UWANJA wa Huba tayari upo hewani, nami nina ari na nguvu za kukupakulia kitu kipya. Ni mada ya mwendelezo inayoainisha zaidi matatizo ambayo yanaweza kusababisha kuachwa na mpenzi wako hata kama alikuwa anakupenda sana. Katika sehemu ya kwanza, tayari tumeshaanza kuona baadhi ya mambo hayo.
Kabla ya kuelekea katika sehemu ya pili ya mada yetu, kwanza napenda kuwakumbusha kwamba kitabu changu kipya cha Joseph Shaluwa…Let’s Talk About Love kipo katika hatua za mwisho kabisa kuingia mitaani.
Ndani ya kitabu hicho utakutana na mada motomoto zitakazokuweka sawa katika uhusiano wako, lakini pia utakutana na Love Messages nyingi ambazo bila shaka zinakwenda kuwa tiba ya kweli katika uhusiano wako na mpenzi wako. Hakikisha hukosi nakala yako pindi kitakapoingia mitaani.
Yap! Sasa tunarejea katika mada yetu ambayo bila shaka inabadilisha kabisa maisha yako ya kimapenzi. Kama mtakumbuka vyema wiki iliyopita nilianza kwa kufafanua kipengele cha utegemezi kwamba unaweza kuwa sababu ya kutemwa na mpenzi wako hata kama atakuwa anakupenda sana kwa kukwepa ukorofi wako.
Unajua rafiki zangu, unapokuwa mtu wa matatizo kila siku, kiukweli inafikia hatua unachosha! Kila siku una matatizo, mara leo hiki, mara kesho kile. Ni lini basi utakuwa huna matatizo? Ni kweli kabisa, kwamba kama unakuwa unamtegemea sana mpenzi wako, ni rahisi kubadilisha uamuzi wake, kwani ataona wewe ni mwanamke wa kumchuma tu na huna malengo naye na maisha ya baadaye.
Hebu sasa twende tukaone sababu nyingine. Weka utulivu wako wa akili katika mada hii, bila shaka itakubadisha kabisa.
UKOROFI...
Hili nalo ni tatizo katika uhusiano, tatizo hili linatosha kabisa kukukosesha mpenzi wa kudumu ambaye baadaye anaweza kuwa mchumba na hatimaye kuingia katika ndoa. Jichunguze vizuri je, wewe ni mkorofi? Unaufahamu vipi ukorofi? Hapa tunazungumzia dharau, majibu ya mkato na kutokuwa msikivu.
Mwanamke makini ambaye anatarajia kuingia katika ndoa hapo baadaye na mchumba wake lazima atakuwa makini na ulimi wake, hawezi kumjibu vibaya mpenzi wake kwakuwa anajua kuwa anamjibu mumewe mtarajiwa. Jichunguze vizuri, utagundua kuwa kuna tatizo hili katika uhusiano wako uliopita.
Ukorofi mwingine ninaozungumzia hapa ni kumpangia mwenza wako muda wa kuwa naye faragha, akikuhitaji muda fulani unamkataa na kutoa sababu kibao zisizo na msingi, huu ni ukorofi ni sawa na kumruhusu mpenzi wako atafute mwanamke mwingine wa nje. Unadhani akifanya hivyo na akikolezwa kimahaba, utampata tena? Hapo lazima atakuacha na utaishia kulaumu kuwa kila siku unaachika. Hii ni kati ya sababu hizo, hebu tuangalie sababu nyingine itakayoweza kukukosesha mchumba wa kudumu.
HUONESHI MAPENZI...
Naweza kusema kuwa hii ni sababu kubwa zaidi na yenye uzito wa kukukosesha mchumba wa kudumu. Huwezi kuwa na mpenzi ambaye huna uhakika kama ana mapenzi ya kweli na wewe au anakulaghai. Njia mojawapo ya kuonyesha kuwa ni kweli mpenzi wako unampenda kwa dhati ya moyo wako na siyo kujilazimisha ni kuonyesha mapenzi ya kweli.
Hebu jiulize, unaonyesha mapenzi kwa mwandani wako? Swali hili linawahusu wote, yaani wanaume na wanawake, walio ndani ya ndoa na wachumba. Sijui kama naeleweka vyema ninaposema kuonyesha mapenzi kwa mwandani wako. Hapa kuna mambo mengi ikiwemo mashamsham na kuonyesha kuwa huna kinyaa kwa mpenzi wako.
Mwingine hata kumbusu mpenzi wake inakuwa shughuli, sasa kama hata kumbusu tu mpenzi wako unashindwa, hivi wewe una mapenzi kweli? Utakuta mwingine akiwa faragha anashindwa kumridhisha vyema au hataki kushiriki na mwenzake, huyu atakuwa anahitaji nini kama siyo kuachwa?
USHAURI WA BURE
Kama ni kweli una nia ya kuwa na mume hapo baadaye, lazima utulie na uishi kwa mwanamke mwenye malengo na mapenzi ya dhati. Achana na tabia za Kiswahili, usisikilize ushauri mbaya wa marafiki. Onesha mapenzi ya kweli, mheshimu mchumba wako maana huyo ndiye anakwenda kuwa mume wako hapo baadaye.
Uamuzi wa kuolewa au kumpa mshawasha mpenzi wako wa kukuoa upo mikononi mwako na bila shaka unaweza! Kwa leo naomba niishie hapa, ila kama una maswali, ushauri au maoni, namba yangu ya simu ipo hapo juu na email yangu hii hapa chini. Hadi wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, kwa sasa ameandika vitabu vya True Love na Secret Love vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment