Na Waandishi Wetu
SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco) limeamriwa kulipa fidia ya Sh106 bilioni kwa kampuni ya ufuaji umeme ya Dowans Tanzania Limited baada ya kuvunja mkataba.Uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), Novemba 15, mwaka huu chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhihi Swithin Munyantwali, Jonathan Parker uliamuru Tanesco iilipe Dowans kiasi hicho cha fidia.
"Jopo la wasuluhishi limeamuru zaidi ya Sh36bilioni (dola za Marekani 24,168,343) na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka inayofikia kiasi cha zaidi ya Sh 26bilioni (dola za Marekani 19,995,626) tangu Juni 15, 2010 hadi fidia hiyo itakapolipwa,’ imeeleza sehemu ya uamuzi huo.
Pia jopo hilo la wasuluhishi wa migogoro ya kibiashara liliamuru Sh60bilioni (sawa na dola za kimarekani 39,935,765) na riba ya kiasi cha asilimia 7.5 ambayo ni sawa na Sh 55bilioni (dola za Marekani 36,705,013.94) zilipwe kuanzia Juni 15, 2010 hadi wakati wa malipo.
Jopo hilo lilisisitiza kuwa ada na gharama za wasuluhishi na za utawala Sh1bilioni (dola za Marekani 750,000) kwa wasuluhishi wa ICC zinatakiwa zilipwe na pande zote husika.
"Tanesco wanatakiwa kumlipa mdai (mlalamikaji) Sh3bilioni (dola 1,708, 521) ikiwa ni gharama za uendeshaji wa kesi na gharama zingine na kwamba madai mengine yaliyotolewa na pande zote katika kesi hiyo yanatupwa.
Mpango wa kuuza mitambo hiyo uliwahi kuibua mjadala mzito nchini huku baadhi ya wabunge akiwemo mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe wakikubaliana na dhamira hiyo jambo lililosababisha serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kutangaza rasmi kuwa haina mpango wa kununua mitambo hiyo.
Kufuatia uamuzi huo Dowans iliamua kutangaza kuiuza mitambo yao nje ya nchi jambo lilosababisha serikali kuiwekea pingamizi katika Mahakama ya Biashara ikitaka wamalize kwanza masuala ya mikataba.
Siku chache baadaye Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), iliikamata mitambo hiyo kwa madai kuwa ilikuwa ikidaiwa ushuru.
Hatua ya kuiwekea pingamizi ili mitambo hiyo isiuzwe ilipigwa vikali na Dowans na kuamua kukimbilia katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court) iliyopo nchini Ufaransa ili kuhakikisha mitambo hiyo inaweza kuuzwa.
Lakini taarifa iliyotolewa na Dowans jana ilionyesha kuwa mgogoro huo umepatiwa ufumbuzi na kwamba kampuni hiyo na Tanesco sasa wamekubaliana baada ya mahakama hiyo kuketi.
“Jopo la waamuzi uliojumuisha waamuzi watatu chini ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), limetoa tunzo kuhusu mgogoro baina ya Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Limited (kwa pamoja ‘Dowans’), kwa upande mmoja dhidi ya Tanesco kwa upande mwingine.
“Dowans wameridhika na tunzo iliyotolewa na jopo hilo na kwa matokeo hayo wanayo furaha kuutangazia umma kuwa mgogoro baina yetu na Tanesco sasa umekwisha,”alisema sehemu ya taarifa hiyo.
Akizungumzia uamuzi wa kumaliza mgogoro huo baina ya Tanesco na Dowans, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja alisema hajapata taarifa hiyo rasmi wala maamuzi yaliofikia katika mahakama hiyo.
“Kwa sasa nipo nje ya ofisi kama ni kweli Mahakama hiyo imeweza kuwasuluhisha ni lazima nitaletewa taarifa na kuweza kusoma rasmi ili kujua iwapo katika makubaliano hayo suala la kuuza mitambo hiyo nalo wamekubaliana nalo au la ndio nitaweza kuzungumza chochote,”alisisitiza Waziri Ngeleja.
Waziri Ngeleja alisema kuwa anachojua yeye pingamizi la serikali lipo mahakamani na kwamba hakuna mabadiliko yoyote.
Kwa upande wa Tanesco, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alipoulizwa alisema kwa sasa Tanesco hawezi kusema chochote watatoa taarifa mara baada ya uongozi wa Tanesco kukutana.
Mara ya kwanza dhamira hiyo ya serikali kupitia Tanesco kutaka kununua mitambo ya Dowans, iliibua mjadala mkali miongoni mwa Watanzania, huku wakionyesha shaka kuhusu uamuzi huo.
Mjadala huo ulitokana na malumbano ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Shellukindo na ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma, iliyokuwa chini ya Zitto (Chadema). Kati Kamati ya Shellukindo ikisisitiza kutokuwepo umuhimu kwa Tanesco kununua mitambo hiyo.
Mvutano wa kamati hizo ulikuwa mkubwa, baada ya Zitto kusisitiza kuwa atamuomba Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuitisha mkutano wa kamati hizo mbili ili kujadili upya suala hilo na kwamba utetezi wake wa kununua mitambo hiyo unatokana na kuweka mbele maslahi ya taifa.
Wakati huo, Watanzania wengi ambao walikuwa wakitoa maoni yao kwa gazeti hili kwa njia ya simu za mkononi na katika mitandao ya ‘internet’, walionyesha kupingana katika suala hilo, jambo linaloonyesha kuwapo kwa mgawanyiko wa wazi kuhusu kununuliwa au kutonunuliwa kwa mitambo hiyo.
Kutokana na mjadala huo uliochukua mwelekeo wa kupinga ununuzi wa mitambo hiyo, hatimaye Tanesco ilitangaza kuondoa nia yake hiyo kwa kile ilichoeleza kuwa mjadala wake umechukua sura ya kisiasa kuliko kuzingatia utaalamu.
Shirika hilo lilichukua uamuzi huo siku chache baada ya Spika Sitta, kutoa mwongozo na ushauri wa kupinga nia hiyo ya Tanesco iliyopigiwa chapuo na serikali ambapo msimamo wa Tanesco ulitangazwa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake, Dk Idris Rashid, katika mkutano na waandishi wa habari ambapo alisema wameamua kuondoa nia hiyo kwa kuwa mwelekeo wa ununuzi wa mitambo ya Dowans, unalipeleka shirika hilo kwenye ugomvi wa wanasiasa, jukwaa ambalo alidai hawana mamlaka nalo.
Alisema Tanesco itaandika barua serikalini kwa Waziri wa Nishati na Madini, kumfahamisha kuhusu maamuzi hayo, ambayo yalionyesha dhahiri kuchukuliwa kwa shingo upande.
Akifafanua zaidi kuhusu mahitaji halisi ya umeme nchini na mazingira yaliyoifanya Tanesco kutaka kununua mitambo ya Dowans ili izalishe umeme wa dharura, alisema shirika hilo liliwasilisha tathmini ya hali halisi ya uzalishaji wa umeme nchini kwa wakati huo na matarajio ya uzalishaji wa umeme kwa muda wa kati na mrefu na pia mahitaji.
Alisema, Tanesco iliwasilisha taarifa kwamba hali ya ukuaji uchumi inafanya mahitaji ya umeme yaongezeke kwa megawati 75 kila mwaka na kwamba kulingana na tathmini hiyo, hivi sasa nakisi ya mahitaji ikilinganishwa na uzalishaji ni megawati 150.
Mkurugenzi huyo alibainisha ifikapo mwezi Desemba, nakisi hiyo itakuwa ni megawati 225 kwa uchache, ikiwa hapatakuwa na ongezeko lolote la uzalishaji wa umeme.
Alisisitiza pia kuwa shirika lake ilizingatia kuwa, ongezeko la uzalishaji uliotarajiwa kutoka vyanzo vya Kiwira na Tegeta, lisingesaidia kwani vyanzo hivyo visingeingia kwenye mtandao kwa muda uliokuwa umepangwa, kwa sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wa Tanesco.
Dowans ilirithishwa mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura mwaka 2006 baada ya kampuni iliyoshinda zabuni hiyo, Richmond Development Company LLC kushindwa kuleta mitambo hiyo na baadaye kukumbwa na kashfa ya ushindi wa zabuni hiyo uliosababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake na baadaye kufuatiwa na mawaziri wawili, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.
Jenereta hizo za kufufua umeme ambazo zinatumia gesi asilia zilitangazwa kuuzwa nje ya nchi kwa zaidi ya Sh101 bilioni ingawa bishara hiyo ilishindwa kufanyika baada ya serikali kuiwekea pingamizi mahakamani kampuni hiyo isiuze mitambo hiyo.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment