo ukainufaisha Yanga ambao wakafanya mambo ya haraka kumvuta nchini.
SIMBA YAZUIA MAMILIONI
Unaambiwa buana sare ya mabao 2-2 iliyopata Yanga dhidi ya Simba, juzi Jumamosi imezuia mamilioni kwa nyota wa Jangwani, baada ya kupishana na Sh200 milioni kwa kutoshinda.
GSM kupitia Bilionea wao Ghalib Mohamed waliwashtua nyota timu hiyo dakika chache kabla ya mchezo kuanza wakiwaambia endapo wangeshinda kama kawaida kulikuwa na motisha ya kuvuna kiasi cha Sh200 milioni.
Ahadi hiyo iliwachanganya wachezaji ambapo licha ya kupambana kurudisha mabao mawili waliyotanguliwa na Simba, lakini walishindwa kupata bao la ushindi ili wavune fedha hizo.
Hata hivyo inaelezwa kwamba huenda mabosi hao wakawafikiria cha kuwapa vijana wao kwa jinsi walivyopambana na kupindua matokeo hayo.

No comments: