Diwani wa Kata ya Mshangano ,Samuel Mbano akionesha barua ya kujiuzulu
Diwani wa Kata ya Mshangano ,Samuel Mbano aliyejiuzulu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Ruvuma.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya James Danny Mgego akithibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwa diwani wa Kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro Ruvuma.
Diwani wa Kata ya Mshangano katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, Samuel Mbano, ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya udiwani.
Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na kile alichokitaja kama kufanya kikao bila ya idhini ya chama na kujadili maendeleo ya kata yake bila kuwashirikisha viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kutozingatia ilani ya chama.
Mbano amesema kuwa amejiuzulu kwa hiari yake ili kulinda heshima ya chama na maslahi ya serikali yake kwa ujumla.
Aidha, amesisitiza kuwa licha ya kuachia ngazi, bado ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na kuendelea kukipigania chama chake kwa namna yoyote
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Songea, James Danny Mgego, amethibitisha kupokea barua rasmi ya kujiuzulu kwa diwani huyo.
Mgego amesema kuwa katika barua hiyo, Mbano hajatoa sababu nyingine zaidi ya kutaja kuwa amejiuzulu kwa lengo la kulinda heshima ya chama na serikali.
Mgego ameongeza kuwa ndani ya CCM, mtu anapojiona amefikia ukomo wa nafasi yake anaweza kujiuzulu kwa hiari yake.
Ameeleza kuwa kwa sasa chama hakijatoa tamko rasmi kuhusu suala hilo, lakini barua ya diwani huyo tayari imepelekwa kwa ngazi za juu za chama kwa hatua zaidi.
Hadi sasa, hakuna maelezo zaidi kutoka kwa uongozi wa CCM kuhusu hatua itakayofuata baada ya kujiuzulu kwa Mbano.
Wananchi wa Kata ya Mshangano wanasubiri maamuzi ya chama kuhusu nafasi hiyo na hatma ya uongozi wa kata yao.
No comments:
Post a Comment