ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 18, 2020

Waepuke Marafiki Hawa Ili Ufanikiwe Penzini

TUNAZIDI kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai. Ni Jumatatu nyingine tunakutana hapa kupeana elimu ya maisha ya uhusiano na maisha kwa ujumla.

Kwenye dunia hii, ni vizuri sana kujifunza mambo mbalimbali kupitia maandishi kama hivi, inasaidia sana katika kujiongezea uwanja mpana wa kung’amua mambo.

Maisha ya uhusiano yana changamoto nyingi, unazokutana nazo sasa hivi siyo utakazokutana nazo kesho au baadaye.

Unayoyashuhudia wewe, si anayoyapitia mwenzako, kupitia wazungumzaji au waandishi kama hivi, unaweza kupata mambo mengi mno ambayo yamekusanywa pamoja. Karibu ujifunze!

Kama mada inavyojieleza hapo juu. Kuna watu ambao kimsingi kwenye maisha yako, unatakiwa kuwaepuka kama ukoma ili uweze kwenda vizuri na mwandani wako.

Wengi wetu hujikuta tunakosea kwa kushindwa kujiepusha na watu wasiofaa kwenye maisha yetu na kujikuta tukiishia kwenye mfarakano kama si kushindwa kabisa kupiga hatua.

Marafiki zangu, mbinu ya kuwaondoa marafiki wabaya maishani, inatumiwa na watu wengi hata katika maisha ya kawaida.

Watu wengi ambao wamefanikiwa kiuchumi, waliamua kuwaondoa watu wenye mtazamo hasi kwenye maisha yao na taratibu wakaanza kufanikiwa.

Hata kwenye uhusiano wa kimapenzi, epuka sana kuzungukwa na watu ambao wana mtazamo hasi juu ya maisha.

Watu ambao hawakushauri mambo ya msingi, hawataki usimame kwenye msimamo mzuri wa uhusiano, waepuke.

Watu wanaotaka uwe mbeambea kama wao, wanaotaka muishi vijiweni, mumseme fulani bila sababu za msingi, hao ni watu wa kuwaepuka.

Watu ambao hawana cha kukushauri zaidi ya kupiga soga na kushinda vijiweni hao hawafai kabisa.

Kwa kawaida, mwanadamu ukizungukwa na watu wa aina hii, hata kama wewe si mtu wa hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa wewe kuwa kama wao.

Ndugu zangu, heshima ya mtu inaanzia kwake yeye mwenyewe. Anza kujipa thamani kwanza wewe ili watu unaowataka waweze kuja kwenye maisha yako.

Ukiwa mtu wa kulewa au malaya, hata marafiki zako watakuwa wa aina hiyohiyo. Anza kujipa thamani unayoitaka maishani mwako.

Ukishafanikiwa kwenye hilo, anza sasa kumsaka mtu ambaye atakuwa na mawazo kama yako.

Ukiishi na mtu mwenye mawazo kama yako, anayewaza mambo chanya, hakika mtafanikiwa.

Kuishi na mtu ambaye yeye anawaza hasi tu, anakukatisha tamaa kwa kila unalotaka kufanya, ndugu zangu ni shida!

Ishi na mtu anayetaka maendeleo, mtu anayeiwazia kesho yenu. Mtu anayetamani kuona mnayaendea mafanikio.

Mtu huyo hatokei tu bahati mbaya, lazima wewe mwenyewe ujitengenezee mfumo huo wa maisha.

Ujitambue, ujipe hadhi ambayo unaitamani. Elekeza akili yako katika kupata mtu wa aina hiyo, akija basi hakika mtafanikiwa sana.

Pamoja na wewe kujiweka kwenye nafasi hiyo, lakini kubwa zaidi ni kumuomba pia Mungu. Akuoneshe mtu sahihi wa aina yako.

Mungu atakupa unachotaka sawasawa na maombi yako maana anakuwa ameziona pia juhudi zako. Umefanikiwa kujiwekea misingi mizuri ya maisha, atakupa wa kufanana na wewe.

Kupanga ni kuchangua, chagua kuzungukwa na watu wazuri, mtu mzuri atakuja kwa ajili yako. Hawezi kuja kama umezungukwa na watu wa ajabuajabu.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Marafiki mnaweza kunifuata kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.GPL

No comments: