KANISA Katoliki la Kristu Mfalme mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, limeendelea kuwaadhibu waumini wake inaodai kuwa waliisaliti imani yao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, baada ya juzi kutangaza kuwasimamisha na kuwafukuza waumini wengine 17 wa Kanisa hilo.
Kufukuzwa kwa waumini hao kuhudhuria Ibada za Misa Takatifu na kufungiwa Sakramenti zote, kunatokana na wenzao wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 400 waliopewa adhabu kama hiyo hivi karibuni na kanisa hilo kwa kinachodaiwa kuwa wameisaliti imani ya Kanisa hilo.
Majina hayo yalitangazwa wakati wa ibada ya misa ya kwanza juzi ambapo majina ya waumini hao yalikuwa yamegawanywa kwenye makundi mawili.
Kundi la kwanza ni la waumini ambao hawawezi kusamehewa na Padri yeyote isipokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Sumbawanga pekee, wakati kundi la pili ni la waumini sita ambao wamevuliwa Ukristo wao ambao hata wakitubu, hawawezi kusamehewa.
Padri aliyekuwa akiendesha misa hiyo ambaye ni Paroko Msaidizi na hakutaka kutaja jina lake huku hata waumini wakiogopa kulitaja, aliyasoma majina hayo rasmi muda mfupi kabla ya kumaliza misa.
Paroko huyo alidai shughuli hiyo ni ya kudumu kwa kuwa Kanisa liko vitani kuhakikisha linakuwa safi na si vinginevyo.
“Nasema hivi kwa kuwa siku hizi hata simu zinarekodi basi kwa wale wanaorekodi haya warekodi ni ruksa, tumepata habari kuwa hata magazeti yameanza kuandika habari hizi, nasema yaendelee tu kwani kanisa linafuata sheria na liko sahihi," alisema Padri huyo.
Hata hivyo, Paroko Msaidizi huyo hakutaja majina ya wahusika wa adhabu hizo mbili, katika uamuzi ambao tayari umezua gumzo kwa watu mbalimbali mjini hapa na katika mikoa mingine nchini.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Charles Kabanga anakusudia kukata rufaa kwa Baba Mtakatifu mjini Rome kupinga kufutwa Ukristo wake hivi karibuni.
Akizungumza na gazeti hili, Kabanga alisema anajiandaa kuuza mali yake asafiri hadi Rome kwenda kuonana na Baba Mtakatifu kupinga kuondolewa Ukristo wake na Paroko wa Kanisa Katoliki, Padri Leonard Teza ambaye ni Paroko wa Kanisa la Familia Takatifu lililopo eneo la Kizwite mjini hapa.
"Kwanza nitaonana na Kadinali Pengo (Muadhama Polycap Kadinali Pengo) na asiponirudishia Ukristo wangu, basi nipo tayari kuuza mali zangu na kufunga safari hadi Rome kukata rufaa kwa Baba Mtakatifu ambaye ndiye kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki Duniani," alisisitiza mwanasiasa huyo.
Alisema, hatua yake hiyo inatokana na adhabu hiyo kali aliyopewa na Paroko wa Kanisa likimtuhumu kutenda makosa makuu matatu ambayo ni sawa na kuisaliti imani ya Kanisa hilo.
Akifafanua, alisema Oktoba 29, mwaka huu, alikabidhiwa barua na Padri Teza ikimtaarifu kuwa amevuliwa Ukristo wake rasmi kuanzia tarehe hiyo.
Alisema anashutumiwa kwanza kumshabikia mgombea ubunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa tiketi ya CCM, Aeish Hilaly wakati akifahamu wazi kwamba ni Muislamu na alimnadi kwa kutumia dhana ya mafiga matatu ambayo mgombea huyo aliyafananisha Utatu Mtakatifu katika imani ya Kikristo.
Kosa la pili analoshutumiwa Kabanga, ni kukufuru msalaba, kwamba baada ya uchaguzi kumalizika na matokeo kutangazwa ambapo mgombea wa Chadema, Norbert Yamsebo alishindwa, wana CCM walifanya maandamano huku wakiwa wamebeba msalaba kama ishara ya kumzika mgombea huyo wa Chadema.
Tatu, alisema anashutumiwa na Kanisa hilo kwa kutukana mapadri kwamba nao wana mapungufu yao, yakiwemo kuwa na vimada ambao wamewajengea nyumba na pia kuzaa nao.
Anadaiwa pia kuwa alitukana kwamba baadhi ya watoto wa mtaani wanaorandaranda mijini hapa wamezaliwa na baadhi ya mapadri wa Kanisa hilo.
Alisema amekanusha makosa yote hayo mbele ya Padri Teza ambaye alimtaka atubu, lakini alikataa kutubu kwa kuwa hajatenda makosa hayo.
Alisema alimwambia Paroko huyo hata yeye kama angekuwa kwenye nafasi aliyonayo kama Mwenyekiti wa CCM, basi lazima wakati wa uchaguzi, angehubiri kuhusu mafiga matatu kwa kuwa CCM ilikuwa inaamini kuhusu mafiga matatu kuwa lazima achaguliwe rais, mbunge na diwani kutoka CCM na si vinginevyo.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment