Patricia Kimelemeta na Hussein Issa
TAASISI ya Saratani ya Ocean Road, ina mpango wa kuleta mafundi wa kutengeneza mashine za tiba ya mionzi ya ugonjwa huo kutoka Canada.
Mafundi hao unaotarajiwa kuingia nchini katika kipindi cha wiki mbili zijazo, wanakuja kuvifanyia ukarabati, vifaa vilivyosababisha mashine hizo kuzima kwa siku mbili tofauti na kusababisha wagonjwa kushindwa kupata huduma za matibabu.
Hatua hiyo imekuja baada ya mashine mbili zinazojulikana kwa jina la Theratron, kushindwa kufanya kazi baada ya vifaa vya kupimia mionzi kuzima kutokana na kufanya kazi kwa mfululizo.
Mkurugenzi wa Huduma na Tiba wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dk Diwani Msemwa, alisema kuzima kwa vifaa hivyo kumetokana na kuzidiwa nguvu, kulikosababishwa na idadi kubwa ya wagonjwa kiasi cha kuzifanya mashine hizo kufanya kazi zaidi ya saa 24 bila kupumzishwa.
Alisema hali hiyo, imesababisha wagonjwa kushindwa kupata huduma kwa muda wa siku mbili tofauti.
Alisema, mashine hizo zina uwezo wa kutibu wagonjwa 70 hadi 80 kwa siku, lakini kwa sasa zinatibu wagonjwa zaidi ya wagonjwa 100 na kwa zaidi ya saa 24,jambo ambalo limesababisha kuzidiwa nguvu na kuzima ghafla.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment