
Dar es Salaam. Marekani imepiga marufuku Watanzania kushiriki bahati nasibu ya kupata viza kuingia nchini humo.
Katika bahati nasibu hiyo, viza hutolewa kwa watu takribani 50,000 kutoka nchi zenye kasi ndogo ya maendeleo huingia nchini humo kwa ajili ya kufanya kazi.
Miongoni mwa nchi zilizopigwa marufuku kushiriki bahati nasibu hiyo ni Suda, huku nchi za Nigeria na Eritrea raia wake wakipigwa marufuku kuomba viza za kuhamia Marekani.
Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) limeripoti kuwa ofisa wa ngazi ya juu nchini Marekani amesema kuwa nchi hizo sita zimeshindwa kufikia kiwango stahiki cha ulinzi na kupashana taarifa.
"Nchi hizi kwa sehemu kubwa zinataka kutoa msaada lakini kwa sababu mbalimbali zimefeli kufikia viwango vya chini tulivyoviweka," amesema Naibu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Chad Wolf.
Wolf amesema maofisa wa Marekani watakuwa tayari kushirikiana na nchi hizo sita ili kuimarisha matakwa ya ulinzi kwa nchi hizo ili iwasaidie kutoka kwenye orodha hiyo.
Nchi hizo mpya zinaungana na nchi nyingine saba ambazo raia wake wamepigwa marufuku kuingia Marekani tangu mwaka 2017 ambazo ni Libya, Iran, Somalia, Syria, Yemen, Korea Kaskazini na Venezuela.
Mbali na bahati nasibu, Marekani imemzuia mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda kuingia nchini humo.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa Januari 31, 2020 na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema mkuu huyo wa mkoa amezuiwa kuingia nchini humo pamoja na mkewe, Mary Massenge.
Inaeleza kuwa anazuiwa kutokana na tuhuma za kushiriki kukandamiza haki za binadamu.
Inafafanua kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu alioufanya jijini Dar es Salaam ni pamoja na kunyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wao.
"Wizara ina taarifa za uhakika kuwa Makonda amehusika katika uvunjifu huo wa haki kupitia nafasi yake kama mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,” inasema taarifa hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo ametumia akaunti yake ya Twitter kutangaza zuio hilo.
Pia taarifa ya Wizara hiyo imeitaka Serikali ya Tanzania kuheshimu haki za binadamu ikiwemo uhuru wa kujieleza na haki ya mikutano ya amani.
Mwananchi limemtafuta Makonda jana usiku na leo asubuhi Februari Mosi, 2020 bila mafanikio na simu yake ya mkononi haikuwa hewani.
No comments:
Post a Comment