ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 9, 2022

BALOZI WA TANZANIA NCHINI ETHIOPIA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO UNECA


Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Kamisheni Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika, Mhe. Innocent Eugene Shiyo akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA), Mhe. Dkt. Vera Songwe.
Mhe. Balozi Shiyo akiwa katika picha ya pamoja na Dkt. Songwe mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.


Mhe. Innocent Eugene Shiyo, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Kamisheni Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe.Dkt. Vera Songwe, Katibu Mtendaji wa Kamisheni Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA).

Wakati wa hafla hiyo, Mhe. Dkt. Vera Songwe alimpongeza Balozi Shiyo kwa kuteuliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) yenye Makao Makuu Jijini Addis Ababa, Ethiopia na amemkaribisha na kumtakia heri katika utekelezaji wa majukumu yake.

Wakati wa mazungumzo yao, Balozi Shiyo na Dkt. Vera Songwe wamekubaliana kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na UNECA katika masuala ya kipaumbele ikiwemo utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, Mpango wa Maendeleo wa Afrika wa Agenda 2063 na juhudi za kukwamua uchumi dhidi ya madhara ya UVIKO-19.

Dkt, Vera Songwe ameeleza utayari wa UNECA kuisadia Tanzania kujenga na kuimarisha uwezo katika mikakati ya kukuza sekta za utalii,afya, kilimo,sekta binafsi, ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), mapambano dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi na uwezeshaji Wanawake kwenye matumizi ya Teknolojia.

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika ilianzishwa mwaka 1958 kwa ajili ya kukuza maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii katika nchi za Afrika, kukuza Mtangamano wa Kikanda na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya Afrika.

No comments: