ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 25, 2011

Jerry Muro adaiwa kutishia kuua

ALIYEKUWA Mtunza Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani, Michael Wage ameeleza mahakamani alivyotishwa na kutakiwa kutoa rushwa ya Sh milioni 10 na aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro na wenzake. 

Wage ambaye ni shahidi wa tatu katika kesi ya kuomba na kutaka kupokea rushwa inayowakabili kina Muro katika Mahaka ya Hakimu Mkazi Kisutu, akitoa ushahidi wake jana alidai kuwa alipigiwa simu na Muro aliyemweleza kuwa ana tuhuma nzito dhidi yake. 


Alidai kuwa alipokea simu hiyo akiwa Bagamoyo Januari 28 mwaka jana na Muro alijitambulisha kwake na kumueleza kuwa anamuhitaji kwa mahojiano kuhusu tuhuma hizo. 

Kwa mujibu wa madai hayo, walikubaliana kukutana kesho yake katika hoteli ya Califonia saa tano asubuhi ambako Muro alimwambia Wage ni vyema wakazungumzie tuhuma hizo katika hoteli ya Sea Cliff. 

Wage alidai Muro alimwambia kuwa katika hoteli hiyo ndiko aliko bosi wake na wakakubaliana na kwenda Sea Cliff kwa kutumia gari ya Muro na kuiacha gari yake pale pamoja na dereva wake. 

“Muro alinieleza kuwa nakabiliwa na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za na ufisadi na kwamba anaandaa kipindi cha kueleza tuhuma hizo na biashara zangu katika kipindi cha Usiku wa Habari cha TBC1,” alidai Wage. 

Wakiwa njiani, Wage alidai mbele ya mahakama hiyo akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Stanslaus Boniface, kwamba Muro alipiga simu kwa mtu ambaye hakumfahamu lakini katika maongezi yao alimtaja Wage Alidai baada ya kukata simu hiyo, alitaka Muro amtaje aliyekuwa akiongea na Muro alimjibu alikua akiongea na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambaye anahitaji kufanya naye mahojiano kabla hajafikishwa mahakamani. 

“Muro alinitishia kuwa yeye ni afisa wa jeshi na ana nyota tatu amesomea Uingereza na Marekani, alifungua dashboard ya gari na kutoa pingu, akaniambia nikileta fujo atanifunga, alinitolea na bastola na kuniambia pia ikishindikana kunidhibiti ananipiga risasi kwa kutumia bastola hiyo,” alidai. 

Kwa mujibu wa madai hayo, walipofika Sea cliff walipokewa na mtu aliyetambulishwa kwake kuwa ni Naibu Mkurugenzi wa Takukuru na jina lake moja ni Musa na wakaingia hotelini na baadaye aliingia mtu mwingine Muro akamtambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa taasisi hiyo. 

Muro anadaiwa kuwaeleza wale watu kuwa Wage ni mla rushwa mkubwa wa Bagamoyo na kwamba habari zake zitatangazwa kituo cha TBC1 na kwamba ni lazima ashitakiwe kwa kosa hilo. 

“Walinitisha kwa kuniambia kuwa sio watu wote wanaopelekwa mahakamani wana hatia, walisema Amatus Liyumba alibambikiwa kesi na rafiki yake wa BoT,”alidai. 

Alidai walimwambia atoe Sh milioni 10 ili asaidiwe ambapo alikubali na kuwaomba awapatie Sh milioni moja kwanza ambazo anazo na nyingine angewapa kesho yake na baada ya hapo aliondoka katika hoteli hiyo. 

Wage alidai alikwenda kituo cha kati cha Polisi kutoa taarifa, ambapo maofisa wa Polisi waliambatana na Karoli kwenye mgahawa wa City Gargen Januari 31 mwaka jana na kumpigia Muro aende kuchukua fedha hizo ambapo Muro anadaiwa alipofika pale na kuwaona askari alijaribu kutoroka lakini alikamatwa na kupelekwa Polisi. 

Ilidaiwa gari la Muro lilipopekuliwa lilikutwa na miwani ya Karoli, na pingu, baadaye Muro alitoa bastola aliyokuwa nayo kiunoni. Kesi hiyo inaendelea leo mahakamani hapo.



                                                                          Chanzo:HabariLeo

No comments: