Sunday, August 11, 2024

TANZANIA YASISITIZA ULIPAJI MICHANGO SADC


Kulia ni Mratibu wa Kitaifa wa Masuala ya SADC kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Bw. James Msina wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika tarehe 10 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha Kamati ya Fedha ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilichofanyika tarehe 10 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.

TANZANIA imeahidi kukamilisha mchango wake wa mwaka katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kuzisisitiza nchi nyingine wanachama kufanya hivyo ili kuiwezesha Jumuiya hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Hayo yamejiri wakati wa Kikao cha Kamati ya Fedha cha Jumuiya ya SADC kilichofanyika tarehe 10 Agosti 2024, Harare, Zimbabwe.

Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba ambaye ameambatana na Mratibu wa Kitaifa wa Masuala ya SADC kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Bw. James Msina.

Akichangia katika mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba amesema kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa majukumu yanayotekelezwa na Jumuiya kwa ustawi wa kanda hivyo, itaendelea kuwa mwanachama hai na kukamilisha michango yake mapema ili kuwezesha Jumuiya ya SADC kutekeleza vyema shughuli zake, ambazo nchi yetu ni mnufaika.

‘’Tanzania inaahidi kukamilisha michango yake ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Jumuiya zenye maslahi kwa nchi wanachama, ikiwemo Tanzania, hivyo napenda kusisitiza kwamba Tanzania itatimiza ahadi hiyo siku chache zijazo’’ alisema Dkt. Mwamba.

Aidha, mapendekezo ya kikao hicho yatawasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri la SADC kwa ajili ya kufanyiwa kazi katika mkutano wake utakaofanyika tarehe 13-14 Agosti, 2024.

Pamoja na masuala mengine kikao hicho kimejadili masuala yafuatayo:- Hali ya Michango kwa Nchi Wanachama; Hali ya Michango kwa Washirika wa Maendeleo; Taarifa ya utekelezaji wa Taarifa ya Fedha kwa mwaka 2023/24 na Utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Kikanda.

Masuala mengine yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho yanahusiana na Bajeti ya Nyongeza na Uhamisho wa Vifungu vya Bajeti, Taarifa za athari za kibajeti za rasilimaliwatu; Mpango wa Kati wa Mapato na Matumizi wa mwaka 2023/24-2026/27 na Taarifa ya Kamati ya Ukaguzi ya SADC.

No comments: