ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 12, 2025

SERIKALI YAENDELEA KUCHOCHEA MABADILIKO YA KIDIGITI KUKUZA UHIFADHI NA UTALII


Na: Happiness Sam- Same


Katika jitihada za kukuza sekta ya utalii na kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano katika maeneo ya Hifadhi za Taifa, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa watalii wanapata huduma bora za mawasiliano wanapokuwa hifadhini, sambamba na kuwezesha shughuli za uhifadhi kufanyika kwa ufanisi zaidi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Hayo yamesemwa jana Aprili 11, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Jerry Silaa wakati wa ziara yake katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyopo mkoani Kilimanjaro kukagua na kuhakikisha upatikanaji wa mitandao ya simu katika maeneo ya hifadhi hiyo na vijiji jirani.

Waziri Silaa alisema kuwa “ jumla ya Minara 38 itajengwa katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo Jumla ya Minara 6 itajengwa katika wilaya ya  Mwanga  kupitia mradi wa Tanzania ya Kidigitali, pia kupitia timu  ya wataalamu waliokuja kufanya utafiti tayari utambuzi wa eneo la kuweka Mnara ambao utatumika kwa lango la Ndea la kuingilia Hifadhi ya Taifa Mkomazi pamoja na maeneo mengine ya vijiji na kata za jirani umeshafanyika”.  

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Emanuel Moirana ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi aliongeza kuwa upatikanaji wa mawasiliano ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi utasaidia sana katika shughuli za utalii kwani watalii wataweza kuwasiliana kirahisi na kushiriki katika usambazaji wa taarifa kuhusu hifadhi pamoja na kurahisisha mawasiliano wakati wa shughuli za doria ndani ya hifadhi.

“Mawasiliano ni jambo muhimu kwa wageni wetu, kunapokuwa na mtandao mzuri hifadhini watalii wataweza kusambaza taarifa duniani kuhusu uzuri wa Mkomazi na pia kufanya shughuli nyingine muhimu wakati wa safari zao za utalii, pia kama hifadhi itasaidia katika utekelezaji na uendeshaji wa shughuli za doria,” alisema Kamishna Moirana.




Naye, Diwani Kata ya Toroha Palesio Nalio alisema kuwa upatikanaji wa mawasiliano katika hifadhi hiyo na vijiji jirani utasaidia katika kutatua changamoto za migongano kati ya wanyamapori na  binadamu kwani utarahisisha utolewaji wa taarifa pindi wananchi wanapoingiliwa na wanyama katika maeneo yao hali itakayopelekea upatikanaji wa msaada kwa haraka.

Ziara ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi ilikuwa na lengo la kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ambayo alitoa tarehe 25 Machi, 2025 wakati wa ufunguzi wa lango la Ndea na kusisitiza umuhimu wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu katika maeneo ya hifadhi hiyo.

Aidha Waziri Silaa katika ziara yake aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na uongozi wa Wilaya ya Mwanga wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mwanahamisi Mukunda.







No comments: