ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 25, 2020

IJUE SOCIAL SECURITY NUMBER (SSN) YA MAREKAN

Sio kitambulisho, ni namba. Tuanzie hapo!

Naipongeza serikali ya Tanzania kwa kuanzisha kitambulisho cha taifa. Ni hatua muhimu sana kimaendeleo. Kwa Marekani, kitambulisho hicho cha taifa kinafanana sana na kitu kinachoitwa Social Security Number (SSN). Marekani haina kitambulisho cha taifa zaidi ya paspoti. Hata leseni za gari ni za majimbo, hazijaandikwa United States Driving license.

Kuna mengi kwenye namba hii ya Marekani ambayo yanaweza kukiboresha kitambulisho cha taifa cha Tanzania.

SSN ni namba ambayo ndio uti wa mgongo wa mfumo wote wa maisha ya wamarekani. Ni namba ambayo watu hawalazimishwi kuipata. Wanaitafuta wenyewe kwa sababu bila ya hiyo namba maisha ni shida sana nchini Marekani.

Namba hii hutolewa kwenye kadi isiyo na picha. Picha kwenye vitambulisho huweza kughushiwa. Vilevile picha hubadilika kulingana na umri wa mtu. Picha huwekwa kwenye vitambulisho vya muda maalumu kama miaka mitano au kumi, kama ilivyo kwenye leseni za gari, ukazi wa mji na paspoti. Kadi hii ingekuwa na picha, kadi nyingi zingekuwa na picha za watoto wachanga. Kwa sababu wamarekani wengi hupewa namba hii wiki chache baada ya kuzaliwa.

Ni namba ya kudumu nayo maisha yote. Inabadilishwa kwa dharura tu kama ya wizi au mambo mengine ya kiusalama. Wageni na wahamiaji wanaokidhi vigezo pia hupewa namba hii.

Sharti kubwa sana katika kupewa namba hii ni kuonyesha cheti cha kuzaliwa. Vitambulisho vyote vya maana vya mtu kama leseni ya gari, paspoti, cheti za ukazi havitolewi bila ya kuwa na namba hii.

Ni namba muhimu sana, mtu anaweza hata kumficha mkewe. Haiwekwi kwenye vitambulisho. Haiwezekani polisi akukamate umpe kitambulisho chenye namba yako hii muhimu kijamii.

Ni namba tofauti kwa kila mtu. Serikali hutumia namba hii kufuatilia vipato vya watu, ili iweze kukusanya akiba na kulipa mafao mbalimbali kwa wenye kuhitaji msaada wa serikali kwa kukosa kazi, ugonjwa, uzee, kustaafu na kadhalika.

Ni namba ambayo hutumika kukusanyia kodi za kipato kwa kila mtu. Inasaidia kuhakikisha nchi nzima kila mtu analipa kodi zilizopangwa. Mwishoni mwa mwaka kodi huhakikiwa. Kwa alielipa kodi zaidi ya alichotakiwa kulipa anarudishiwa pesa, na alielipa kodi kidogo hudaiwa kodi.

Nje ya serikali namba hii hutumika kupatia mikopo, kufungua akaunti, kujiandikisha shule, kupata bima, kununua nyumba, gari na mengi mengineyo.

Kubwa zaidi hii ndio namba inayotumika kuombea kazi, kufungua biashara, kwa wageni hutumika kuombea vibali vya kufanya kazi . Kadi za wageni zina maandishi haya “Valid for work only with DHS authorization”. Ikimaansha mwenye kadi hiyo haruhusiwi kufanya kazi ndani ya Marekani bila ya kibali za kufanya kazi.

Ni namba inayokamatisha wahalifu, ni namba inayokamata wazazi wasiotoa matunzo kwa watoto wao, ni namba inayomuwakilisha mtu katika kila kitu chake muhimu.

Kwa taifa zima ni namba inayorahisisha kufanya sensa na kujua nchi ina watu wangapi. Ni namba inayowafanya wamarekani kupokea mafao yao ya uzeeni hata wakiwa nje ya nchi. Jambo ambalo lina manufaa makubwa kiuchumi kwa nchi zinazopokea wastaafu kutoka Marekani.

Ni namba ambayo inaweza kuwatoza kodi wamarekani hata wakifanya kazi nje ya Marekani. Tanzania inaweza pia kunufaika kwa kutumia namba hii ili kufikia vipato vya raia au wazawa wake wanaofanya kazi nje ya Tanzania.

Yote haya yakijumlishwa, ni jambo lenye manufaa kwa Tanzania kuruhusu wazawa wake wote kupata namba hii kihalali hata kama wako nje ya Tanzania. Hasa kwa kuzingatia kuwa hakuna kompyuta duniani yenye orodha ya majina ya waliokana uraia wa nchi zao. Na wala hakuna kompyuta itakayowajua watakaochukua kitambulisho cha taifa cha Tanzania na baadae wakachukua uraia wa nchi nyingine.

Kwa kutumia kauli ya profesa Lumumba wa Kenya “there is a sense” katika haya “and I submit” waraka huu kwa watanzania wote.

Mungu Ibariki Tanzania!

Zain Hamza
Washington DC

No comments: