MATOKEO ya mtihani wa kidato cha nne, uliofanyika Oktoba mwaka jana yametoka huku katika watahiniwa bora wa kitaifa, wasichana wakiongoza kwa asilimia 80 na wavulana kuambulia asilimia 20.
Matokeo hayo yanaonesha kati ya watahiniwa 10 bora kitaifa, wavulana ni wawili huku shule za seminari hasa za wasichana zikiendelea kuongoza kama ilivyo ada.
Akitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako, amesema pamoja na mafanikio hayo kwa wasichana, kiwango cha ufaulu cha jumla kimeshuka.
Mwanafunzi wa kwanza bora Tanzania ni Lucylight Mallya wa sekondari ya wasichana ya Marian mkoani Pwani akifuatiwa na wasichana wenzake Maria-Dorin Shayo (Marian) na Sherryen Mutoka (Barbro-Johansson, Dar es Salaam).
Aliyeshika nafasi ya nne kitaifa ni Diana Matabwa akifuatiwa na Neema Kafwimi wote wa St. Francis na Beatrice Issara (St Mary Goreti, Kilimanjaro).
Nafasi ya saba ndiyo iliyoshikwa na mvulana Johnston Dedani (Ilboru, Arusha) na ya nane Samwel Emmanuel (Ufundi Moshi, Kilimanjaro). Lakini nafasi za tisa na kumi zilichukuliwa na wasichana, Bertha Sanga (Marian) na Bernadeta Kalluvya (St. Francis).
Moja ya vituko vilivyofanywa na baadhi ya watahiniwa ni pamoja na kuandika matusi kwenye karatasi za kujibia mitihani.
Dk. Ndalichako alisema wanafunzi hao walitukana kwenye karatasi za Biolojia, Historia, Kemia na Jiografia na kwa kosa hilo, wanafunzi hao wamefutiwa matokeo.
Licha ya mafanikio hayo kwa wasichana yanayodhihirisha kaulimbiu kwamba mwanamke akiwezeshwa anaweza, ubora wa kufaulu kwa madaraja unaonesha watahiniwa 40,388 sawa na asilimia 11.50 wamefaulu katika madaraja ya kwanza hadi la tatu.
Kati yao, wasichana waliofaulu ni 12,583 sawa na asilimia 7.81 na wavulana ni 27,805 sawa na asilimia 14.62.
Hata hivyo, wavulana ndio waliokuwa watahiniwa wengi katika mtihani huo, kwa kuwa wasichana waliosajiliwa walikuwa asilimia 45.88 na wavulana asilimia 54.12.
Mafanikio hayo kwa wasichana ni makubwa ikizingatiwa kuwa mfumo dume umekuwa ukiwaathiri katika masomo yao, ikiwamo kupangiwa kazi nyingi za nyumbani, kuliko wavulana na pia wengi waliacha shule kutokana na mimba.
Pia katika mlinganisho wa ufaulu wa mwaka jana na mwaka huu, matokeo hayo yameonesha kiwango kushuka. Wakati mwaka jana waliofaulu walikuwa asilimia 72.51 mwaka huu ni asilimia 50.40 tu.
Hali hiyo inaonesha tatizo si shule za kata kwa kuwa matokeo hayo, kwa shule hizo ni ya pili, lakini wadau wanahusisha matokeo mabaya na uamuzi wa Serikali wa mwaka 2008 wa kuruhusu waliofeli mtihani wa kidato cha pili, kuendelea na masomo bila kurudia mtihani.
Wanafunzi wengi waliofeli mtihani wa kidato cha pili, ndio waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana na matokeo yao kuwa mabaya kuliko mwaka uliopita.
Dk. Ndalichako alisema waliofanya mtihani walikuwa 352,840 sawa na asilimia 97.04 ambapo watahiniwa 10,749 sawa na asilimia 2.96 hawakufanya mtihani huo.
Shule 10 bora kwa kigezo cha ‘Grade Point Average A=1 na F=5 zenye watahiniwa zaidi ya 40 ni Uru Seminari ya Kilimanjaro, Marian na St.Francis.
Nyingine ni Cannosa, Feza Boys na Barbro Johanson za Dar es Salaam, Msolwa ya Morogoro, St Mary Goreti ya Kilimanjaro, Abbey ya Mtwara na St Joseph Sem Iterambogo ya Kigoma.
Shule 10 bora kwa kigezo hicho pia zenye watahiniwa chini ya 40 ni seminari ya Don Bosco, sekondari ya wasichana ya Bethelsabs ikifuatiwa na Seminari ya St. Joseph- Kilocha na seminari ya Mafinga zote za Iringa.
Nyingine ni Feza Girls ya Dar es Salaam, seminari ya Maua ya Kilimanjaro, Queen of Apostles Ushirombo ya Shinyanga, seminari ya Sengerema ya Mwanza na seminari ya Dungunyi Singida.
Alisema shule 10 za mwisho zenye watahiniwa zaidi ya 40 ni sekondari za Changaa, Thawi, Hurui, Kikore, Kolo zote za Dodoma, sekondari ya Pande Darajani ya Tanga, Igawa ya Morogoro, Makata ya Lindi, Mbuyuni na Naputa za Mtwara.
“Shule 10 za mwisho zenye watahiniwa chini ya 40 ni Sanje ya Morogoro, Daluni ya Tanga, Kinangali ya Singida; Mtanga, Mipingo na Pande za Lindi; Imalampaka ya Tabora, Chongoleani ya Tanga, Mwamanenge ya Shinyanga na Kaoze ya Rukwa,” alisema Ndalichako.
Akizungumzia watahiniwa wa kujitegemea, alisema waliosajiliwa walikuwa 94,525 wakiwamo wasichana 49,252 sawa na asilimia 52.10 na wavulana 45,273 sawa na asilimia 47.90 na mwaka jana walikuwa 96,892 hivyo watahiniwa kupungua kwa 2,367 sawa na asilimia 2.44.
Alisema watahiniwa 88,586 wakiwamo wasichana 46,358 na wavulana 42,228 walifanya mitihani huku watahiniwa hao 5,939 sawa na asilimia 6.28 wakiwa hawakufanya mtihani.
Katika ufaulu ni watahiniwa 8,295 sawa na asilimia 35.17 ya waliofanya mtihani ndio waliofaulu ikilinganishwa na asilimia 28.82 ya waliofaulu mwaka jana, hivyo kiwango cha ufaulu kuongezeka kwa asilimia 6.35.
Matokeo ya watahiniwa 1,448 waliofanya mtihani bila kulipa, yamesitishwa hadi watakapolipa ada wanayodaiwa na faini katika kipindi cha miaka miwili na baada ya muda huo kumalizika, matokeo yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.
Ndalichako alisema wamesitisha matokeo ya wanafunzi wawili waliotumia sifa zinazofanana hadi wakuu wa shule watakapowasilisha nyaraka zinazothibitisha uhalali na mmoja mwenye namba S 3484/0014 kutokana na kutumia sifa za mtu mwingine hadi uchunguzi utakapokamilika.
Alisema pia Baraza limefuta na kuwaondoa katika usajili wa mitihani watahiniwa wanne wa sekondari za Kisaka na Nguvu Mpya kwa kutumia sifa za watahiniwa wengine.
Aidha, watahiniwa wengine 35 wa sekondari ya Bara wamefutiwa matokeo kwa kuwa walisajiliwa katika shule hiyo kwa kutumia majina ya watahiniwa waliochaguliwa kujiunga na shule hiyo lakini hawakuripoti.
Dk. Ndalichako alisema pia wamemfutia mwanafunzi wa sekondari ya Ludewa aliyefanya mitihani bila usajili.
Wengine waliofutiwa ni wanne wa sekondari ya Ibanda waliokuwa si wanafunzi halali wa shule hiyo na 42 walioondolewa baada ya kubainika sifa za kidato cha pili walizowasilisha hazikuwa sahihi.
“Watahiniwa wengine 56 wa kujitegemea tumewafutia matokeo baada ya kuondolewa kwenye usajili kwa kutokuwa na sifa za kufanya mtihani, lakini wakafanya mitihani katika vituo vya Mwigo Sekondari 29 na Twitange Sekondari walifanya 27,” alisema Dk. Ndalichako.
Aliongeza kuwa watahiniwa 311 wa shule na wawili wa kujitegemea, wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika kufanya udanganyifu.
Alisema Baraza pia limefuta usajili wa kituo cha watahiniwa wa kujitegemea na mba P1189 cha Biafra, Dar es Salaam, kwa kukiuka taratibu za uendeshaji mitihani.
Kituo hicho kwa mujibu wa Dk. Ndalichako kilikuwa na watahiniwa wengi kuliko uwezo wake na kusababisha usumbufu uliofanya Kamati ya Mitihani ya Mkoa kuhamishia watahiniwa katika vituo vingine bila ushirikiano wa uongozi wa kituo.
Chanzo:Habari Leo
No comments:
Post a Comment