ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 28, 2011

Wasomi: Matokeo kidato cha nne ni janga kwa taifa

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako
Fidelis Butahe na Hussein Issa
SIKU moja baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya kidato cha nne yanayoonyesha nusu ya wanafunzi kushindwa, wasomi na wadau wa elimu wameeleza kusikitishwa na hali hiyo wakisema kuwa “hili ni janga la taifa”.  Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema hali hiyo inatisha na ni hatari kwa mustakabali wa taifa, huku mmoja wao akimtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya kuchunguza matatizo ya elimu na kupendekeza njia za utatuzi wake.

Juzi Necta ilitangaza matokeo ya kidato cha nne uliofanyika Oktoba, 2010 yanayoonyesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa asilimia 22 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2009 huku wasichana wakiwa wanaoongoza kwa kufanya vizuri.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako alisema mtihani huo ulifanywa na watahiniwa 177,021 na asilimia 50.40 ya watahiniwa wote, wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 69,996 sawa na asilimia 43.47 na wavulana ni 107,025 sawa na asilimia 56.28.  “Mwaka 2009 watahiniwa waliofaulu walikuwa sawa na asilimia 72.51 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo,” alisema Dk. Ndalichako. 
Kufuatia matokeo hayo, jana Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Dk Kitila Mkumbo, alisema kuwa matokeo hayo ni janga la kitaifa na kuongeza kuwa shule ni sehemu ya kujifunza na sio mahala pa vijana kukulia.

Kwa mujibu wa msomi huyo, matokeo hayo ni kama yalitarajiwa kwa kuwa walimu wametelekezwa na mazingira yao ya kazi ni duni.  “Matokeo haya ni kama yalitarajiwa tu, walimu ni kama wametelekezwa, mazingira yao ya kazi ni duni sana, haya ndio matokeo yenyewe,” alisema Mkumbo. 

Mhadhiri mwingine chuoni hapo, Bashiru Ally alisema "Sekta ya elimu sasa imekumbwa na ugonjwa wa kuambukiza ambao kila Mtanzania ni lazima apate dawa. Hilo ni janga kwani hata kama mwanao atasoma shule nzuri na kufaulu, bado ni mtanzania na ataendelea kuishi Tanzania." 

Kwa mujibu wa Bashiru elimu nchini, imepasuka vipande viwili na imejenga matabaka ya walio nacho na watu wasionacho.  “Elimu ya Tanzania imegawanyika kati ya wenye nacho na wasio nacho, hata ukitizama shule za seminari ada yake ni kubwa mno na zipo kibiashara zaidi, ada ya mwaka mmoja kwa shule hizi ni zaidi ya  fedha anayolipa mwanafunzi anayesomea shahada ya pili (Masters) hapa chuo kikuu,” alisema Bashiru.  

Alifafanua kuwa hali hiyo inaigawa sekta hiyo kwani wanaopata bahati ya kupata elimu bora ni watoto wa wenye uwezo na kuongeza kuwa haiwezekani darasa lenye idadi  ya wanafunzi zaidi ya 100, litoe mwanafunzi bora.  “Mimi hata siku moja sikuwahi kusoma shule binafsi, nimesoma shule za serikali na tulikuwa tunafaulu vizuri mpaka tunafika chuo kikuu, lakini leo, shule hizo hizo tulizosoma zinashika mkia katika matokeo ya kidato cha nne,” alisema Bashiru.  

Alisema kuwa tatizo la kushuka kwa  ufaulu ni uwekezaji mdogo katika sekta ya elimu na hivyo akaishauri serikali kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza matatizo yanayoikumba sekta ya elimu na jinsi ya kuyatatua.  “Sio kama walimu wa kufundisha hawapo, jiulize hizi shule za binafsi zinapata wapi walimu? Mwalimu hawezi kufundisha wakati vitendea kazi hakuna na anaishi katika mazingira magumu. 

Shule ni silaha ya maisha, rais anataka kuunda tume ya katiba mpya, pia inafaa aunde tume kutazama matatizo ya elimu,” alisema.  Aliongeza, “ Tena matatizo sio kidato cha nne tu hata huku vyuo vikuu, idadi ya wanafunzi ni kubwa, utakuta mwanafunzi  anasoma hapa lakini wazazi wake hawajui mtoto wao anakula na kulala wapi. Wahadhiri nao wana matatizo yao, ndio maana nasema kuna ulazima wa kuundwa tume, sekta nzima ya elimu imekufa,”.  

Mhadhiri mwingine katika chuo hicho, Profesa Abdallah Safari alisema kuwa serikali imepuuza elimu.  “Walimu wanalipwa fedha kidogo, wanafundisha katika mazingira mabovu, vitendea kazi hakuna, idadi ya wanafunzi darasani kubwa, haya ni matunda ya kile kilichopandwa na serikali,” alisema Profesa Safari.  Kwa upande wake Dk Ndalichako alipoulizwa kuhusu kushuka kwa ufaulu hasa kutofanya vizuri kwa shule za serikali, alisema kuwa matokeo hayo ni fundisho kwa shule hizo.  

“Matokeo haya ni changamoto kwa shule za serikali. Elimu ni ushindani, zisipokuwa makini zitaendelea kuwa nyuma siku zote,” alisema Dk Ndalichako.  Juzi Dk Ndalichako, aliwaambia waandishi wa habari wakati akitangaza matokeo hayo kuwa wasichana wamefanya vizuri zaidi kuliko wavulana.  "Kati ya watahiniwa kumi bora, sita ni wasichana na wanne ni wavulana," alisema Dk Ndalichako na kumtaja kinara wa matokeo hayo kuwa ni Lucylight Mallya kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St Marian iliyopo mkoani Pwani.  Hii ni mara ya pili kwa shule hiyo kutoa mwanafunzi bora katika mtihani wa kidato cha nne baada ya Immaculate Mosha aliyeibuka kinara katika matokeo ya mwaka 2009.  

Alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 40,388 sawa na asilimia 11.50, wamefaulu katika madaraja I hadi III.  “Wasichana waliofaulu katika madaraja I hadi III ni 12,583 sawa na asilimia 7.81 na wavulana ni 27,805 sawa na asilimia 14.62,”alisema Dk Ndalichako.  Alisema idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani huo ni 46, 064 sawa na asilimia 52.09 ya waliofanya mtihani.  

Alisema katika kundi hilo, wasichana waliofaulu ni 22,405 sawa na asilimia 48.41 na wavulana ni 23,659 sawa na asilimia 56.13. Mwaka 2009 watahiniwa wa kujitegemea 49,477 sawa na asilimia 54.12 walifaulu, alisema.  Aliongeza kuwa watahiniwa 458,114 wakiwamo  wasichana 216,084 sawa na asilimia 47.17 na wavulana 242,030 sawa na asilimia 52.83 ndio waliojisajili kufanya mtihani huo mwaka jana.  

“Mwaka 2009 watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 351,152, hivyo idadi ya watahiniwa imeongezeka kwa watahiniwa 106,962 sawa na asilimia 30.5,” alisema Dk Ndalichako na kuongeza:    “Waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2010 ni 441,426 sawa na asilimia 96.36 na watahiniwa 16,688 ambao ni sawa na asilimia 3.64 ya watahiniwa wote waliosajiliwa, hawakufanya mtihani.  “Kuna ongezeko la watahiniwa wa shule 109,329 ambao ni sawa na asilimia 43.0 ikilinganishwa na idadi ya waliosajiliwa mwaka 2009. Watahiniwa waliofanya mtihani walikuwa 352,840 sawa na asilimia 97.04, watahiniwa 10,749 sawa na asilimia 2.96 hawakufanya mtihani,” alisema Dk Ndalichako.  

Alifahamisha  kuwa mwaka 2009 watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa walikuwa 96,892 na 2010 kulikuwa na watahiniwa 94,525 ikimaanisha kulikuwa na upungufu wa watahiniwa 2,367 sawa na asilimia 2.44 ikilinganishwa mwaka 2009.  “Watahiniwa 88,586 wakiwemo wasichana 46,358 na wavulana 42,228 walifanya mtihani huo, watahiniwa wa kujitegemea 5,939 sawa na asilimia 6.28 hawakufanya mtihani. 

Shule zenye watahiniwa zaidi ya 40 zilikuwa 3,194 na zenye watahiniwa chini ya 40 zilikuwa 489.  Akizungumzia matokeo ya mtihani wa maarifa (QT), alisema watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 26,540  kati yao wasichana ni 16,101 na wavulana 10,439.  

Alisema mwaka 2009 jumla ya watahiniwa 25,040 walisajiliwa kufanya mtihani huo kukiwa na ongezeko la watahiniwa 1,500,  sawa na asilimia 5.99 ikilinganishwa na mwaka 2009 na kwamba jumla ya watahiniwa 23,585, sawa na asilimia 88.87 ya waliosajiliwa walifanya mtihani huo.  

Alisema katika mtihani wa maarifa (QT) jumla ya watahiniwa 8,295 sawa na asilimia 35.17 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu ikilinganishwa na asilimia 28.82 ya waliofaulu mwaka 2009.  Alisema kuwa kiwango cha ufaulu kwa mtihani wa maarifa kimeongezeka kwa asilimia 6.35 ikilinganishwa na wamaka 2009.  “Jumla ya watahiniwa 311 wa mtihani wa kidato cha nne na watahiniwa 2 wa mtihani wa maarifa (QT) wamefutiwa matokeo yao yote ya mtihani kwa mujibu wa kifungu cha 52 (b) cha kanuni za mtihani baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu katika mtihani huo,” alisema Dk Ndalichako. 


Chanzo:Mwananchi

No comments: