ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 28, 2011

Mambo ya kuepuka unapokuwa faragha na mpenzi wako!


Wiki hii nitazungumzia mambo ambayo hutakiwi kuyafanya pale unapokuwa faragha na mwezi wako.

Nimelazimika kuandika makala haya baada ya kubaini kuwa, wapo wanaofanya mambo fulani si kwa nia mbaya lakini kwa sababu tu sehemu hiyo haistahili kuyafanya hayo, wanajikuta wametibua hali ya hewa.

Kubainisha usiyopenda ufanyiwe
Kama kuna kitu ambacho mpenzi wako anakufanyia mkiwa faragha halafu ukawa hukipendi, hutakiwi kumuambia kwa maneno bali tumia vitendo katika kufikisha ujumbe.

Kwa mfano, yawezekana mpenzi wako huwa anakoroma sana mkiwa mmelala baada ya ‘mambo flani’, usimwambie mimi sipendi unavyokoroma bali unaweza kugeukia upande mwingine bila yeye kujua kwamba, umemkwepa.

Au anakushika sehemu ambayo hupendi aishike, usikasirike na kumuambia, ‘bwana mimi sitaki’. Unaweza kumuacha kwani huwezi kufa kwa yeye kukushika sehemu hiyo.

Kulalamika
Huenda kuna mambo huko nyuma mpenzi wako aliwahi kukufanyia na hayakukufurahisha. Wakati mko faragha hutakiwi kuyagusia hayo kwani unaweza kumtoa mpenzi wako kwenye ‘mudi’ aliyokuwa nayo na kutoona ulazima wa kuendelea kuwa nawe.

Labda iwe hauko tayari mfanye chochote siku hiyo na kwamba ulitaka mkutane ili umpe ‘sure’ lakini kama ilikuwa ni siku ya kupeana furaha halafu mkakutana na kuanza kumwambia umbeya uliowahi kusikia huko nyuma kwamba anatoka na fulani, ni lazima furaha hiyo itatoweka.

Kuzungumzia mpenzi wa zamani
Ni kweli na hata yeye anajua kabla ya kuwa na wewe ulikuwa na mtu mwingine ambaye alikuwa na mazuri na mabaya yake. Utakuwa unafanya jambo baya sana kama utatumia muda wenu wa kuwa faragha kumzungumzia mpenzi wako huyo.

Hata kama ni kwa mambo mazuri, kwanini iwe hapo? Imekuaje umemkumbuka muda huo na isiwe siku nyingine? Au ni kuonesha kwamba bado yuko kichwani mwako? Endapo utakuwa ni mtu wa kumtaja mpenzi wako mara kwa mara mbele ya mpenzi wako wa sasa, utamfanya afikirie vinginevyo.

Kulaumu
Yawezekana kweli mpenzi wako anakufanyia yasiyokufurahisha lakini angalia namna ya kulaumu. Wapo wanaowalaumu wenzao na kufikia hatua a kuvuka mipaka.

‘Sasa ndiyo nini unanifanyia hivyo, mbona hata Juma hakuwahi kunifanyia hivyo? Au ndio kunidhihirishia kwamba hunipendi?’ Maneno haya anayatamka msichana mbele ya mpenzi wake.

Kulalamika huko tena kwa kutolea mifano watu wengine kutamfanya mpenzi wako ahisi huyo uliyemtaja unaamini ni bora kuliko yeye, jambo linaloweza kumtibua.

Lalamika lakini lalamika yako iwe katika lugha ya kimahaba kwani kikubwa ni kufikisha ujumbe na kumfanya abadilike.   

Kukosoa
Ni kweli siyo vibaya kumkosoa mpenzi wako lakini unadhani mkiwa faragha itakuwa ni sahihi kufanya hivyo? Mpenzi wako anatarajia mkiwa wote eneo hilo atasifiwa katika kila jambo na hapo ndipo tunaambiwa wakati mwingine kujifanyisha kunaruhusiwa.

Hivi haijawahi kutokea mpenzi wako anakufanyia jambo fulani mkiwa faragha akiamini litakufurahisha, wewe ukaona hamna kitu? Onesha kulifurahia kinafiki lakini mkiwa nje unaweza kumwambia ‘Mpenzi wangu huwa napenda sana unaponifanyia hivi lakini ukinifanyia hivi ndiyo nachanganyikiwa zaidi.

Hii itamfanya siku nyingine akufanyie kile unachokipenda zaidi. Kosoa kitaalamu ili usije ukamkwaza mpenzi wako.

Kuweka mipaka
Mpenzi wako ni mtu muhimu sana katika maisha yako. Inafikia hatua kutokana na umuhimu huo chako kinakuwa chake na chake kinakuwa chako.

Mfanye awe huru kukuambia chochote anachojisikia ilimradi kisiwe cha kukuudhi. Usimuwekee mipaka na kujiona vingine hastahili kukufanyia wala kukuambia.

Kuchomekea shida zako
Huenda una shida ambayo ulikuwa unataka mpenzi wako akusaidie lakini tambua faragha siyo mahali pa kuelezana shida zenu, hilo lisubiri wakati mko baa au sehemu nyingine.

Unajua kwanini hutakiwi kuchomekea shida zako mkiwa eneo hilo? Ni kwa sababu unaweza kumfanya mpenzi wako ahisi unataka malipo kwa kile ulichomfanyia au utakachomfanyia.

Siyo sehemu ya kumwambia mpenzi wako akununulie simu au kumweleza matatizo mengine yanayohitaji fedha, atahisi unafanya biashara hata kama katika uhalisia siyo kweli. 

Kuonesha wasiwasi
Ukiwa na mpenzi wako faragha unatakiwa kuondoa wasiwasi wote juu yake.Yawezekana kweli anavyokufanyia vinakufanya uhisi penzi lake kwako ni la kizushi lakini ukiwa naye faragha jitahidi kuepukana na hisia hizo.

Amini kwamba ni wako na hukuna mwingine mwenye nafasi kama uliyo nayo kwake. Jiulize kama kuna mwingine kwanini muda huo yuko na wewe na anakupa furaha unayoihitaji?

Kujifanya mjuaji sana
Hakika hutakiwi kuwa kama mtu uliyepitwa na wakati lakini pia usijifanye unajua kila kitu. Wakati mwingine mpe fursa mpenzi wako akufundishe hata katika kile ambacho una elimu nacho.

Kuna hali fulani atajisikia kukuelekeza kitu kuliko kuanzia mwanzo mpaka mwisho wewe ndiye kinara tu.

Mpenzi msomaji wangu, ni mengi sana ambayo unatakiwa kuyaepuka uwapo faragha na mpenzi wako lakini hayo ni kwa uchache. Kikubwa ni kuhakikisha eneo hilo linakuwa la furaha kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

Usije ukafanya jambo ambalo litamfanya mpenzi wako ajute kuwa nawe. Kila unapokutana naye hakikisha unamfanyia mambo ambayo yatalifanya penzi lenu lizidi kunoga.

Atajisikia mweye bahati kuwa na wewe lakini pia atafanya kila liwezekanalo kuhakikisha hakukosi katika maisha yake.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.

No comments: