ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 29, 2010

Masha ang'oa vitasa ofisi ya Mbunge Mwanza

Mr Masha
Frederick Katulanda, Mwanza
ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, amehamisha vifaa mbalimbali vya ofisi ya Bunge Jimbo la Nyamagana, kwa madai kuwa alivinunua mwenyewe kipindi uongozi wake. Akizungumza na Mwananchi jana, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, alisema baada ya kutoka Bungeni alikwenda kuingia katika ofisi hiyo, lakini baada ya kukabidhiwa alikuta vitasa vya mlango, simu ya mezani picha ya Rais na samani za kukalia vikiwa zimechukuliwa.
 
Kwa mujibu wa Wanje, baada ya kufuatilia aliambiwa kuwa vifaa hivyo viliondolewa na Masha kwa madai kwamba, alivinunua kwa fedha zake mwenyewe.

“Nimefuatilia kwa DAS (Katibu Tawala wa Wilaya) nikaambiwa amechukua Masha, nikafuatilia kwa Katibu Tawala wa Mkoa yeye alijibu kuwa naye alifuatilia suala hilo kupitia kwa Das na kupewaa majibu kama yangu, sasa sijajua ni kwa nini, ninavyojua ofisi haipaswi kukosa samani kwa vile kuna fedha za kununulia vitu hivyo,” alisema.

Kwa Upande wake, Masha alikiri kuondoka na vitu hivyo na kwamba, asingeweza kuacha vifaa vyake binafsi katika ofisi hiyo.

Masha alisema vifaa alivyoondoka navyo ni vile tu ambavyo ni mali yake. 

“Wakati naingia hapa nilikuta ofisi ikiwa na kiti kimoja na meza tu, vifaa vingine niliweka vyangu, kama kompyuta na meza zake, simu na samani nyingine kulingana na mahitaji yangu,” alisema Masha.
Alisema Wenje anapaswa kuwasiliana na ofisi ya mkuu wa wilaya, ili kupewa vifaa vya ofisi hiyo ambavyo yeye aliviondoa alikuwa havitumii kwa vile wao wanajua vilipo.

“Jamani vifaa vya ofisi anapaswa kuuliza ofisi ya mkuu wa wilaya, sasa kama anataka nimwachia na vyangu binafsi, mie nimetoa vyangu…hivyo vya ofisi vipo, nadhani amefika na kukutana na kiti kimoja na meza vile vingine vilivyokuwemo pia vilikuwa mali ya ofisi,” alieleza Masha.

Hata hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza (RAS), Doroth Mwanyika, hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo kutokana na kuwa nje ya ofisi, lakini ofisa mmoja wa ofisi yake alithibitisha kuwepo kwa malalamiko ya Wenje na kwamba, yalikuwa yakishughulikiwa.


                                            CHANZO:MWANANCHI

No comments: