ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 29, 2010

Kwanini Mwamwindi Alimpiga Risasi Dr Kleruu? Nimefanya Mahojiano Na Mtoto Wa Mwamwindi...



Jana Jumamosi jioni nilikuwa na mazungumzo marefu na Bw. Amani Mwamwindi. Mstahiki Meya wa Iringa aliyemaliza muda wake. Huyu ni mwana wa marehemu Saidi Mwamwindi ambaye simulizi juu ya kilichotokea kule Isimani mwaka 1971 tumeifuatilia.

Bw. Amani Mwamwindi alikubali kufanya mazungumzo nami hiyo jana nyumbani kwake Mlandege hapa Iringa. Ni simulizi ya kusikitisha, kusisimua na yenye kutoa mafunzo. Inahusu pia maarifa ya uongozi na dhana nzima ya utawala bora. Naandika haya saa saba za usiku Jumapili. Ngoje nikapumzike. Baadae Jumapili ya leo nitaanza kuwasilimua niliyosimuliwa.

Kumekucha. Jumapili saa kumi na mbili asubuhi. Naanza kusimulia nilichosimuliwa;

Nimefika Nyumbani kwa Amani Mwamwindi. Ni majira ya saa kumi na nusu jioni. Ni nyumba ya kawaida sana katikati ya eneo wanaloishi watu wengi, karibu kabisa na soko. Ni kata ya Mlandege.

Nagonga mlango mkuu. Anayenifungulia ni Amani Mwamwindi.
” Karibu Bwana Mjengwa”. Tunafahamiana, tumewahi kukutana kabla. Miguuni hana viatu, amevaa soksi nyeusi.


Ananikaribisha kiti sebuleni. Anaagiza nilitewe kinywani. Naye anakaa kitini. Mazungumzo ya ana kwa ana. Kichwani najiuliza; unaanzaje mahojiano na mtu aliyefiwa baba yake kwa kunyongwa miaka arobaini iliyopita?

”Bw. Mwamwindi, pole sana kwa tukio lile la mwaka 1971. Mimi nimelifuatilia kiasi. Kuna simulizi nyingi mitaani. Nimeanzisha mjadala bloguni. Vijana wengi wanaonyesha kuwa na kiu ya kutaka kujua ukweli hasa wa tukio lile. Kwa vile uko hai, nikaona nikutafute tusikie kutoka kwako.”

Mwamwindi ananiangalia usoni.
” Alaa!” Anatamka. Kisha kinafuata kimya.

Nakumbuka, kuwa nimetoa maelezo ya utangulizi, sijauliza swali.
” Je, ni kweli kuwa Dr Kleruu alikwenda Isimani kwa marehemu mzee Mwamwindi kuhimiza suala la kilimo ndipo akakutana na kifo chake? ” Namwuliza kwa staili ya kurusha mshale bila kulenga hasa ninachotaka kupiga. Namjengea mazingira ya kuogelea katika kile anachokijiua. Na swali hili kwake analiona zuri sana.

” Swali zuri, umeuliza kama Kleruu alikwenda kuhimiza kilimo. Hapo ndipo lilipoanzia tatizo.”

Nakumbuka swali muhimu kabla hajaendelea.

” Mzee Mwamwindi, hivi ulikuwa na umri gani siku hiyo ya tukio?”
” Nilikuwa na miaka 21, na marehemu mzee alikuwa na miaka 42.”

Nauliza tena.
” Tunasoma kuwa ilikuwa siku ya Krismasi. Je, ilikuwa ni Jumapili au siku gani? Na wewe ulikuwapo nyumbani kwa mzee?”
” Ni kweli ilikuwa siku ya Krismasi, Desemba 25, 1971. Ni siku ya Jumamosi” Anajibu Mwamwindi.

” Turudi kwenye tatizo lilipoanzia” Namwomba Mzee Amani Mwamwindi.

” Kulikuwa na tofauti ya kimtazamo. Na ugomvi ulianzia siku ya Alhamisi, Desemba 23 kwenye ukumbi wa welfare pale Mshindo. Kleruu aliwakusasanya wakulima wakubwa wa Isimani. Nataka ujue kuwa Isimani ilikuwa na wakulima wakubwa sana na mmoja wao ni marehemu baba yangu. Mle ukumbini kulitokea malumbano makali sana baina ya wazee wale na mkuu wa mkoa Kleruu.

Wazee hakukubaliana na Kleruu kuwaita pale kuzungumzia kilimo cha eka mbili au tatu wakati wao kila mmoja ukubwa wa shamba ulianzia eka mia mbili. Na tayari walikuwa na ushirika wao. Mimi nikiwa na miaka 21 nilikuwa karani wa chama cha ushirika.

Siku ile Mzee alitoka kwenye mkutano ule na kuja nyumbani kwangu hapa tulipo, Mlandege. Akanieleza juu ya mkutano ule na jinsi walivyokosana kimazungumzo na Kleruu. Akaniambia, kuwa mle mkutanoni alimwambia Kleruu ni vema akawasaidia wale ambao hawajaanza hata kutembea kuliko kuhangaika na watu wenye uwezo wa kutembea na kukimbia. Na baba yangu hakwenda shule.


Kwenye Umoja wao wa wakulima wa Isimani, baba na wenzake walijipanga vema. Walishaanza kuzungumzia haa uwezekano wa kumlipa mwanasheria, hata kama ni wa kutoka Uingereza, aje kuwatetea katika uovu ule wanaotaka kufanyiwa. Hawakukubaliana na utekelezaji wa sera za Ujamaa kwa staili ile aliyotaka Kleruu. Kuingia kwenye ushirika na wengine wakati wao walishaanza zamani. Fikiri, wao walifyeka mashamba yao tangu miaka ya hamsini. Hoja yao ni kuwa mapori yalikuwa hayajaisha kwa wengine kwenda kufyeka na kulima. ” Anazungumza Mzee Mwamwindi. Anaonekana kuwa na mengi sana, na hamu ya kusimulia zaidi. Nabaini pia, kuwa kwake yeye mkuu yule wa mkoa ni Kleruu na hamtaji kama ' Dr Kleruu'. Namwacha aendelee.

” Sasa baada ya ile alhamisi, mzee akashinda Ijumaa. Jumamosi ikawa siku ya Krismasi. Kwa vile wafanyakazi wake wa shambani walikuwa mapumziko ya krismasi. Na yeye ni mwislamu, na alikuwa mchapa kazi kweli, basi, alikwenda shamba lake la jirani akiwa na mdogo wangu, sasa ni marehemu, anaitwa Mohamed. Wakawa wanalima kwa trekta.

Siku hiyo Kleruu, pamoja na kuwa ni Mkristo, aliamua kutokula Krismasi. Alivaa kofia yake ya pama. Inaaminika alibeba pistol yake pia. Kleruu akaendesha mwenyewe gari lake la mkuu wa mkoa aina ya Peugeot Injection, rangi ya bluu. Katika orodha yake, Kleruu alikuwa na watu watatu wa kuwashughulikia miongoni mwa wakulima wale wakubwa wa Isimani. Target nambari moja alikuwa Bw. Rashid Juma wa Nyangólo. Nambari mbili ni marehemu baba. Namba tatu simjui.

Kleruu alipofika Nyang’olo hakumkuta mkulima Rashid Juma. Siku hiyo ya Krismasi Rashidi Juma alipata habari, kuwa kuna ng’ombe wake walipotelea milimani. Alikwenda huko milimani kusaka ng’ombe wake. Hivyo, Kleruu akafunga safari kurudi kwa target namba mbili, baba yangu Mzee Mwamwindi. Ni njia hiyo hiyo, Nyang´'olo iko mbele ya ilipokuwa ngome ya mzee.” Anasema Mwamwindi akionekana kuzama katika simulizi inayomgusa. Nami namsikiliza kwa makini.

”Basi, Kleruu akafika kwa Mzee. Baba akiwa shambani akaliona gari la Kleruu limesimama nje ya mji wake. Kisha akamwona Kleruu akitembea kumfuata shambani. Baba alihisi tu, kuwa Kleruu amekuja na shari.

Kleruu akamwuliza Mzee kwa ukali, ” Mbona mnafanya kazi leo siku ya Krismasi?”. Baba akamwomba Kleruu waende wakuzungumze nyumbani. Akamwambia mdogo wangu Mohammed aendelee kulima. Mzee akatangulia mbele, nyuma anamfuatia Kleruu. Kabla ya kufika kwenye nyumba yake wakayapita makaburi. Kleruu akamtamkia baba mzee Mwamwindi; ” Hapa ndipo unapozika mirija yako?” Alitamka hivyo huku akimtomasa tomasa mzee na kifimbo alichoshika mkononi.

Jambo hilo lilizidi kumkasirisha marehemu mzee. Akafika nyumbani kwake. Mlangoni alisimama mke wake mdogo. Inaonekana mzee alishafanya uamuzi. Jana yake alikwenda kuwinda. Hakupata mnyama. Bunduki yake moja aia ya riffle kati ya bunduki zake mbili ilikuwa bado ina risasi. Akamwambia mke wake mdogo huku Kleruu akiwa anasikia;
” Kanichulie bunduki yangu”…… ( Simulizi hii inaendelea baadae. Jamani, Jumapili leo, nipumzike kidogo!)


Kleruu akamwuliza Mzee kwa ukali, ” Mbona mnafanya kazi leo siku ya Krismasi?”. Baba akamwomba Kleruu waende wakuzungumze nyumbani. Akamwambia mdogo wangu Mohammed aendelee kulima. Mzee akatangulia mbele, nyuma anamfuatia Kleruu. Kabla ya kufika kwenye nyumba yake wakayapita makaburi. Kleruu akamtamkia baba mzee Mwamwindi; ” Hapa ndipo unapozika mirija yako?” Alitamka hivyo huku akimtomasa tomasa mzee na kifimbo alichoshika mkononi.

Jambo hilo lilizidi kumkasirisha marehemu mzee. Akafika nyumbani kwake. Mlangoni alisimama mke wake mdogo. Inaonekana mzee alishafanya uamuzi. Jana yake alikwenda kuwinda. Hakupata mnyama. Bunduki yake moja aia ya riffle kati ya bunduki zake mbili ilikuwa bado ina risasi. Akamwambia mke wake mdogo huku Kleruu akiwa anasikia;
” Kanichukulie bunduki yangu”…… Endelea…


“ Je, aliposikia hayo Dr Kleruu alifanyaje?”

” Nadhani alipigwa na butwaa. Hakuamini kama baba angefikia hatua hiyo”

”Na ilikuwaje basi Mwamwindi alipoletewa bunduki?”

” Ilienda haraka, Mzee Mwamwindi akainua bunduki yake. Tayari ilikuwa loaded na risasa tangu jana yake alipotoka kuwinda. Kleruu aliinua mikono yote miwili kama mtu anayesalimu amri. Mwamwindi akampiga risasi ya kwapani. Kleruu akabaki hai. Akapiga risasi nyingine. Ikamwua pale pale.” Anasimulia Mzee Amani Mwamwindi.

Kinafuatia kimya. Anainama, namwona usoni, kuwa huzuni imemjia. Bila shaka, ni kitendo kile cha baba yake kumpiga risasi na kumwua Dr Kleruu ndicho kilichoashiria mwanzo wa ukurasa mgumu katika familia ya Mwamwindi , Isimani na pengine Iringa kwa ujumla.

Nafikiria kumwuliza swali lifuatalo; Risasi ya pili ya Mzee Mwamwindi ilimpiga Dr Kleruu katika sehemu gani ya mwili? Nasitisha swali hilo. Litasubiri mara nyingine. Mzee Amani Mwamwindi anaendelea kunisimulia;

” Mdogo wangu Mohammed akiwa shambani alisikia mlio wa bunduki. Alidhani kuwa baba amepigwa risasi. Alikimbia kurudi nyumbani. Na pale ilipowekwa kumbukumbu ya Kleruu nyuma yake ndio ilipokuwa nyumba ya mzee. Hivyo, pale ulipowekwa mnara ni mbele ya nyumba. Kwa sasa nyumba hiyo haipo.

Alipofika nyumbani, Mohammed akamkuta baba amesimama, na Kleruu amelala chini, amekufa. Mzee alichukua kofia ya pama ya Kleruu, akaivaa. Akaingiza mkono mifukoni mwa Kleruu, akachukua funguo za gari la Kleruu. Mzee alimwambia mdogo wangu amsaidie kumwinua Dr Kleruu. Mzee alimshika miguuni na mdogo wangu Mohammed alimshika kwenye mikono. Wakamwingiza kwenye buti la gari.

Baba akaendesha mwenyewe gari lile la Mkuu wa Mkoa Kleruu, Peogeot Injection, rangi ya bluu likiwa linapepea bendera ya taifa. Aliendesha kuelekea mjini Iringa. Njiani kuna walioshangaa kumwona Mwamwindi akiendesha gari la Mkuu wa Mkoa huku akiwa kichwani amevalia pama la Kleruu.

Mzee alipoingia mjini Iringa breki ya kwanza ilikuwa hapa tulipo, nyumbani kwangu Mlandege. Kama nilivyosema, wakati huo nilikuwa kijana wa miaka 21. Nilishakuwa na mji wangu, nilijenga kibanda changu hapa tulipo. Nilifanya kazi kama karani wa Ushirika. Siku ile ya tukio nami nilikwenda kwenye shamba langu Ifunda.
Basi, Mzee alipofika hapa nyumbani akaambiwa kuwa nimekwenda shamba Ifunda. Alisikitika sana.” Anasema Mzee Mwamwindi huku naye bado akionyesha huzuni machoni. Miaka 40 baada ya tukio.


Alipotoka hapa alipita nyumbani kwake pale Mshindo, na baadae akasimama kwa binamu yake. Ile nyumba ya njano nyuma ya benki ya CRDB, si unaijua?” Ananiuliza.

” Ndiyo” Namjibu.
” Pale alikuwa anakaa binamu yake na baba. Basi, alipofika pale akakutana n abinamu yake. Binamu yake yule alishangaa kumwona mzee akiwa na damu kwenye nguo zake. Akashangaa pia kumwona akiwa na gari la Kleruu lenye bendera ya taifa ikipepea. Akamwuliza nini kimetokea? Mzee hakuweza kuongea akaeleweka. Alitamka; ” Nimeenda kwa Amani ( Mimi) nimeambiwa kaenda shambani kwake Ifunda”. Alionekana kuchanganyikiwa.

Akaingia kwenye gari. Akaendesha moja kwa moja hadi Kituo cha polisi. Akamkuta polisi kijana. Akashuka, akamwambia; ” Njoo chukua mzigo wako”. Akaweka chini pia kofia ya pama ya Kleruu.

Polisi alipofungua buti ya gari akashangaa kuona mzigo wenyewe ni mwili wa Mkuu wa Mkoa, Dr Kleruu. Mzee akawa amejisalimisha.

Niliporudi nyumbani kutoka Ifunda nikazikuta habari hizo mbaya. Nikaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Mzee pale Mshindo. Nikawakuta akina mama wanalia. Ilikuwa ni kilio. Hiyo bado ilikuwa ni Jumamosi, siku ya Krismasi. Nikauliza; kuna aliyekwenda kumwona baba pale polisi? Jibu likawa hapana. Nikaenda moja kwa moja polisi ili nikamwone baba na nimsikie kauli yake.

Nilipofika polisi nikaanza kujieleza kwa askari polisi kuomba ruhusa ya kuongea na Mzee. Wakati nikifanya hivyo mzee nae alisikia sauti yangu. Akatamka; ” Mwanangu huyo, mruhusu niongee nae”. Nikaongea na Mzee.

( Jamani nayaandika haya alfajiri sana. Ningependa niendelee, lakini nisitishe hapa kwa asubuhi hii. Nitaendelea kusimulia usiku wa leo au kesho alfajiri, maana Jumatatu imeingia hapa Iringa. Ngoja nikawachemshie uji wana wangu kabla hawajaenda shule!)
                   Chanzo http://mjengwa.blogspot.com/

No comments: