ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 5, 2010

Je, Ni Kwanini Mwamwindi Alimpiga Risasi Dr Kleruu? (4)



” Ndio Mzee wangu, nisimulie habari za Marehemu Said Mwamwindi, maana nimekutana na mwanae , Amani Mwamwindi, naye kuna aliyonisimulia. Je, ulipata kukutana na marehemu Said Mwamwindi wakati wa uhai wake?”

” Aah! Said Mwamwindi, nilimfahamu sana." Ananiambia huku anacheka. Kisha anaendelea kusema;

" Unajua, tulikua nae hapa mjini. Na hata siku ile ya tukio mimi na vijana wenzangu wa wakati ule tulikuwa tunacheza bao pale Miyomboni, tulishangaa sana kumwona Said amesimamisha gari la Dr Kleruu nyumbani kwa shangazi yake na huku amevalia pama la Dr Kleruu.

Nakumbuka alitunyoshea mkono akiwa anatabasamu. Tulizungumza kwa kushangaa, tukajiuliza; jamani hivi Serikali leo imempa Said Mwamwindi gari atembelee? Yakafuata yaliyofuatia. Maggid, ninayo mengi ya kukusimulia kwa yaliyotokea katika wakati ule….” Anasema Mzee Nzowa. Endelea..

“ Ndio, nilimfahamu Said, na jina lake hasa aliitwa Said Abdalah Siulanga Mwamwindi. Nyumba ya baba yake ilikuwa pale Mshindo karibu na ukumbi wa Welfare. Baba yake aliwahi kuwa Jumbe enzi hizo za nyuma. Said alikuwa mtu wa kilimo na nakumbuka alianzia kwenye magari, alikuwa dereva kabla hajaenda kufyeka mapori ya kilimo kule Isimani.”

Je, unakumbuka wajihi wa marehemu Said Mwamwindi?

“ Ah, Yule bwana alikuwa mrefu na aliyeshiba hasa. Ukimwona utasema huyu jamaa amekaa kiutemi-utemi. Yaani, unavyoomwona mwanae, Amani Mwamwindi sasa , ndivyo kwa kiasi kikubwa alivyoonekana Said Mwamwindi. Wamefanana sana.

Na je, Dr. Kleruu, alikuwa mtu wa namna gani, wajihi wake na mengineyo?

”Alaa, Dr Kleruu, tulikuwa vijana wakati ule, na yeye alikuwa Mkuu wa Mkoa kijana hapa Iringa. Nafikiri alichukua nafasi ya Bw. Chamshama. Alikuwa mfupi kidogo. Ila bwana, alikuwa machachari sana . Nikisema ’machachari’ nadhani unanielewa.
Haraka sana tuliona dalili kuwa Dr Kleruu asingekuwa na wakati mzuri hapa Iringa.

Alianza mapema sana kuonyesha tabia za Ubwana na hata kunyanyasa aliowaongoza. Na katika hao aliowaongoza kulikuwa na watu wazima waliomzidi umri na wenye hekma na busara kumzidi yeye, ingawa hawakusoma elimu ya darasani.”

Je, unaweza kutoka mfano wa ’Ubwana’ mkubwa wa Dr Kleruu aliouonyesha wakati huo?

”Iko mifano mingi, na ukweli Dr Kleruu alisemwa vibaya katika midomo ya watu hapa Iringa. Ilifika mahala dereva akilipiga overtake gari la Dr Kleruu hapa Iringa, basi, atasimamishwa na anaweza kuzabwa vibao na Kleruu mwenyewe. Aah! Jamaa yule alikuwa mbabe bwana !” Anasema Mzee Omary Nzowa huku akicheka kwa sauti. Kisha anaendelea.

” Unajua Dr Kleruu alitokea Mtwara kabla ya kuja Iringa. Sasa kuna wakati alitamka; ” Hamnijui mimi, kawaulizeni watu wa Mtwara!” Sasa hayo si maneno ya kuwaambia watu wa Iringa, na hata mahali pengine popote.” Anasema Mzee Nzowa. Anaonyesha kuwa na hamu zaidi ya kusimulia.

” Na nikwambie kitu kimoja Maggid, muhimu katika maisha ni kuishi vema na watu. Hata kama ni kiongozi, huwezi kufanikiwa katika kazi yako kama huna mahusiano mazuri na unaowaongoza. Na hata katika maisha ya kawaida, unaweza kuingia katika misukosuko isiyo ya lazima kama huna mahusiano mazuri na wenzako katika jamii.

Nitakupa mfano hai unaonihusu mimi. Mwishoni mwa miaka ya 50 nilikamatwa nyumbani kwa kutokulipa kodi ya kichwa. Tulikuwa bado kwenye utawala wa mkoloni. Nilikuwa nadaiwa shilingi saba tu. Sikuwa nazo.

Basi, nikaambiwa na askari wa kodi tuongozane hadi ofisini kwa DC. Tena walinifunga kamba mikononi. Nilifahamu, huko kwa DC ningeishia kuchapwa bakora na hata kuwekwa ndani. Unajua Maggid enzi hizo damu ilikuwa ikichemka na sisi vijana ndio tuliokuwa tukionekana kuiunga mkono TANU. ” Ananiambia Mzee Nzowa akikumbuka enzi za ujana wake.

” Sasa basi, wakati tunakwenda kwa DC, niliwaomba sana wale askari wa kodi. Walikuwa Waafrika wenzetu. Nikawaambia, jamani ee, tafadhali tupite njia hii ya sokoni. Ni soko lile la zamani ambalo mpaka leo hii bado linatumika. Askari walikubali wakidhani nimechagua mwenyewe njia nitakayoonekana na watu na hivyo kujidhalilisha mwenyewe. Kumbe, mimi nilikuwa na maana yangu.

Tulipofika eneo la sokoni nikasikia jamaa zangu wakiuliza kwa sauti; ” Omary shida gani?”. Nikajibu kwa sauti; ” Kodi, shilingi 7!”. Basi, huwezi kuamini, hata kabla sijamaliza soko, vijana wale wa sokoni walichangishana. Shilingi saba zikapatikana. Kodi ile nikalipa na nikaachiwa huru.. Pointi yangu hapo ni umuhimu wa mahusiano mema na watu.” Mzee Nzowa anaeleza kwa kusisitiza.

Je, unafikiri ni kwanini Dr Kleruu alipata tabu sana kufanya kazi na watu wa Iringa?
” Mi nadhani Kleruu, kwa jinsi alivyokuwa, angepata tabu kufanya kazi mahali po pote pale. Tatizo ni ile hali ya kutanguliza Ubwana na kuwadharau wananchi. Hakika wakati ule Mwalimu Nyerere alipata tabu sana na namna ya ku-deal na viongozi kama akina Kleruu. Kumbuka , Tanzania kama nchi ilikuwa taifa changa sana. Hatukuwa na wasomi wengi. Nilimfahamu Nyerere, hili la Kleruu lilimsumbua sana Mwalimu.

Nikwambie Maggid, Ujamaa na Kujitegemea kama itikadi na sera za Mwalimu haukuwa tatizo. Tatizo lilikuwa kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya utekelezaji. Hawa hawakuwa wanasiasa, wakati mwingine walionekana kama Wanyapara. Mwalimu wakati ule hakujua kila kitu kuhusu watu aliowateua kumsaidia. Ni kweli Mwalimu alitia saini hukumu ya kunyongwa kwa Mwamwindi, lakini naamini hakufurahia, bali hali ya wakati ule ilimlazimisha kufanya vile.

Sisi tuliomfahamu Mwalimu tunajua kuwa hukumu ile ni moja ya maamuzi magumu yaliyomsononesha sana Mwalimu. Unajua wakati ule kuna Wakuu wa Mikoa waliojenga hoja, kuwa kama Mwamwindi kwa tendo lile asingepata adhabu ile, basi utendaji wao wa kazi mikoani ungekuwa mgumu. Ndio, hoja hizo ziliibuka. Kwa kiongozi wa nchi ni mtihani. Siyasemi haya kumtetea Mwalimu bali ni kutambua ukweli kuwa Mwalimu alikuwa ni binadamu kama wewe na mimi.”

Unasema ulimfahamu Nyerere na kwamba unaamini kwa wakati ule tatizo kwa Mwalimu Nyerere ilikuwa kwa baadhi ya aliowapa dhamana ya kumsaidia katika utekelezaji. Je, Mwalimu aliwahi kulizungumza jambo hili nawe ukamsikia ? Namwuliza Mzee Nzowa.

” Huo ndio ukweli. Mimi nimekuwa katika Chama ( CCM) tangu mwaka 1956. Kadi yangu ya uwanachama wa TANU niliikatia nikiwa Mbeya. Ni Nyerere mwenyewe, kwa mkono wake, pale Mbeya, mwaka 1956 alinijazia kadi yangu ya TANU. Alianza na Kanali Ayoub Simba ikaja ya kwangu. Hata leo, ukiangalia namba za kadi ya TANU ya Kanali Ayoub Simba na ya kwangu zinafuatana. Tulikuwa bado vijana sana, na Mwalimu alifanya mwenyewe kazi ya kuhamasisha vijana kuingia TANU. Mwenzangu Ayoub yeye akaja akaingia jeshini , akafikia mpaka cheo cha Ukanali, akawa mbunge pia, kule Mafia. Yule ni kada wa siku nyingi.

Sasa kama nimepata kumsikia Mwalimu akiongea kuhusu hili la uongozi. Kwa kweli si mara moja. Nimemsikia Mwalimu akitamka, kuwa njia iliyo nzuri sana ya kumsaidia katika uongozi wake ni kwa tulio karibu na watu kumwambia moja kwa moja juu ya mazuri na mabaya wanayofanya wateule wake. Kwamba ni hatari wananchi wakianza ama kuchoka kulalamika au kuwaogopa viongozi wao. Unajua Mwalimu hakuishia tu kutumia watu wa Usalama wa Taifa, aliwatumia pia watu wa kawaida kupata taarifa sahihi.” Anasema Mzee Nzowa. Namwuliza swali lingine.

Mzee turudi kwenye kilichotokea kule Isimani, inasemekana kulikuwa na mtikisiko mkubwa hapa Iringa baada ya Dr Kleruu kupigwa risasi na Mwamwindi. Je, hali ilikuwaje hasa?

” Ni sahihi, hali ilikuwa ngumu. Wengi tuliathirika na mkasa ule, kwa namna moja au nyingine. Unajua ilifika mahali wakati ule mtu ukigongewa mlango usiku, basi, unavaa kabisa, shati, suruali na viatu, maana huenda ukifungua mlango usirudi tena kitandani kwako!”

Hivi Iringa ya wakati ule ilionekaje, unakumbuka? Namwuliza Mzee Nzowa.
” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana, wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona nina picha zipi za zamani”. Mzee Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.

Wakati tunamsubiri Mzee Nzowa na picha zake na maelezo, Jumatatu moja usiku napokea simu kutoka Uingereza;

” E bwana Maggid, niko Uingereza, nafuatilia kisa hiki cha Mwamwindi na Dr Kleruu. Mimi nilikuwa kijinini Nyang’olo wakati wa tukio lile. Ni kijiji cha jirani na alikoishi marehemu Said Mwamwindi. Nilikuwa na miaka kumi. Nakumbuka mambo mengi sana , hata Dr Kleruu nilimwona, alipenda sana kuja Nyang’olo. Sasa unasikia....” ( Simulizi hii itaendelea)

                                           CHANZO:MJENGWA BLOG

No comments: