Tuesday, June 25, 2024

FAMILIA ACHENI KUONEANA AIBU KATIKA MALEZI YA WATOTO


Baadhi ya watoto wakitoa burudani katika maadhimisho yaliyofanyika kimkoa
Na Khadija Kalili, Michuzi Tv
IMEELEZWA kuwa kutokana na tabia ya jamii kuoneana aibu ndani ya familia kumesababisha vitendo vya ukatili kuendelea ndani ya jamii ambapo hali hiyo imezipeleka familia pabaya hasa watoto kufichwa baadhi ya mambo

Mkoa wa Pwani umesema kuwa utachukua hatua kali kwa watu wanaowafanyia ukatili watoto na kuwakwamisha kufikia ndoto zao na kukosa haki zao kwa ujumla.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala wakati wa Siku ya Mtoto wa Afrika kimkoa iliyofanyika Mjini Kibaha.
Twamala amesema kuwa baadhi ya taarifa zinaonesha kuwa wanaofanya vitendo hivyo ni ndugu wa karibu.

"Ukatili unafanywa na ndugu wa karibu ambapo familia zinashindwa kuchukua hatua sababu ya kuogopa muhali hili hatulikubali,"amesema Twamala.

Amesema kuwa kutokana matukio hayo kufanywa na baadhi ya wanafamilia ambapo humalizana kifamilia badala ya kupeleka kwenye vyombo vya sheria.

"Tuwalee watoto wetu katika maadili mazuri ili kujakupata viongozi bora wa kesho na wao pia watakuwa wazazi bora wa baadaye hivyo tuwapatie haki zao za msingi ikiwemo afya na lishe ili kuwaondolea udumavu,"amema Twamala.

Aidha ameongeza kuwa anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawekea mazingira mazuri watoto ikiwa ni pamoja na kupata elimu, huduma za afya na huduma nyingine za msingi.

Akisoma risala ya watoto wa Mkoa wa Pwani Evelin Mhema amesema kuwa baadhi ya changamoto ni pamoja kufanyiwa vitendo vya ukatili mimba za utotoni, ubakaji, vipigo na vitendo vingine vinavyowanyima haki zao.

Mhema amesema kuwa watashirikiana na viongozi wakiwemo walimu ili waweze kufikia ndoto zao walizojiwekea kwa kusoma kwa bidii na kutii wazazi na walezi wao.

Kwa upande wake Said Mwinjuma amesema kuwa matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa changamoto kwa vijana na kusababisha mmomonyoko wa maadadili.

Mwinjuma amesema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwalinda watoto wao kwa kuwapatia malezi bora ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya na wasiwaache wajilee wenyewe na wawapatie elimu na stadi za kazi.

Wakati huohuo Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga amesema kuwa watoto pia wanaowajibu wao kujilinda kwa kutotembea usiku na kwenda kwenye mabanda ya video na kulindana wenyewe kwa wenyewe.

Mlenga amesema kuwa pia wasipokee zawadi au kuomba fedha kwa watu wasiowafahamu na wazazi wawalinde watoto kwa kutokuwa wakali sana pindi watoto wanapowakosea wawaelekeze kwa upendo.

No comments: