ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 20, 2021

Biden Kuapishwa Leo, Trump Atoa Kauli ya Mwisho Ikulu


RAIS Donald Trump amelihutubia taifa la Marekani kabla hajaondoka madarakani na kusema: “Tumefanya kile ambacho tulikuja kukifanya na tumefanya mambo mengine mengi.”

Katika video aliyoiweka kwenye mtandao wa YouTube, alisema; “Mapambano yalikuwa makali, vita ilikuwa ngumu… kwa sababu hicho ndicho mlinichagua kukifanya”. Trump anaondoka madarakani akiwa bado hakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa Novemba, ambao ulimuibua Joe Biden kuwa rais.

Biden ataapishwa leo Jumatano

Wiki mbili za mwisho za utawala wa Trump zimekumbwa na ghasia baada ya wafuasi wake kuvamia jengo la bunge la Capitol Hill, wakipinga matokeo ya uchaguzi.

“Ghasia za kisiasa ni shambulio la kila kitu tunachothamini kama Wamarekani. Kamwe hatuwezi kuvumilia,” Trump alisema katika video yake, ambapo bado hakutambua ushindi wa mrithi wake

Trump alisema nini zaidi?


Trump mwenyewe ameshtakiwa kwa uchochezi juu ya shambulio la uvamizi wa bunge na atakabilina na kesi hiyo baada ya kuondoka madarakani. Ikiwa atakutwa na hatia, anaweza kuzuiwa kufanya shughuli zozote za umma.

Trump ni rais wa kwanza kushtakiwa mara mbili. Kesi yake ya kwanza ilimhusisha na kutumia wadhifa wake vibaya nchini Ukraine lakini alifanikiwa kushinda kesi hiyo baada ya kupata kura nyingi kutoka kwa chama chake cha Republican.

Ghasia hizo za kisiasa zimefunika changamoto inayoikabili Marekani ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona ambapo zaidi ya Wamarekani 400,000 wamekufa kutokana na Covid 19 na watu milioni 24 wameathirika na janga hilo.

Katika ujumbe wake, Trump alisema utawala wake umeweza kujenga uchumi wa Marekani kwa kiwango cha juu zaidi katika historia ya dunia. Soko la hisa la Marekani limeongezeka, ingawa uchumi bado uko katika wakati mgumu kutokana na janga la corona.

Waajiri wengi walisitisha ajira za watu mwezi Desemba, mauzo ya rejareja yalishuka katika miezi ya hivi karibuni huku madai ya wasiokuwa na ajira yakiwa yameongezeka. Donald Trump, katika hotuba yake ya dakika 20, alisema utawala wake umefanya kile ambacho walikuja kukifanya na wamefanya zaidi.

“Vita ilikuwa kubwa , mapambano yalikuwa makali, ni maamuzi magumu kwa sababu hiyo ndiyo iliyowafanya mnichague,” alisema. Ghasia na chuki aliyoipandikiza Trump wakati wa kuondoka kwake madarakani vimesababishwa na uvamizi wa jengo la bunge la Capitol wiki mbili zilizopita, ambao vimeharibu sifa zake na itamchukua muda mrefu kubadili mtazamo wa watu juu ya hilo.

Baada ya miaka minne za mila na desturi zilizozoeleka, watu wanamtathmini kuw, Trump anaondoka madarakani akiwa ameiacha Marekani ikiwa imebadilika – kiuhalisia na kimtazamo na hata taifa hilo limebadilika moja kwa moja. Kuwa aliweka ahadi na ameitekeleza.

Biden anajitayarisha vipi kuingia madarakani?

Biden na mke wake wanaondoka nyumbani kwao Delaware kwenda kuishi Ikulu Washington, ambapo rais huyu mteule alihudumu kwa miaka 36 kama seneta kabla hajawa makamu wa rais wa Barack Obama kuanzia mwaka 2008 mpaka 2016.

“Nikifa, Delaware itaandikwa katika moyo wangu,” alisema kwa hisia wakati akihutubia kuaga na Jumatano (leo) ataenda Ikulu na katika jengo la bunge Capitol kwa ajili ya kuapishwa majira ya saa sita mchana.

Uapisho huu hautafanana na uapisho mwingine wowote: Washington ina ulinzi mkali tangu jengo la Capitol kuvamiwa siku chache zilizopita ambapo maelfu ya askari wanafanya doria nje ya ukuta wa White House.

Idadi ndogo tu ya watu itaruhusiwa kuhudhuria kushuhudia shughuli hiyo ya uapisho, tofauti na miaka ya nyuma ambapo mamia ya maelfu ya watu walikuwa wanahudhuria tukio hilo.

Miongoni mwa watu ambao hawatahudhuria shughuli hizo Rais Trump. Ataondoka kwenda Florida Jumatano asubuhi. Rais wa kwanza kutohudhuria shughuli za uapisho wa mrithi wake alikuwa Andrew Johnson mwaka 1869.
 Chanzo GPL

No comments: