ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 2, 2011

Dowans wapingwa rasmi mahakamani


HATIMAYE Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu(LHRC) kwa kushirikiana na mashirika 16 ya wanaharakati wametimiza azma yake ya kupinga nia ya serikali kuilipa fidia Kampuni ya ufuaji wa umeme wa dharura ya Dowans.


Novemba 15, mwaka jana Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhishi Swithin Munyantwali, Jonathan Parker iliamuru Tanesco iilipe Dowans fidia ya Sh.94 bilioni kwa kuvunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Kufuatia uamuzi huo, Januari 25 mwaka huu Dowans iliwasilisha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam maombi ya usajili wa tuzo yake hiyo kupitia kwa Wakili wake Kenedy Fungamtama, ili ulipwaji wa fidia yake hiyo ufanyike kisheria.




Maombi hayo ya Dowans yatari yameshasajiliwa na kupewa namba ya usajili madai namaba 8 ya mwaka 2011 na tayari yameshapangiwa jaji wa kusikiliza maombi yake hayo.

Lakini jana LHRC kwa niaba ya mashirika hayo mengine ya wanaharakati waliwasilisha rasmi pingamizi hilo mahakamani hapo pingamizi hilo wakianisha hoja za msingi saba kupitia Kampuni ya uwakili ya South Law Chambers Advocates.

Sambamba na hoja hizo wanaharakati hao wanaiomba Mahakama hiyo isiisajili tuzo hiyo ya Dowans na pia itamke kuwa tuzo hiyo haikuwa sahihi.

Mbali na LHRC katika pingamizi hilo wengine waliojisajili ni Timu ya Wanasheria wa Mazingira na Kampuni ya Sikika linaloshughulika na haki za jamii za Kiuchumi nchini.

Wajibu pingamizi hilo ni pamoja na Dowans Tanzania Limited, Dowans Holdings South Africa Limited na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).

Katika hoja ya kwanza ya pingamizi hilo wanaharakati hao wanadai kuwa hawakuridhika na tuzo hiyo iliyotolewa na ICC kwa Dowans kwa kuwa mjibu pingamizi wa tatu(Tanesco) ni shirika la umma linalomilikiwa na serikali ya Tanzania.

Wanadai kuwa ingawa linaendeshwa kwa pesa za zinazotokana na huduma zake lakini pia sehemua ya pesa za kulindesha zinatokana na Watanzania walipa kodi.

Katika hoja ya pili wanadai kuwa hakuna mkabata wa kisheria uliofungwa baina ya Tanesco na kampuni ya Dawans uluiosababisha kuwepo kwa mgogoro ulioilazimu ICC kutoa tuzo hiyo kwa kampuni hiyo.

Sambamba na hoja hiyo wanaharakati hao wameambatanisha na mkataba baina ya Tanesco na Kampuni ya Richmond ambao Dowans iliurithi, unaodaiwa kuwa na mashaka kisheria, kama kielelezo.

Hoja ya tatu wanadai kuwa chini ya Sheria za Tanzania mkataba na tuzo hiyo kwa Dowans ni batili na umejaa dosari za kisheria.

Katika hoja ya nne wanaharakati hao wanadai kuwa chini ya Sheria za Tanzania kampuni ya Richmond haikuwa na nguvu ya kisheria kuingia mkataba na Serikali ya Tanzania au na Tanesco kwa niaba yake ambao unaweza kutekelezwa.

Wanaharakati hao wametia nguvu hoja yao hiyo kwa kuambatanisha na kielelezo cha taaridfa ya matokeo ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wake.

Wanaharakati hao wanadai katika hoja yao ya tano kuwa kutokuwepo kwa mkataba hai kati ya Richmond na Tanesco jukuimu lilitakiwa kutekelezwa na wajibu pingamizi wa kwanza na wa pili ambalo ndilo lilisababisha kutolewa kwa tuzo hiyo ni batili.

Hivyo kwa mazingira hao wanaharakati haso katika hoja yao hiyo wanadai kuwa tuzo hiyo iliyotolewa na ICC haiwezi kukubaliwa wala kutekelezwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Hoja ya sita ya pinagmizi hilo wanaharakati hao wanadai kuwa tuzo hiyo ilitolewa hata kabla ya mgogoro mwingine katika Mahakama nyingine Houston nchini Marekani baina ya Richmond na Dowans Tanzania Limited juu ya umiliki wa mashine za kuzalishia umeme, ambazo zinahusiana na tuzo hiyo.

Katika hoja ya saba ya pingamizi hilo wanaharakati hao wanadai kuwa maombi ya usajili wa Tuzo iliyotolewa na ICC ambayo yamewasilishwa Mahakama Kuu haupaswi kukubaliwa kwa kuwa imetokana na mkataba batili baina ya Richmond na Tanesco.

Wanaharakati hao wanasisitiza kuwa mkataba huo ulifikiwa kinyume cha manunuzi ya umma, kinyume cha sheria na kunyume cha sera ya umma.

Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema ambaye ndiye mshauri mkuu wa serikali kwa masuala ya kisheria, imeshatangaza kuridhia kuilipa kampuni hiyo fidia hiyo kwa madai kuwa imeridhika na hukumu hio kuwa ni ya sahihi.

Hata hivyo nia hiyo ya serikali ambayo ilirudiwa na Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, imezua mjadala mkubwa huku wasomi wa fani mbalimbali wakiwemo wanasheria, wanasiasa na wanaharakati wakipinga malipo hayo kuwa ni batili,

Miongoni mwa Watanzania wanaopinga malipo hayo ni pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samweli Sitta ambaye anadai kuwa serikali kuilipa Dowansa fidia hiyo ni sawa na kuhujumu uchumi wa nchi.

Source: Mwananchi

No comments: