ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 6, 2010

Ghost ajiuzulu Harambee Stars

MuleeJacob 'Ghost' Mulee amejiuzulu kuifundisha timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars, baada ya timu hiyo kuchapwa 2-0 na Uganda Cranes jijini Dar es Salaam katika michuano ya Cecafa.

Huo ni mchezo wa tatu kwa Stars kupoteza mfululizo, na wanarejea nyumbani bila hata pointi moja.

"Nabeba lawama zote kwa kiwango kibovu tulichoonesha hapa, na naamini sistahili kuendelea kuifundisha timu hii," amesema Mulee baada ya mchezo.
Hii ni mara ya tatu kwa Mulee kuifundisha timu hiyo ya tafa ya Kenya.

Timu ya ushindi

"Nilikuja hapa na wachezaji wazuri kutoka ligi ya Kenya, na kama siwezi kushinda hata mchezo mmoja, basi njia pekee ni kuacha kazi," amesema.
Mulee, ambaye aliipeleka timu hiyo katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004 nchini Tunisia, akiifundisha kwa mara ya kwanza, aliteuliwa kuifundisha tena miezi kadhaa iliyopita, na ameshindwa kuibadili na kuwa timu ya ushindi.
Wachezaji waligoma siku ya Ijumaa, wakisema hawajalipwa na chama cha soka cha Kenya.

Nafasi

Harambee Stars walipata nafasi kadhaa za kufunga ikiwemo ya wazi ambapo shuti la Goerge Odhiambo lilizuiwa na kipa wa Uganda Robert Odongkara.
Uganda ilipata nafasi yake katika dakika ya 83, na Okwi Emmanuel hakufanya makosa.
Dakika saba baadaye, kipa wa Stars Bonface Oluoch alimfanyia rafu Robert Ssentongo na kupewa kadi nyekundu, huku Andy Mwesigwa akipachika mkwaju wa penati. Beki Ndeto Mulinge ndiye alikaa langoni.

Nane bora

Katika mchezo mwingine, Ivory Coast imeichapa Sudan 3-0, katika mchezo wa awali, na hivyo kujihakikishia nafasi katika nane bora.
Kone Zoumana aliandika bao la kwanza katika dakika ya 36, kabla ya Kipre Tchetche kufunga mabao mawili katika dakika za 59 na 77.
Kwa matokeo haya, robo fainali Zambia itapambana na Ethiopia mapema Jumanne, kabla ya Ivory Coast kucheza na Malawi.
Uganda itacheza na Zanzibar siku ya Jumatano huku Tanzania ikipambana na Rwanda.

No comments: