Tuesday, February 9, 2010

Chokochoko za mseto zaanza Z'bar

VYAMA 16 vya upinzani visiwani hapa vimekataa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoshirikisha vyama vya CCM na CUF kwa madai kuwa havitaondoa mpasuko wa kisiasa.

Msimamo huo umetolewa jana visiwani hapa na mwenyekiti wa umoja wa vyama 16 vya siasa Zanzibar, Juma Ali Khatib, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Alibainisha kuwa umoja huo umeshangazwa na uamuzi wa CCM na CUF kuamua muundo wa serikali ya mseto bila kuvishirikisha vyama vingine ambavyo navyo ni wadau muhimu wa siasa za visiwa hivyo.

Alisema kamwe mpasuko wa kisiasa katika visiwa vya Zanzibar hauwezi kutatuliwa ikiwa vyama fulani vinatengwa au kubaguliwa kwa aina yoyote ile.

“Hatukubaliani na hiki kinachotaka kufanywa na CCM na CUF, kwa nini hawatushirikishi na sisi?” alihoji Khatib ambaye ni Katibu Mkuu wa TADEA.

Alisema kwamba vyama hivyo vimepokea kwa mshtuko mkubwa kuhusiana na muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa kwa sababu wamevitenga vyama vingine vya siasa Zanzibar.

Aliongeza kuwa umoja huo umefanya mkutano wa kujadili mustakabali wa siasa za Zanzibar baada ya makubaliano ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, na Rais Aman Abeid Karume.

Alisema waliamua kufanya mkutano huo kwa kuwa suala liloafikiwa na Seif na Karume lina masilahi kwa taifa hilo hivyo haitokuwa busara kama litapita hivihivi bila kujadiliwa kwa kina.

Alisema kimsingi wanakubaliana na hoja ya uundaji wa serikali ya mseto lakini hawakubaliani na CCM na CUF kujitwisha jukumu hilo peke yao pasi na kuyashirikisha makundi mbalimbali ya kijamii. Alibainisha kuwa tabia ya CCM na CUF kuvitenga vyama vingine katika mazungumzo ya kutafuta utatuzi wa mpasuko wa kisiasa katika visiwa hivyo itaathiri siasa za nchi hiyo kwa siku za usoni.

Khatib aliongeza kuwa kama CUF na CCM havitakaa chini na kuvijumuisha vyama vingeni suala hilo litafikishwa mahakamani.

“Kama hoja zetu hazitosikilizwa na kufanyiwa kazi hatutasita kwenda mahakamani kudai haki yetu!” alisema Khatib.

Alisema kwamba makovu ya kisiasa yaliyojitokeza tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hayakuathiri wanachama wa CCM na CUF pekee yao hasa kwa kuzingantia vyama hivyo vimekuwa vikipata kura zaidi ya 10,000.

Alibainisha kuwa wameunda kamati itakayosimamia maazimio sita yaliyopitishwa na umoja huo wa vyama kabla ya utekelezaji wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar.

Aliyataja maazimio hayo kuwa ni kufuatilia suala la hoja ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kama ilivyofikiwa na Baraza la Wawakilishi; na kuwasiliana na ofisi ya rais kwa ajili ya kukutana viongozi wa vyama vya siasa na Rais wa Zanzibar.

Mengine ni kuzungumzia hali ya kisiasa baina ya Rais wa Zanzibar na vyama vya siasa kuhakikisha vinashirikishwa katika serikali ya umoja wa kitaifa zikiwemo taasisi za dini na walemavu.

Mambo mengine yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kuuelimisha umma juu ya uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa, tafasiri ya ‘Umoja wa Kitaifa’ na kuunda kamati ya watu wanne itakayosimamia mpango mzima kabla ya kufikiwa kwa Serikali ya Mseto Zanzibar.

Umoja huo wa vyama 16 unaotaka ujumuishwe kwenye serikali ya mseto ni DP, TADEA, CHADEMA, NCCR Mageuzi, AFP, TLP, SAU, UDP, UPDP, CHAUSTA, UMD, JAHAZI Asila, P.T.P Maendeleo, DEMOCRASIA Makini, NRA na NLD

No comments: