Advertisements

Friday, February 21, 2020

Mwanamke Aliyeishi Kwenye Ndoa na Binamu Yake, Aanika Mazito


CARO NDUTI ni mama ya watoto wawili na kwa muda wa miaka minne ndoa yake ilifana sana, lakini anasema alifurahia matunda ya ndoa hiyo kwa muda tu kama alivyomsimulia mwandishi wa BBC, Anne Ngugi.

Caro ambaye alizaliwa mwaka wa 1981 anasema kuwa alilelewa vijijini na kwamba alikuja mjini Nairobi, Kenya, kwa mara ya kwanza alipoanza maisha ya ndoa na pia maisha ya kutafuta ajira. Alikutana na baba wa watoto wake wakiwa washirika kanisani, kama vijana wadogo wote walikuwa shuleni na walikuwa wameshikilia maadili ya kidini.

Wakati huo wawili hao wakiwa washirika wa kanisa, hawakufikiria mapenzi yangeliota mizizi kati yao. Baada ya shule alikutana tena na rafiki yake wa kanisani mwaka wa 2002 alipoijiunga na taasisi ya mafunzo.

Anakumbuka alikuwa akimtembelea katika taasisi ya mafunzo aliyokuwa anasoma na hapo wakaanza uhusiano wa kimapenzi, licha ya kuwa alikuwa bado anasoma walianza kuishi pamoja kama mume na mke, japo taasisi yenyewe ilikuwa ya bweni.

“Mpenzi wangu alinisihi nipate ujauzito kabla ya kumaliza chuo kikuu, kwani alikuwa na wasiwasi kuwa wakati ningefuzu kutoka chuo hicho ningemtoroka. Nilimpenda sana na sikuwa na ufahamu wa maisha kwani nilikuwa ni msichana mdogo tu, nikakubali kupata ujauzito,” Caro aliendelea kusimulia.


Baada ya kumaliza mwaka wa mwisho wa chuo alikuwa na ujauzito wa miezi kadhaa na kwamba hata jamaa za mpenzi wake walikuwa wanamfahamu kama mke wake.

Caro anasema aliongeza kuwa sherehe za kumaliza shule zilifana sana: “Mume wangu alishiriki sherehe yangu ya kumaliza masomo huku akiandamana na watu wa familia yake wakiwa wamejaza gari kuja kunichukua kitendo hicho kilinifanya kujihisi kupendwa sana na familia ya mume wangu”.

Mwaka wa 2003 Desemba alijifungua mtoto wao wa kwanza ambaye ni mvulana, na kulingana na Caro walikuwa jamii iliyokuwa na furaha na utangamano, anasifu mumewe kwa kuwa baba na mpenzi mzuri nyakati hizo.

Baada ya muda pia Caro alijifungua mtoto wa pili mwaka wa 2006 ambaye alikuwa ni mvulana pia, lakini katika muda huo alianza kugundua kuwa tabia za mumewe zilikuwa zinampa wasiwasi na hofu; alikuwa anaona dalili za mwanamme aliyekuwa na wanawake wengine nje ya ndoa.

Anasema kuwa kwa kuwa alikuwa na umri mdogo sana wa miaka 22 aliogopa kumuuliza mumewe maswali ya udanganyifu katika ndoa kwa hio aliishi kana kwamba halikuwa linafanyika licha ya kuwa lilikuwa linamkera.

“Nilikuwa najiuliza hakuna chochote ninachokosa katika ndoa, kwa hiyo wacha afanye mambo yake nje mradi mimi nimeridhika, mwanamke ni kuvumilia,” Caro aliongezea.

Cha kushangaza ni kuwa alikuwa anawajua baadhi ya wanawake mumewe alikuwa anashiriki ngono na wao, mara nyingi mumewe hakuficha michepuko yake haikuwa siri.

“Wakati mwingine nilikuwa nawafahamu, tulikuwa tunakula na kunywa na wao katika majumba ya starehe, ni kana kwamba mume wangu alihisi kuwa nilikuwa muoga wa kuuliza maswali,” Caro alisema.

Wakati mmoja binamu yake ambaye anamtambulisha kama dada yake, kwani kulingana naye walilelewa katika mazingira sawa, Caro alilelewa na mama ya binamu wake, kwani mama yake Caro aliaga dunia akiwa na umri wa miaka saba, kwa hiyo mlezi wake alikuwa ni yule shangazi yake ambaye alimfananisha kama mama , na kwa hiyo watoto wa shangaziye walikuwa kama ndugu na dada zake.

Binamu wake alipomaliza shule ilibidi pia aanze kutafuta maisha mjini; kile anachofahamu ni kuwa yale matembezi ya binamu yake kwake ndio chimbuko la mahusiano ya kimapenzi kati yake na mume wake. Anakumbuka kuwa mume wake alikuwa hata harudi nyumbani tena, hata ilifika mahali ambapo mume wake alikuwa hafichi tena uhusiano wake na binamu yake na Caro.

“Nakumbuka mume wangu alikuwa ananipigia simu na kuniambia kuwa hatarejea nyumbani atakuwa na binamu yangu, sikuwa na la kufanya ila kuvumilia ”

Cha kushangaza anasema kuwa yule dada yake (binamu) aliyekuwa na uhusiano na mumewe alianza kumtukana mara kwa mara kupitia ujumbe wa simu.

Licha ya kwamba alikuwa akimuonyesha mume wake ujumbe huo wa matusi, hakuwahi kumtilia maanani.

”Nilikuwa napokea ujumbe wa matusi kutoka kwa binamu yangu, tena matusi mabaya sana,” aliendelea kusema.

Kila mara walipokutana na mumewe na alimuuliza mume kwa nini anakubali binamu yake amtusi na mumewe alikuwa anamjibu kwa ukali “mbona asikutusi?”

Uhusiano kati ya mume wa Caro na dadake uliendelea hadi pale uhusiano huo ulipogunduliwa na jamaa zao, licha ya kuwa mama ya binamu yake kupinga uhusiano huo.


Mwaka wa 2008 Caro aliamua kuwa angemwachia binamu yake mume.

Caro aliposhindwa na maisha hayo aliondoka na kuanza kuishi pekee yake. Lakini baada ya muda mume wake alimtafuta na wakarejea tena nyumbani.

Licha ya kuwa binamu yake alikuwa anaishi na mumewe kama wanandoa, aliamua kurudi nyumbani kwa maslahi ya watoto wake ambao alihisi walihitaji malezi ya baba yao. Sasa ikawa mtindo ni Caro na mumewe kuachana , baada ya muda wanarudiana, kwani licha ya uhusiano wake na dada yake kuwepo, binamu yake alijifungua watoto wawili wa kike.

Caro alikuwa amekubali kulea watoto wa binamu yake kwa minajili ya amani na utengamano kwenye jamii, na kwa kuwa alitamani sana uhusiano kati ya binamu yake na mumewe uishe kabisa. Cha ajabu alipokuwa anapigania uhusiano wa hao wawili uishe upande mwingine aligundua kuwa mumewe alikuwa anafanya uhusiano na kila msichana wa kazi aliyekuwa anaajiri wakati huo.

Maisha yakawa magumu sana, na hapo ndipo Caro akashindwa kuvumilia tena maisha ya mumewe ya michepuko ya kila wakati sio kwa binamu yake, ila hata kwa wasichana wa kazi aliokuwa anawaajiri.
Caro aliondoka siku mmoja kwenye ndoa yake na hakurudi tena kwa mumewe.

Caro anasema kuwa aliyekuwa mumewe angali na dada yake au binamu yake kama mume na mke lakini kwake yeye alishawasamehe kabisa. Caro anasema kuwa haijakuwa rahisi kwani tabia ya mume wake ilimfanya kuwa na uchungu mwingi pamoja na hali ya kujichukia.

“Imechukua muda sana kwangu kujikubali na pia kujiona kama mwanamke mrembo, nilitamani sana baba ya watoto wangu awe karibu nao, lakini michepuko yake ilizidi sana ” Caro alisema.

Anawasihi wanawake ambao wanapitia mambo kama aliyopitia kuwa wa haraka kusamehe na waachilie mambo ya kale, kwani anasema kuwa uchungu ambao wanawake huhifadhi katika mioyo yao, huwa sio mzuri katika maisha ya kawaida yao, na wakati mwingi huwa kikwazo kikubwa katika mahusiano mengine ya maisha yao.

Caro anawaeleza kuwa wanawake kama hao wasife moyo wa kuanza upya hata kama ni katika hali ya kimapenzi au kukubali kupendwa..

GPL

No comments: