ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 5, 2026

UTALII WA MISITU WA TANZANIA WAPATA JUKWAA KOREA KUSINI



Na Mwandishi Wetu, Seoul


Fursa za utalii wa misitu na uwekezaji katika miundombinu ya utalii ndani ya misitu ya hifadhi inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zimetangazwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Seoul International Travel Fair (SITF) 2026 yanayoendelea jijini Seoul, Korea Kusini.

Ushiriki huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) za kupanua masoko ya utalii katika eneo la Mashariki ya Mbali na bara la Asia, ambalo linaendelea kuwa miongoni mwa masoko yenye ukuaji mkubwa wa watalii duniani.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mhifadhi Someni Mteleka wa TFS alisema ushiriki wa Tanzania unatoa fursa ya kutangaza vivutio vya utalii wa misitu vilivyopo nchini pamoja na kujifunza mahitaji na matarajio ya watalii wa kimataifa.

Alisema idadi kubwa ya washiriki wa maonesho hayo wameonesha kuvutiwa na utalii wa mazingira asilia na kueleza nia ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya misitu nchini.

“Tumeshuhudia watu wengi wakivutiwa na utalii wa mazingira asilia na kuonesha hamu ya kutembelea maeneo mbalimbali ya misitu nchini Tanzania, ikiwemo Mlima Rungwe, Maporomoko ya Kalambo, Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Amani, Milima ya Magamba, Msitu wa Chome na Mlima Hanang. Fursa hii pia inatuwezesha kujifunza matarajio yao ili tuendelee kuboresha huduma na miundombinu ya utalii ikolojia,” alisema.



Kwa mujibu wa Mteleka, Korea Kusini ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa kuendeleza utalii wa mazingira asilia unaojumuisha misitu, milima, maziwa, mito, mabwawa na maporomoko ya maji, hali inayofanana kwa kiasi kikubwa na utajiri wa vivutio vilivyopo Tanzania.

Alisema uzoefu unaopatikana kupitia maonesho hayo utaisaidia Tanzania kuimarisha mipango ya kuendeleza utalii wa misitu kama zao jipya la utalii lenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na ajira.

“Tutatumia uzoefu huu kujenga uwezo wetu katika kuendeleza miundombinu na huduma zinazowezesha utalii wa misitu kukua na kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi. Hii itasaidia kufanikisha azma ya Serikali ya kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030 sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema.

Korea Kusini imeendelea kuwa mfano wa mafanikio katika maendeleo ya utalii wa mazingira asilia, jambo linalofungua fursa kwa Tanzania kujifunza mbinu bora za usimamizi wa vivutio, huduma za wageni na uwekezaji katika miundombinu ya utalii wa ikolojia.

Maonesho ya SITF 2026 huwakutanisha wadau wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani, wakiwemo wawekezaji, waendeshaji wa biashara za utalii, wanunuzi na wauzaji wa huduma za utalii, kwa lengo la kukuza ushirikiano na biashara katika sekta hiyo.




No comments: