MADAKTARI wamepatwa na wakati mgumu baada ya kubanwa walipokuwa wakijichanganya kutoa maelezo ya awali kuhusu watoto 10 waliokutwa wamezikwa katika shimo moja Mwananyamala kwa Kopa Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea jana katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Jordan Rugimbana katika mkutano wa waandishi wa habari na madaktari, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, Kamanda wa Polisi Kinondoni na watendaji wengine wa wilaya hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Bw. Rugimbana ilikuwa ikieleza kuwa watoto watatu walizaliwa wakiwa wafu, watoto saba walizaliwa kabla ya wakati na wote walikabidhiwa kwa wazazi kwa ajili ya maziko.
Lakini Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dkt. Sofinius Ngonyani alisema watoto watatu walizaliwa wafu na wengine saba ni mimba zilizoharibika kati ya wiki 4-6.
Kauli hiyo ilizua utata kwani walioshuhudia walisema watoto wote 10 walikuwa wakubwa na si mimba za wiki, kwani mimba zilizoharibika zenye ukubwa huo huwa haijafikia kuwa kiumbe bali huwa ni damu.
Daktari alishindwa kuendelea kutoa maelezo baada ya waandishi wa habari kuonesha dhahiri kuwa hawakuamini hadi Mkuu wa Wilaya aliamua kuingilia kati na kuinuka kutoa ufafanuzi kwa mara nyingine.
"Tusikilizane, nilivyoona mimi ni vitoto vichanga, naomba tutumie lugha za wataalamu," alisema na kuongeza kwamba wataalamu wanajua aina za watoto hao.
Hata hivyo, alisema kwa mazingira yoyote iwe mimba zilizoharibika au watoto waliokufa utaratibu uliotumika kuwazika sio unaostahili, hivyo watafanya uchunguzi kuanzia kwa wazazi wa watoto hao kumjua aliyehusika.
Aliendelea kufafanua kwamba eneo walilofukiwa watoto hao ni sehemu ya makazi na si eneo rasmi lililotengwa kwa ajili hiyo, hivyo inaonesha wazi kwamba makubaliano yalikuwa kati ya wazazi na huyo aliyekwenda kuzika watoto hao.
Alitoa mwito kwa wananchi wanaotaka kusaidiwa kuzika watoto wao kufuata mamlaka inayohusika na endepo wangefuata taratibu za hospitali badala ya njia za panya hali hiyo isingetokea.
Waandishi wa habari pia walihoji ni vipi shuka la hospitali likutwe katika shimo hilo na isijulikane nani aliyefanya hivyo.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Raphael Ndunguru alisema kutokana na mazingira yasiyoeleweka, aliamua kuunda tume ya watu watano kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.
Alisema tume hiyo itachunguza kuona kanuni na utaratibu wa hospitali zinasemaje, katika kesi ya watoto hao inakuwaje, namna maiti zilivyotoka wodini, shuka lilivyotoka chumba cha kuhifadhia maiti na kufikishwa katika shimo hilo.
"Tunatoa siku saba kuanzia leo, uchunguzi ufanyike na ripoti itolewe," alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema kazi yao ni kuchunguza waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria, ambapo wanamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa mahojiano na mwingine bado wanamsaka kwa sababu ya kuhusika na uzembe huo.
Alisema uchunguzi utakapokamilika na watuhumiwa wote kupatikana watafikishwa mahakamani na katika kufanikisha hilo wanawatafuta wenye watoto, kwani namba zao za simu zipo, ili wasaidie kumtambua aliyehusika.
Kwa upande wa wauguzi katika Hospitali ya Mwananyamala walipohojiwa kuhusiana na tukio hilo walizungumza kwa woga kwamba hali hiyo imewanyima raha na kuwafanya wanashindwe kufanya kazi.
"Kila unapopita unasikia Mwananyamala wauaji, inasikitisha sana, hospitali ilishafikia katika hali nzuri kwenye utoaji huduma lakini imeingia doa," alisema kwa unyonge na kuomba asitajwe jina gazetini sababu si msemaji.
Maiti za watoto hao zilikutwa juzi kwenye shimo katika eneo lililopembezoni mwa makaburi ya Mwanyamala kwa Msisiri B yalipo makazi ya wananchi zikiwa zimezungushiwa shuka jeupe lenye nembo ya Hospitali ya Mwananyamala.
Majina katika kanga
Majina ya wazazi wa watoto waliofukuliwa katika shimo la taka jirani na makaburi ya Mwananyamala kwa Kopa yamekutwa katika kanga zilizoviringishiwa katika miili ya watoto hao.
Kamanda Kenyela alisema majina ya wazazi hao Furaha Rajab mkazi wa Manzese, ambaye alijifungua mtoto wa kiume Januari 23, mwaka huu na kuwa na maumbile yasiyo ya kawaida
Alisema vitabu vya hospitali hiyo vinaonesha kuwa alichuliwa na baba yake aitwae Bw. Idrisa Zuberi Januari 24.
Alisema mzazi wa pili alijulikana kwa jina la Ruth Mtanga na kumbukumbu zinaonesha alijifungua mtoto wa kiume akiwa njiani kwenda hospitalini Januari 27 saa 12:00 asubuhi
Alisema kichanga hicho kilifariki baada ya kufikishwa hospitalini na kumbukumbu za chumba cha kuhifadhiwa maiti hazioneshi maiti hiyo kuingia wala kutoka.
Alimtaja mzazi mwengine ni Bi. Regina Samwel mkazi wa Kimara na kumbukumbu za hospitali hiyo zinaonesha alijifungua mtoto wa kike akiwa amekufa pia kumbukumbu za chumba za kuhifadhia maiti hazioneshi maiti hiyo kuingia wala kutoka.
Kamanda kenyela aliongeza kuwa vichanga vingine saba vilikua vimefungwa kwenye shuka yenye mandishi ya hospitali hiyo wodi namba IA lakini hazina kumbukumbu zozozote zinazoonesha kuwa wamezaliwa na kufa katika hospitali hiyo.
Aliongeza kuwa polisi na madaktari walifika eneo la tukio na kuchunguza vichanga hivyo na kungundua vimezaliwa vikiwa na miezi saba hadi tisa, maiti zimehifadhiwa katika hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi.
Imeandaliwa na Gladness Mboma, Kulwa Mzee na Nassra Abdulla
Source: Majira
No comments:
Post a Comment