Tuesday, November 26, 2024

JAMII YATAKIWA KUTOA TAARIFA UKATILI UNAPOFANYIKA.



Na John Walter -Manyara

Wito umetolewa kwa wananchi kuungana na serikali kutokomeza ukatili wa kijinsia Kwa kutoa taarifa sahihi pindi wanapoona vitendo hivyo vikifanyika pamoja na kutoa ushahidi mahakamani.

Kauli hiyo imetolewa  Novemba 25, 2024 na Askofu wa kanisa la Elim Pentecoste Peter Konki ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni maalum ya siku 16 za kupinga ukatili kwa Wanawake na wasichana kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii iliyofanyika Babati mkoani Manyara.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Umoja wa vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya ameiomba Serikali ya Mkoa wa Manyara kuwashirikisha Waandishi wa Habari katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Manyara Anna Fisso amesema asilimia 60 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatokea katika Mazingira ya nyumbani kwakuwa wanaofanya vitendo hivyo ni ndugu wa karibu ambao wanaaminiwa na familia.

Amesema kumekuwa na matukio ya kikatili ambayo yanafanywa na ndugu wa karibu ambapo watuhumiwa wengi huwachukuliwa hatua za kisheria kutokana na kesi hizo kuzimaliza kifamilia.

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara Zacharia Mtigandi, Amesema Mkoa wa Manyara ni wa pili kwa matukio ya ukatili , hivyo chama hicho kimekuwa kikiandaa semina za kupinga ukatili na kuwawezesha washiriki wa semina hizo.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake