Advertisements

Friday, February 21, 2020

Hatima ya Kinana, Membe, Makamba wakati wowote

By Peter Saramba, Mwananchi mwananachipapers@mwananchi.co.tz

Mwanza. Hatima ya makada waandamizi wa CCM, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Bernard Membe itajulikana wakati wowote baada ya kukamilika kwa siku saba zilizotolewa na Kamati Kuu ya CCM kwa kamati ya nidhamu kukamilisha suala lao na kuwasilisha taarifa.

Februari 12, 2020, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliwaambia waandishi wa habari kuwa Kamati Kuu ilitoa muda huo kuwasilisha katika vikao husika.

Kinachosubiriwa sasa ni kuona iwapo makada hao waandamizi watasamehewa au watachukuliwa hatua.

Juhudi za kuwafikia viongozi na watendaji wa CCM kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa baada ya simu ya kiganjani ya Katibu mkuu, Dk Bashiru Ally, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Hamphrey Polepole na Makamu Mwenyekiti, Phillip Mangula kuita bila kupokewa.

Hata hivyo, wachambuzi wametoa maoni tofauti kuhusu hatua wanazoweza kuchukuliwa viongozi hao, wengi wakikubaliana kuwa hatua yoyote itakayochukuliwa iwe kuwasamehe au kuchukua kuwaadhibu itazingatia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kinana na Makamba ambao ni makatibu wakuu wastaafu wa CCM pamoja na Membe aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje, walihojiwa kwa nyakati tofauti Dodoma na Dar es Salaam kutokana na kutuhumiwa kwa makosa ya kimaadili.

Agizo la viongozi hao kuhojiwa lilitolewa na Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana Mwanza, Desemba 13, 2019.

Wakati Membe alihojiwa Dodoma, Kinana na Makamba walikwenda katika ofisi ndogo ya chama hicho tawala Lumumba jijini Dar es Salaam, chini ya Makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Mangula.

Vigogo hao walihojiwa baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mtu anayejiita mwanaharakati, ambaye alikuwa akitoa tuhuma dhidi yao.

Nguvu ndani, nje ya chama

Ukweli uliodhahiri ni kwamba CCM itakuwa na wakati mgumu kuamua adhabu ya kuwatimua wakati huu ambao Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu kutokana na vigogo hao kila mmoja kuwa na nguvu ya kisiasa ndani na nje ya chama.

Kinana ndiye aliyeongoza kampeni zote za wagombea urais wa CCM tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uliporejeshwa nchini mwaka 1992, akiwa meneja wa kampeni na baadaye katibu mkuu.

Pia Kinana ndiye aliyeongoza kampeni ya kurejesha haiba ya CCM kwa umma kwa kuzunguka nchi nzima kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kuna wakati aligeuka mbogo dhidi ya viongozi na watendaji wa Serikali kwa kufikia kuwaita mizigo.

Kwa upande wake, Makamba ambaye alitumika katika mikutano kadhaa ya kampeni za CCM mwaka 2015 na pia ni mjuzi na mbobezi wa masuala ya siasa za kimkakati na mbinu za ushindi, sifa ambayo ni lazima itavifanya vikao vya uamuzi vya chama kutafakari mbinu za kumaliza suala hilo.

Membe, kachero na mwanadiplomasia si tu alikuwa miongoni mwa wana CCM 38 waliowania uteuzi wa kupeperusha bendera ya CCM mwaka 2015 na kuishia hatua ya tano bora, bali pia ni mmoja wa wajumbe wa kamati za kimkakati katika chaguzi kadhaa zilizopita ndani na nje chama.

Wachambuzi wanena

Mchambuzi wa masuala ya siasa na mtetezi wa haki za binadamu jijini Mwanza, Edwin Soko alisema uamuzi wa CCM dhidi ya vigogo hao utajikita katika misingi miwili.

Ametaja misingi hiyo kuwa ni maelezo na utetezi wao mbele ya kamati na pili ni faida na athari kwa chama kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

“Sitarajii kama CCM wanaweza kufanya kosa la kuwafukuza Kinana, Makamba na Membe. Licha ya ubobezi, uzoefu, ushawishi na nguvu zao ndani na nje ya chama; viongozi hawa pia wanajua mbinu za ushindi za chama hicho,” aliongeza Soko.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema kitendo cha uongozi wa CCM kuwafikisha makatibu wakuu wastaafu mbele ya kamati ni cha udhalilishaji na kutothamini mchango wao kwa chama na Taifa.

“Ningekuwa kiongozi wa CCM, ningewaita wazee hawa faragha kusikiliza hoja zao na kuyamaliza kimya kimya. Busara lazima itumike kumaliza tofauti ya mawazo na maoni kwa sababu ni jambo la kawaida kutofautiana mitazamo hata kama mko chama kimoja,” aliongeza Mpangala.

Mwanasheria na mchambuzi wa masuala kisiasa nchini, Dk Onesmo Kyauke alisema iwapo watatiwa hatiani, Kinana na Makamba wanaweza kupewa adhabu ya karipio au onyo kutokana na ukweli, “Ila Membe anaweza kukumbana na adhabu ya onyo na kuwekwa chini ya uangalizi na kuzuiwa kugombea kwa muda fulani.”

No comments: