Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari leo jijini Dar, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alianza kwa kuthibitisha tukio hilo kwa kusema Mbowe alivamiwa usiku wa kuamkia leo na watu wasiojulikana wakati akiwa anaingia nyumbani kwake jijini Dodoma.
Alisema, baada ya shambulio hilo alikimbizwa kwenye Hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma na kwamba bado anaendelea na matibabu lakini wanafanya utaratibu wa kumsafirisha hadi jijini Dar kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Mnyika alilitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kwa uhuru ili waliohusika na jambo hilo wafahamike kwa haraka na kuchukuliwa hatua stahiki.
“Taarifa ya kamanda wa polisi imetoa viashiria kwamba kama ilivyokuwa kwa tukio la kupigwa risasi kwa mheshimiwa Tundu Lissu ambapo polisi walijitokeza harakaharaka, katika tukio hili pia wamejitokeza harakaharaka wakitaka kwa namna yoyote lisihusishwe na siasa.
“Kwa sababu wamesema wanafanya uchunguzi hawapaswi kufunga milango ya uchunguzi na kuliita hili tukio la kawaida kwa sababu tukio hili lina viashiria vya kisiasa kwani taarifa zinaeleza wakati wanamshambulia walisikikika wakisema ‘tuone utafanya vipi hizo kampeni’,” alisema Mnyika na kuongeza.
“Waliomshambulia Mwenyekiti Freeman Mbowe kuna maneno walikuwa wanayatamka zaidi ya haya ya kwamba wewe unaisumbua sana Serikali, walikuwa wanasema kwamba hatudhamirii kukuuwa lakini pamoja na kutamka maneno hayo walikuwa na silaha ambazo hawakuzitumia
…..
“Walimshambulia maeneo mbalimbali ya mwili katika hatua ya sasa eneo lililoathirika zaidi ni mguu wake wa kulia lakini kwa kuwa ameshambuliwa maeneo mbalimbali ya mwili bado uchunguzi unaendelea kujua kiwango cha madhara ambayo ameyapata.
“Siku chache kabla ya mwenyekiti kushambuliwa kulisambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikimnukuu mtu anayejiita ni mchungaji wa kitaifa anaitwa kwa jina la Mashimo akizungumza akiashiria kuna tukio la kiongozi wa upinzani kushambuliwa na akataja jina la mwenyekiti Freeman Mbowe.
“Sio tukio la kawaida polisi kama wanavyosema, wafanye uchunguzi wa kina,sio tukio la kawaida kama waliomshambulia wanamwambia wewe unaisumbua sana Serikali tuone utafanyaje kampeni,tukio kama hili polisi hawakutakiwa kutoa kauli waliyoitoa kwamba ni tukio la kawaida.
“Bado uchunguzi unaendelea kujua kiwango cha madhara ambayo ameyapata na kwa mazingira hayo hayo ya uchunguzi na mahitaji ya kiuchunguzi ndio maana Chama kimeona ni vema aletwe jijini Dar es salaam kwa ajili ya matibabu zaidi na uchunguzi zaidi.
Kwenye mkutano huo, Mnyika alisema Mbowe ameathirika zaidi katika mguu wa kulia japo bado uchunguzi zaidi unaendelea.
Kamanda wa Polisi Dodoma, Gilles Muroto alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi zaidi unaendelea.
Stori: Erick Evarist, Risasi Mchanganyiko
No comments:
Post a Comment