ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 18, 2020

Wanafunzi 73,101 wachaguliwa kujiunga kidato cha tano


Ramadhan Hassan -Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema wanafunzi 73,101 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.

Jafo alisema idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 121,251 ambapo wengine wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu na vyuo vya ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte).

Aliwataka wanafunzi wote wa bweni kuripoti shuleni Julai 18, mwaka huu na masomo yataanza rasmi Julai 20, huku akiwatahadharisha watakaoshindwa kuripoti ndani ya wiki mbili tangu shule kufunguliwa nafasi zao zitachukuliwa na wengine.

Jafo alitoa kauli hiyo jijini Dodoma jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema wanafunzi hao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano ni kutoka shule za Serikali, zisizo za Serikali, waliosoma nje ya mfumo rasmi na waliosoma nje ya nchi baada ya matokeo yao kupata ulinganifu wa Baraza la Mitihani Tanzania.

Jafo alisema shule 434, zikiwamo 32 mpya za kidato cha tano zilizoanza mwaka huu, zimepangiwa wanafunzi.

Alisema kati ya wanafunzi hao wa kidato cha tano waliochaguliwa, wasichana ni 35,005 sawa na asilimia 47.9 na wavulana 38,096 sawa na asilimia 52.1.

Alisema kati yao, 1,572 wamechaguliwa kujiunga na shule za wanafunzi wenye ufaulu mzuri zaidi (vipaji maalumu), ikiwemo wanafunzi wanne wavulana wenye mahitaji maalumu.

“Pia katika uchaguzi huu, kuna wanafunzi 183 wa mahitaji maalumu ambapo wasichana ni 82 na wavulana ni 101,” alisema Jafo.

Kuhusu vyuo, alisema wanafunzi 9,264 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya ufundi, vyuo vya afya na vyuo vya ualimu katika ngazi ya stashahada.

Alisema wanafunzi 38,886 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya ufundi vinavyosimamia na Nacte,

Wamepangwa katika vyuo na taasisi mbalimbali kama vile ardhi, biashara, maendeleo ya jamii, uvuvi, mifugo, kilimo, mazingira, mipango ya maendeleo vijijini.

“Wanafunzi ambao hawataripoti wiki mbili tangu tarehe ya kufungua shule, nafasi zao zitachukuliwa na wanafunzi wengine ambao hawakupangiwa shule katika awamu hii,” alisema Jafo.

Alisema hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule kwa sasa ngazi ya mikoa, halmashauri na shule.

Jafo alisema wanafunzi wanaotaka kufanya mabadiliko ya kozi au chuo walichochaguliwa wanaruhusiwa kufanya hivyo kuanzia Agosti 1 hadi 30 kupitia mtandao wa Nacte.

Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri za Kyerwa, Momba, Mtwara, Ubungo na Nanyamba ambazo hazina shule za kidato cha tano na sita, wahakikishe kufikia Januari 30, mwakani zinakuwa na shule hizo hususani za masomo ya sayansi na hisabati na ziwe zimetengewa bajeti ya chakula

No comments: