Wakati Serikali ikimsisitiza kila Mtanzania kulipa kodi kutokana kipato halali anachoingiza, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) halikufanya hivyo lilipowalipa wafanyakazi wake posho ya Sh61.64 bilioni hivyo kuikosesha Serikali kodi ya Sh17.4 bilioni.
Wakati Tanesco ikifanya hivyo, Mdibibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amesema mashirika 12 kati ya 200 ya umma aliyoyakagua mwaka 2020/21 hayakuwasilisha kodi yaliyoikata Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiasi cha Sh90.08 bilioni.
Katika kiasi hicho, CAG amesema kiasi hicho kinajumuisha Sh53.57 bilioni walizolipwa wafanyakazi wa kudumu na Sh8.07 bilioni kwa watumishi wa muda hivyo kukiuka Kifungu cha 7 (1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato kinachoagiza mapato yatokanayo na ajira yanapaswa kukatwa kodi.
“Nilipopitia makato ya kodi ya mishahara kwa watumishi wa kudumu, watumishi wa mkataba na watumishi wa muda kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2021, nilibaini posho za wafanyakazi jumla ya Sh61.64 bilioni hazikukatwa kodi ambazo ni faida kwa wafanyakazi hivyo kusababisha Serikali kupoteza Sh15.5 bilioni kutoka kwa wafanyakazi wa kudumu na Sh1.9 kwa wafanyakazi wa muda kinyume na sheria ya kodi ya mapato,” amesema Kichere.
Mwenendo huo, CAG ameonya kwamba unaweza kusababisha kuliongezea shirika gharama za faini itakayotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kutowasilisha makato ya kodi kwenye posho za wafanyakazi hao.
CAG ameikumbusha Tanesco kuhakikisha posho inazowalipa watumishi wake zinatozwa kodi kwa mujibu wa sheria.
Mbali na Tanesco, katika mashirika ya umma 200 aliyoyakagua, CAG amebaini 12 yalikata Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kodi ya mishahara, na kodi ya kuendeleza ujuzi lakini hayakuiwasilisha TRA. Mashirika hayo kwa jumla hayakuwasilisha Sh90.08 bilioni.
“Nilibaini kuwepo kodi ambazo hazikuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa muda mrefu hivyo kuongeza hatari ya kuongezeka kwa madeni ya kodi kutokana na ongezeko linaloendelea la riba na adhabu,” amesema Kichere.
Sheria ya Kodi ya Mapato inataka kila taasisi inayokata kodi ya zuio kuwasilisha mapato hayo kwa kamishna wa kodi ndani ya siku saba baada mwisho wa mwezi na Sheria ya Mamalaka ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya Mwaka 2015 inataka kila mwajiri mwenye waajiri wanne au zaidi kutoza na kuwasilisha kwa kamishna, Kodi ya Ujuzi na Maendeleo (SDL) kila mwisho wa mwezi.
Mashirika ya umma yenye wataalamu, wadau wanasema yanapaswa kuonyesha mfano. “Sasa kama wao wanakula kodi wanazotakiwa kuwasilisha TRA unadahni mwananchi atafanyaje,” alisema Juma Nassoro, mjasiriamali jijini Dar es Salaam.

No comments:
Post a Comment