Advertisements

Wednesday, November 17, 2010

Mapenzi humaanisha nini hasa?


NI imani yangu kwamba mtakuwa wazima wa afya njema na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku kama kawaida. Kwa upande wangu mimi ni mzima wa afya njema kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Karibuni tena tujifunze mambo mbalimbali ya kudumisha uhusiano na wapenzi wetu.

Naendelea kuwakumbusha rafiki zangu kwamba, kitabu changu cha Joseph Shaluwa…Let’s Talk About Love kipo katika hatua za mwisho kabisa kabla ya kuingia mitaani. Endelea kuvuta subira utakisoma hivi karibuni. Kikubwa zaidi utasoma mada mbalimbali za mapenzi na meseji nzuri kwa ajili ya kumtumia mpenzi wako.

Yes! Leo tunaangalia, maana hasa ya mapenzi! Hivi unafikiri mapenzi ni nini? Kila mmoja anaweza kuwa na maana yake, lakini kimsingi mapenzi hayana maana ya moja kwa moja! Kwa ujumla mapenzi ni hisia zinazotoka moyoni mwa mmoja kwenda kwa mwingine, zikimaanisha upendo wa dhati. Pendo hukamilika ikiwa wawili hao kwa wakati mmoja wakahisi hisia hizo, ingawa wakati mwingine mmoja ndiyo huwa wa kwanza kuanza kuhisi hisia hizo.

Wakati mwingine inawezekana mkajikuta mmependana tangu siku ya kwanza tu mlipokutana, lakini wengine huchukua muda mrefu kidogo kabla hisia hizo hazijachukua nafasi. Lakini wengine hufikiria mapenzi ni ngono au ngono ni sehemu ya mapenzi. 

Rafiki zangu ambao huamini kwa asilimia mia moja kwamba mapenzi ni ngono, huharibu kabisa maana ya mapenzi. Je, wewe unafikiri nini? Kuna ukweli wowote katika hilo? Hebu twende pamoja katika mada hii ambayo sina shaka itakuacha na mwanga mpya katika maisha yako ya kimapenzi.

Je, mapenzi ni ngono? Kama si ngono, kwanini wapenzi hukutana na kufanya ngono? Kwanini wanandoa hufanya tendo hilo na kupata watoto? Hebu sasa anza kufuatilia vipengele vifuatavyo hapo chini…

NGONO NI LAZIMA?
Hapana! Mapenzi ni kitu kingine na ngono ni kitu kingine, ingawa baadhi ya watu hufikiria kuwa ngono ni sehemu ya uhusiano, jambo ambalo sio la kweli hata kidogo. Kimsingi ngono huja baada ya tamaa kuingia kati ya watu wawili wanaopendana!

Hata hivyo kuna uwezekano mkubwa, ukawa na tamaa ya kufanya ngono na mtu hata kama huna mapenzi naye katika moyo wako. Kimsingi suala la kufanya ngono sio kithibitisho cha kuonyesha mapenzi ya dhati. Baadhi ya walio katika uhusiano, hudanyanywa na kipengele hiki. 

Utakuta msichana anaambiwa na boyfriend wake kuwa, ili aonyeshe kuwa anampenda basi lazima akubali kufanya naye ngono, hata hivyo baada ya kumaliza kufanya ngono, kuna uwezekano mkubwa wa penzi hilo kuyeyuka! Kuwa na msimamo.

MNAWEZA KUFANYA NGONO LINI?
Kimsingi suala la kufanya mapenzi halina kanuni, hakuna muda maalum wa kuanza kufanya mapenzi na mpenzi wako. Ngono ni hisia tu, tena basi huwa bora zaidi kama hisia hizo zikaja kwa wakati mmoja kati yako na huyo unayempenda!

Wataalam wa Saikolojia ya Mapenzi, wanashauri wapenzi wasishiriki tendo hilo mpaka pale watapokuwa wamefahamiana kiasi cha kutosha, hasa kupima afya kwa kuwa magonjwa ya zinaa na hasa Ukimwi yamezigaa kila kona ya dunia. Pamoja na hayo, suala la ngono halikwepeki ikiwa mtaruhusu kukutana sehemu tulivu mkiwa wawili. Jambo la msingi ni kutulia na kujipanga, msifanye ngono kama sehemu ya mapenzi.

Tambua kuwa ngono ni kitu kingine na mapenzi ni kitu kingine, hata kama mtakuwa mmeamua kushiriki katika kitendo hicho, mfahamu kuwa mnasterehesha nafsi zenu na sio 
kuonyeshana mapenzi ya dhati. 

NI KWELI MAPENZI YA NGONO 
HAYADUMU?
Tafiti mbalimbali za wataalam wa mambo ya uhusiano, zinaonesha kuwa wengi walio katika uhusiano huwa hawawezi kuvumilia kuendelea kuwepo katika uhusiano bila kufanya mapenzi. Hata hivyo tafiti hizo za uhakika zinaeleza kwamba baada ya wapenzi kufanya ngono, ile hamu ya kuendelea kuwa na uhusinao hupungua!

Hiyo husababishwa na dharau za kimaumbile, na kujihakikishia kuwa hakuna kitu asichokijua kwa ‘patna’ wake. Wengi hulia baada ya kujikuta wakiingia katika mkumbo huu. Hebu jiulize, kama anakupenda, kwanini anang’ang’ania kufanya mapenzi na wewe haraka?
Wewe ni wake na huenda mna ndoto za kuishi siku moja pamoja, kwanini asivumilie mpaka wakati huo? Akitaka anaweza kuvumulia na kufaidi mambo hayo mkiwa katika ndoa halali yenye baraka zote.

NINI BADALA YA NGONO?
Yapo mambo mengi sana ya kufanya badala ya ngono, huna sababu ya kutoa kipaumbele kwa ngono wakati kuna vitu vingine vingi unavyoweza kufanya na kuyafanya mapenzi yenu yakaendelea kudumu kila siku.

Mnaweza kukaa sehemu nzuri yenye utulivu kwa ajili kupanga maisha yenu ya baadaye. Epukeni sehemu zenye vificho, ambazo zinaweza kuwapa vishawishi vya kufanya mapenzi. Lakini pia. Kutoka pamoja kwa ajili ya chakula usiku (dinner), chakula cha mchana (lunch) na mtoko wa mwisho wa wiki (outing). Vijizawadi vidogo vidogo, kama matunda, maua, nguo na vingine vya kupendeza vinaweza kuyadumisha mapenzi yenu kuliko kung’ang’ania ngono. Upo hapo? Naweka nukta.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com

No comments: