Advertisements

Monday, May 29, 2023

MAKAMU WA RAIS AKIFUNGUA MKUTANO WA 37 WA ALAT


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipokea zawadi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilioandaliwa na uongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) leo tarehe 29 Mei 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala  za Mitaa  Tanzania (ALAT) unaofanyika katika Kituo cha  Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC)  tarehe 29 Mei 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa ALAT Sima Constantine Sima wakati alipowasili katika Kituo cha  Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC)  kufungua Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala  za Mitaa  Tanzania (ALAT) leo tarehe 29 Mei 2023. (Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Angellah Kairuki)

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Angellah Kairuki wakati alipowasili katika Kituo cha  Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC)  kufungua Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala  za Mitaa  Tanzania (ALAT) leo tarehe 29 Mei 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka Mkurugenzi wa ASAS Bw.Ahmed Asas juu ya bidhaa za maziwa zinazozalishwa na kampuni hiyo wakati akitembelea mabanda ya maonesho yaliopo nje ya Kituo cha  Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) alipowasili kufungua Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala  za Mitaa  Tanzania (ALAT) leo tarehe 29 Mei 2023.


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia mipaka na majukumu yao katika utendaji wa kazi ili kuepusha migogoro na miingiliano katika kuwahudumia wananchi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

 Amesema ni lazima watendaji na viongozi wote wa kisiasa kufanya kazi kwa pamoja na kufanya mazungumzo ya kujenga kwa manufaa ya wananchi panapotokea hoja au mitazamo tofauti katika utekelezaji.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi viongozi hao kutambua lengo kuu katika nyadhifa zao ni kuwaletea wananchi maendeleo na siyo migogoro baina yao hivyo ni muhimu kuheshimiana, kuwajibika, kushirikiana kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuondoa vikwazo vyovyote vinavyoweza kukwamisha miradi hiyo. 

Pia amehimiza ushirikiano baina ya Madiwani na Wakurugenzi wa Halmashauri na kuondokana na tabia ya Madiwani kutoa maazimio dhidi ya Wakurugenzi pamoja Wakurugenzi kutowaheshimu Madiwani.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa Mapato na kudhibiti uvujaji wa mapato katika maeneo yao. 

 Ametaja tathmini ya taarifa za mapato kutoka katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na vyanzo vingine vilivyokusanywa kupitia mashine za POS imebaini katika baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa fedha hazipelekwi katika akaunti husika za benki hivyo amewasihi kuzingatia taratibu za fedha na kudhibiti matumizi yasiyo na tija.

Aidha amewahimiza Madiwani kusimamia vema Halmashauri zao na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato. 

Makamu wa Rais amemtaka Waziri wa TAMISEMI kuwachukulia hatua mara moja Viongozi na Watumishi wanaobainika kufanya matumizi mabaya ya fedha za umma, vitendo ambavyo husababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa kiwango cha chini kwa kuwa fedha zilizopangwa kwenda kwenye mradi husika huenda  kwenye mifuko ya viongozi na watumishi wasio waaminifu.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia utawala bora, kukomesha unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, usimamizi wa Nidhamu, Maadili na Uwajibikaji pamoja na kushirikiana na jamii katika kutoa elimu na kulinda maadili ya vijana. 

Pia ameagiza kuimarisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira pamoja na usafi ili kuwa na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Angellah Kairuki amewahimiza viongozi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia vema Halmashauri pamoja na kuwahamasisha na kuwasimamia wananchi katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.

Pia amesema Wizara itaendelea kushirikiana vema na ALAT katika kuzisaidia Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuweka msukumo kwa Halmashauri 56 ambazo hazijafikia makusanyo ya shilingi bilioni 2 au zaidi kwa mwaka ili ziweze kuongeza mapato. 

Halikadhalika ameziasa Halmashauri kuwa chachu na tija katika kupokea wawekezaji na wafanyabiashara katika maeneo yao ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara bila vikwazo.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Constantine Sima amesema Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa imefanikiwa kuziunganisha na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuwezesha kupungua kwa hati chafu za ukaguzi.

Ameongeza kwamba Jumuiya hiyo inasisitiza Halmashauri zote kuweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha thamani halisi ya fedha inaonekana katika miradi inayotekelezwa. Amesema mkutano huo ni jukwaa la kubadilisha uzoefu, maarifa na mifano bora katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa.

Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unakwenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Miundombinu iliyoboreshwa ni chachu ya utoaji wa huduma bora katika Mamlaka za Serikali za Mitaa

 

 

No comments: