ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 25, 2011

TFDA: Maduka ya dawa baridi nchini kusambaratika mwaka huu Send to a

Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo
Felix Mwagara

MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania, (TFDA) imewataka wamiliki wa maduka ya dawa baridi sehemu zilizobaki nchini kuyaboresha maduka yao kwa kuwa mwisho wa kuyabadili na kuwa maduka ya dawa muhimu ni mwaka huu.

Akizungumza jana na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo alisema mpango wa kuyabadilisha maduka ya dawa baridi na kuwa maduka ya dawa muhimu (ADDO) unatarajiwa kumalizika mwaka huu.

“Tupo nyuma ya muda, tulitakiwa tuwe tumekamilisha mpango huo mwaka huu mwezi wa kwanza, lakini kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kifedha ndiyo imesababisha kuchelewesha mpango huu, lakini kwa mwaka huu tutaukamilisha kwa kuyabadili maduka yote ya dawa baridi nchini na kuwa ya dawa muhimu,”alisema Sillo.

Pamoja na lengo hilo, Sillo alisema hadi sasa mamlaka hiyo tayari imeboresha na kubadilisha maduka ya dawa baridi katika mikoa minane ambayo ni Ruvuma, Mtwara, Rukwa, Morogoro, Pwani, Lindi, Singida na Mbeya.

Alisema pia mpango huo upo katika hatua za mwisho katika mikoa mitano ambayo ni Tanga, Kigoma, Dodoma, Shinyanga na Manyara.

Mpango huo pia Sillo alisema upo katika utekelezaji wa hatua ya awali katika mkoa wa Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Mwanza, Mara na Kagera. 

Sillo aliongeza kuwa pamoja na kuwaagiza wamiliki wa maduka ya dawa baridi kuyaboresha maduka yao ili yawe ya dawa muhimu, pia wanatoa mafunzo ya bure kwa watoa huduma wa maduka hayo, na kuwatunuku vyeti.

Alisema mafunzo ya watoa huduma hao wa maduka wanafundishwa na wataalamu wenye shahada jinsi ya kutunza na kuhifadhi dawa, mawasiliano na wagonjwa, namna ya kutoa dozi na hasara zake ikiwa haitokamilishwa au ikizidishwa.

Alisema, mafunzo hayo yanafadhiliwa kwa ushirikiano wa TFDA na Mfuko wa dunia wa kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua kikuu (Global Fund), Shirika la Misaada la Denmark (Danida), Serikali ya Tanzania na washiriki wenyewe.

Naye Meneja wa TFDA Kanda ya Mashariki, Agnes Kijo alisema mpango huo tayari umeshaanza katika Jiji la Dar es Salaam ambapo kwasasa wameanza kutoa semina ya mpango huo katika manispaa zote jijini Dar es Salaam.

“Wanaofungua maduka ya dawa baridi kiholela waache kufanya hivyo wasubiri mpango huu ukamilike ikiwa hatua za awali zimeshaanza katika Manispaa zote,”alisema Kijo.


                                                               Chanzo:Mwananchi

No comments: