Monday, July 29, 2024

NAIBU WAZIRI MKUU DKT.BITEKO MGENI RASMI UZINDUZI WA SERA YA TAIFA YA BIASHARA 2003 TOLEO LA 2023



WIZARA ya Viwanda na Biashara imefanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003 na kutoa toleo la Sera hiyo la 2023 (National Trade Policy 2003 Edition 2023).

Akizungumza na Wanahabari Julai 28,2024 Jijini Dar es Salaam Waziri wa Viwanda na Biashara Seleman Jafo amesema Sera hii ina dhamira ya kuweka Mfumo na Mkakati mathubuti unaolenga kuboresha mazingira yetu ya biashara, kuongeza ukuaji wa kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.

" Sera hii ni marejeo ya Sera ya mwaka 2003 ambayo imefanyiwa marekebisho ili iweze kuendana na mabadiliko ambayo yametokea katika nyanja mbalimbali kikanda na Kimataifa."

Ameongeeza kuwa sera hiyo inayoongozwa na kauli mbiu isemayo “Ushindani wa Biashara katika kuchochea Kasi ya Mabadiliko ya Kijamii na Kiuchumi yanayoongozwa na Viwanda” inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Julai 30, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar Es Salaam.

Pia amesema Mgeni Rasmi katika Hafla ya Uzinduzi wa Sera hiyo ni Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Mhe Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb). Hafla hiyo pia itahudhuriwa na washiriki 300 wanaojumuisha wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Umma, Taasisi Binafsi, Mashirika ya Dini, Wabia wa Maendeleo, Mabalozi, Vyama vya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda na wafanyabiashara.

No comments: