Mshukuru Mungu kwa namna alivyokuumba. Wewe ni kiumbe kamili, huna upungufu wa aina yoyote, hivyo usikubali mtu mwingine aje auponde moyo wako. Hata siku moja usiruhusu mtu acheze sebene na moyo wako.
Unatakiwa kuwa wa kwanza kujihurumia kwa sababu hayupo atakayehisi maumivu kwa niaba yako. Kumruhusu mtu anayekuumiza mara kwa mara ni sawa na kutonesha kidonda ambacho ni injini ya mwili wako, Moyo!
Mapenzi ni afya yako kwa maana, ukiwa na utulivu wa kweli, hukabiliani na majeraha ya moyo mara kwa mara, unakuwa na nafasi ya kuendelea kufaidi pumzi ya uhai kwa muda mrefu zaidi.
Tatizo la upumuaji utalisikia kwa wengine. Kwamba moyo unauma mpaka ushindwe kufanya mambo mengine, itakuwa ni stori ya kufikirika. Amani kwako kwa ujazo unaotakiwa. Mapenzi ni kila kitu.
Wapenzi wenyewe huamua kutokufa mapema. Yaani endapo watakuwa na maelewano, kisha mambo madogo wanayabeba kwa udogo wake, makubwa wanayapatia ufumbuzi kabla hayajaleta athari kubwa.
Aina hii ya watu huishi kwa matumaini yasiyo na shaka yoyote. Kuugua kwao labda Malaria lakini si msongo wa mawazo unaoweza kuumiza kichwa, au udhaifu wa mwili unaosababishwa na moyo kushindwa kufanya kazi inavyotakiwa.
Kuelekea kwenye kuifanya mada yangu kuwa hai, wiki iliyopita nilichambua makundi matatu ambayo kwa namna moja au nyingine, hukaribisha maradhi ya moyo bila kupenda.
Kundi la kwanza: Mtu hana maelewano na mwenzi wake, moyo unamlazimisha atafute suluhu lakini anakuwa mbishi. Anataka kujionesha kwamba yeye yupo salama na hatishiki kwa lolote
Kundi la pili: Ipo jamii ya watu ambao hutaka jamii iwaone wao ni ngangari katika mapenzi. Yaani hawawezi kuumia hata wafanywe nini. Wanajidanganya kwa ‘ubishoo’ wao. Kuna kitu utajifunza leo.
Kundi la tatu: Wapo ambao huumizwa wao lakini kutwa kiguu na njia kutafuta suluhu. Haikatazwi kwa maana anatafuta amani ya moyo wake lakini muhimu ni je, huyo anayehangaikiwa yupo vipi?
HILI NALO LIMO
Mwepesi kuomba msamaha lakini kesho karudia yale yale. Huyu anajitesa bila sababu. Busara ni kutulia na kushika kilicho bora. Ipo mifano mingi ya watu ambao walipoteza maisha ghafla kutokana na migogoro ya kimapenzi. Tanzania pia ipo!
Kuna mwanasaikolojia aliyesema kuwa wawili wanaopendana wanaweza kuamua kutokufa mapema. Alisema kuwa mapenzi ni afya lakini moyo wenye sononeko la mara kwa mara ni kifo.
KUNA FAIDA NYINGI KUELEWANA NA MWENZIO
Mbali na suala la afya ambalo ndilo msingi wa mada hii, kuelewana na mwenzi wako hukuweka kwenye nafasi chanya ya kutofikiriwa ubaya wa aina yoyote. Nitakufafanulia kwa kituo na utaelewa.
Hujawahi kuona mtu kafumaniwa lakini mwenzi wake anaambiwa halafu anabisha? Wengine hudhani limbwata lakini ukweli upo wazi kuwa maelewano yao ndiyo husababisha isiwe rahisi kukubali.
Hajawahi kuona lolote baya kwa mwenzi wake. Wanaelewana kiasi kwamba haoni mwanya wa usaliti, ndiyo maana unapokwenda kumpa taarifa kuwa mwenzi wake anamsaliti, inabidi ujiangalie, vinginevyo atakupiga.
MUHIMU KUZINGATIA
Hakuna sifa kwako wewe kumuumiza mwenzi wako. Wala hutopewa hongera unapokuwa huelewani na mpenzi wako. Ila ni heshima, furaha na amani kuwa kwenye uhusiano usio na migogoro.
Acha hulka za kugombana kwa maana zinakusababishia matatizo mengi. Afya kwa sehemu kubwa lakini upande wa pili ni heshima yako kwenye jamii kushuka. Unapokosana na mwenzio, wanaokuzunguka hukutafsiri kwamba una matatizo.
Hasara nyingine ya kutokuwa na maelewano mazuri na mwenzi wako ni kuibiwa. Ni wako na kuna watu wanamtolea macho lakini wanashindwa jinsi ya kumpata ukiwa naye, kwa hiyo wakigundua hamna maelewano mazuri, wataanza kurusha ndoano.
Usikubali kupitisha siku moja kabla ya kupata suluhu, vinginevyo unaweza kukumbuka shuka wakati kumekucha. Itakuuma mno kugundua kwamba tayari wamemuwahi. Itakutesa katika hisia kwa sababu si ajabu baadaye utagundua umepoteza almasi, umebaki na jiwe.
Utalia kwa kusaga meno lakini majuto mjukuu. Chukua tahadhari leo, mapenzi ni afya yako lakini yanaweza kusababisha kifo chako.
No comments:
Post a Comment