ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 15, 2022

COASCO: TUNZENI KUMBUKUMBU MPUNGUZE HATI CHAFU



Na Ahmad Mmow, Lindi.

Viongozi na watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS) na chama kikuu cha ushirika cha RUNALI mkoani Lindi wametakiwa kutunza kumbukumbu ili vyama wanavyoongoza visipate hati chafu.

Wito huo ulitolewa jana mjini Ruangwa na mkaguzi wa shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika(COASCO) wa mikoa ya Lindi na Mtwara, Nelice Mbanza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya msingi na ushirika(AMCOS) vilivyo chini ya chama kikuu cha ushirika cha RUNALI.

Mbanza alisema kutokuwepo kwa utunzaji sahihi wa kumbukumbu na nyaraka nichangamoto na miongoni mwa sababu zinazosababisha baadhi ya vyama vya ushirika kupata hati chafu vinapokaguliwa.

Alisema ni kama jambo la kawaida kuona vyama vinashindwa kuonesha kumbukumbu mbalimbali vinapoombwa na shirika hilo ili vikaguliwe. Hali inayosababisha vipewe hati chafu.

Alizitaja baadhi ya sababu zinazosababisha vyama kushindwa kuonesha kumbukumbu kuwa ni utunzaji mbaya wa nyaraka na tabia ya viongozi na watendaji kuondoana kiholela madarakani.

Alibainisha kwamba tabia ya kuondoana kiholela madarakani inayosababisha viongozi wazamani na wapya kushindwa kukabidhiana nyaraka za vyama vyao.

Aliwaasa viongozi na watendaji wapya wanapoingia madarakani waache tabia ya kukimbilia kujua benki kuna kiasi gani cha fedha badala ya kuomba kukabidhiwa nyaraka na mali zote za vyama.

" Msikimbilie kuangalia akaunti benki badala ya nyaraka. Hii ni changamoto, tukitaka kumaliza tatizo la hati chafu kuwe na utunzaji mzuri wa kumbukumbu na makabidhiano sahihi ya ofisi," alisisi Mbanza.

Mtaalamu huyo alisema baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika wanashindwa kuonesha vitu muhimu kwenye taarifa zao. Ikiwemo kutokuwepo vielelezo vya matumizi yaliyofanyika. Hali ambayo pia nichangamoto inayotakakiwa kuondolewa ili vipate hati safi.

Nae mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma ambae alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja yaliyoandaliwa na chama kikuu cha ushirika cha RUNALI alivitaka vyama viwekeze katika miradi yenye tija.

Alisema viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza vyama hivyo wanatakiwa wajue kwamba fedha na mali zinazotumika kwa uwekezaji ni zawanachama. Kwahiyo wanachama wanataka waone na wanufaike na uwekezaji unaofanywa na vyama vyao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa RUNALI, Audax Audax Mpunga alisema katika msimu wa 2021/2022 changamoto nyingi ambazo zilisababisha malalamiko kwa chama kikuu, vyama vya msingi na serikali katika misimu iliyopita zilitatuliwa nakusababisha kutokuwepo lawama.

Mpunga alizitaja baadhi ya changamoto hizo ni uhaba wa vifungashio na kuchelewa malipo ya wakulima. Hali ambayo imesababisha kutokuwepo wakulima wanaodai.

Mafunzo hayo yaliyo andaliwa na RUNALI zilitolewa mada mbalimbali kwa washiriki hao. Ikiwemo maandalizi wa mashamba ya mikorosho kuhusu kupulizia, kupalilia na awamu za upuliziaji.

Mada nyingine ni usimamizi wa makarani na namna ya kuondoa changamoto ya upotevu wa mazao ghalani.

No comments: