ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 5, 2026

MAKAMU WA RAIS ASISITIZA NAFASI YA TFS KATIKA KUFANIKISHA KAMPENI ZA UPANDAJI MITI



Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameuagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha unaandaa miche ya miti ya kutosha ili kuimarisha utekelezaji wa kampeni za upandaji miti na juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini.

Dkt. Nchimbi alitoa agizo hilo Juni 5, 2026, wakati akihitimisha kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema upatikanaji wa miche ya miti kwa wingi ni moja ya nguzo muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuongeza uoto wa asili, kulinda vyanzo vya maji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Sambamba na hilo, Makamu wa Rais amezielekeza Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na TFS kuimarisha usimamizi wa maeneo yanayopandwa miti ili kuzuia uharibifu na kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa hadi ikue.

“Ni muhimu kuhakikisha juhudi za upandaji miti haziishii kwenye kupanda pekee, bali zinahusisha pia ulinzi na matunzo ya miti hiyo ili iweze kukua na kutoa mchango unaotarajiwa katika uhifadhi wa mazingira,” alisema Dkt. Nchimbi.

Katika hatua nyingine, ameiagiza Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kubainisha na kusajili misitu inayofaa kuingizwa katika miradi ya biashara ya kaboni kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi kupitia biashara ya kaboni.

Dkt. Nchimbi alibainisha kuwa biashara ya kaboni ni moja ya maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuleta manufaa kwa jamii zinazoshiriki katika uhifadhi wa misitu huku ikichangia utekelezaji wa malengo ya Taifa ya maendeleo endelevu.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu yamewakutanisha viongozi wa Serikali, taasisi za umma na binafsi, wadau wa mazingira pamoja na wananchi kwa lengo la kuhamasisha usimamizi endelevu wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali za asili.

Katika maadhimisho hayo, TFS ilikuwa miongoni mwa taasisi zilizoshiriki kikamilifu kwa kuonesha mafanikio ya shughuli zake za uhifadhi wa misitu, urejeshaji wa mazingira, uzalishaji wa miche ya miti na utekelezaji wa programu mbalimbali za kukuza uchumi wa kijani nchini.








No comments: